Showing posts with label Picha. Show all posts
Showing posts with label Picha. Show all posts

Monday, 29 January 2018

Serikali Haitambui Wahuni

Wakati unaokubalika ni sasa. Ukijitambulisha utatambulika, usipojitambulisha hutatambulika. Serikali haitambui wahuni.

Wednesday, 13 December 2017

Dodge Ram

Dodge Ram, gari la majambazi wa Kolonia Santita, lililohusika katika utekaji nyara wa mpelelezi mashuhuri wa Tume ya Dunia kutoka Israeli Daniel Yehuda, lililokuwa na watu saba ndani, liliisindikiza teksi iliyombeba Yehuda; toka Uwanja wa Ndege wa Copenhagen, hadi Msitu wa Mfalme wa Kangelunden, karibu na Ukumbi wa Kimataifa wa Bella Center, huko TÄrnby, jijini Copenhagen.

Saturday, 9 December 2017

Kwa Nini Biblia Imejaa Mafumbo?

Kwa nini Biblia imejaa mafumbo? Biblia imejaa mafumbo kwa sababu akili za watu bado hazijakomaa kuupokea ukweli. Yesu na waandishi wote wa Biblia waliongea na kuandika kimafumbo, ili Neno la Mungu lijidhihirishe lenyewe kiroho katika mawazo ya mtu.

Friday, 8 December 2017

Shetani na Uumbaji

Lengo kuu la Shetani kuingilia uumbaji wa Mungu kwa kutumia Succubus na Incubus ni kumzuia Yesu asirudi kwa mara ya pili. Anajua akiingilia uumbaji huo na kuwafanya watu wote wawe na roho za kishetani, wokovu hautakuwa na maana, Yesu hatakuwa na mtu wa kumwokoa atakaporudi kwa mara ya pili.

Yesu alikuwa binadamu ili afe kama binadamu kwa ajili ya binadamu. Alikufa msalabani ili sisi wote tuokoke. Lakini Shetani hataki hilo litokee. Akiingilia uumbaji wa Mungu toka tumboni mwa binadamu, binadamu atakayezaliwa hatakuwa na uwezo wa kuongoka. Atakuwa na roho ya jini itakayomjua Shetani badala ya kumjua Mungu. Hivyo kurudi kwa Yesu kwa mara ya pili hakutakuwa na maana, kwa sababu hakutakuwepo na mtu wa kuokolewa.

Hata hivyo, toka mwaka 1995 watu wengi walianza kuamka kiroho dunia nzima; na mwaka 2012 waliamka zaidi, pale ulimwengu ulipoanza kuhama kutoka kwenye masafa ya ngazi ya nne ya ufahamu wa binadamu (‘4th dimension’) kwenda kwenye masafa ya ngazi ya tano ya ufahamu wa binadamu (‘5th dimension’) inayohusika zaidi na ulimwengu wa roho na ambayo bado inaendelea kuhama mpaka dakika hii. Ndiyo maana watu wengi zaidi wanamjua Mungu kipindi hiki kuliko kipindi kingine chochote kile katika historia ya dunia yetu. Kwa sababu hiyo, Shetani hatashinda.

Sunday, 3 December 2017

CS-Miami

CS-Miami ni tawi la Kolonia Santita nchini Marekani. Lina watu katika miji mikubwa 78 ya Marekani, kuanzia Miami mpaka New York – mpaka Los Angeles, California. Linaongozwa na Moreno Morales, ‘El Chupacabra’, au ‘Zimwi’, mkimbizi kutoka Meksiko anayeishi Miami kinyume cha sheria toka mwaka 1988.

Pichani ni jiji la Miami, Florida; na jumba la Morales lililotaifishwa na Tume ya Dunia mwaka 1993, baada ya Operation DC kukamilika rasmi jijini Oslo.

Tuesday, 14 November 2017

Mwanasesere wa Nyoka wa Lisa Graciano

Mwanasesere wa nyoka wa Lisa Graciano, rafiki kipenzi wa Debbie, aliyeokoa maisha ya John Murphy huko Xochimilco (‘Sochimiliko’) – Mexico City.

Debbie na Lisa walitoa mchango mkubwa katika vita ya Tume ya Dunia na Kolonia Santita huko Meksiko; lakini bila Mwanasesere wa Nyoka John Murphy angeuwawa, na Kolonia Santita wangeishinda Tume ya Dunia.

Tuesday, 7 November 2017

Sanduku la Samsonite


Sanduku la Samsonite lililotumiwa na jambazi wa Kolonia Santita Roger Prideux, jambazi wa CS-Paris, kubebea bomu lililoisambaratisha ndege ya Shirika la Ndege la Ufaransa “Flight 279”, kama ilivyoelezewa katika kitabu cha “Kolonia Santita”.

Wednesday, 1 November 2017

CS-Moscow

CS-Moscow, tawi la Kolonia Santita lililotawala huko Urusi na katika nchi za Ulaya ya Mashariki kama vile Belarusi, Moldova na Ukraini; na katika baadhi ya nchi za Ulaya ya Kusini kama vile Masedonia, Montenegro, Uturuki na Ugiriki, liliongozwa na mwanajeshi wa zamani wa “Red Army” Dmitri Olegushka. Aidha, Olegushka alikuwa mwanachama hai wa zamani wa genge hatari zaidi la kimafia duniani liitwalo Solntsevskaya Bratva.

Dmitri Olegushka alikuwa na umri wa miaka 42 mwaka 1992, wakati Operation DC ikitekelezwa duniani kote, na alipigana dhidi ya Tume ya Dunia mwanzo hadi mwisho akiwa nchini Urusi. Olegushka hakuwa na umbo kubwa. Alikuwa mfupi. Alikuwa na nywele fupi nyeusi, uso mpana usiokuwa na ndevu na kitambi kidogo kilichomkaa vizuri. Alikuwa na mke na watoto wawili; na alishirikiana na Arina Gaidar, Tesak Anatoly-Chaika, Nikolay Narochnitskaya na Nakita Sergei Kerensky, kuendesha CS-Moscow. Nakita maana yake ni mtu aliyeshindikana kutekwa, lakini alitekwa nyara.

Mke wa Olegushka aliitwa Paviella. Paviella alishirikiana na mumewe kuendesha CS-Moscow, na msururu wa biashara nyingi za kimafia; wakishirikiana na magenge ya kimafia kama vile Solntsevskaya Bratva, Yamaguchi Gumi, Camorra, ‘Ndrangheta, na Sinaloa ya Amerika ya Kaskazini.

Saturday, 28 October 2017

CS-Copenhagen

Copenhagen; jiji kubwa kuliko yote katika nchi za Skandinavia na mji mkuu wa Denmaki; Makao Makuu ya Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya – WODEC; na makao makuu ya tawi kubwa kuliko yote ya Kolonia Santita duniani, CS-Copenhagen.

CS-Copenhagen ilikuwa na mamlaka katika nchi za Baltiki kama vile Estonia, Lativia na Litwania; Skandinavia kama vile Denmaki, Swideni, Norwe na Aisilandi; Ulaya ya Kaskazini kama vile Denmaki, Estonia, Ufini, Aisilandi, Ayalandi, Lativia, Litwania, Norwe, Swideni na Uingereza; na baadhi ya nchi za Ulaya ya Kati kama vile Uswisi, Ujerumani, Hungaria na Polandi.

CS-Copenhagen ilikuwa na viongozi wafuatao: Regner Steiner Valkendorff “The Storm” au “Kimbunga” (kwa sababu alipeperusha watu); Ida Taico “Weasel Girl” Nidhug; Marcus Overgaard “The Don”; Karen Karlsen; Ulla Wagner “Death Queen”; Banke Mohamed, na Peter Honore mwenye asili ya Ufaransa.

Valkendorff aliiendesha CS-Copenhagen kwa muda wa miaka mitatu na nusu, kabla ya kuuwawa kwa MP5 ya John Murphy huko Meksiko mwaka 1992. Regner, ambaye jina lake humaanisha “shujaa mwenye hekima”, alikuwa na umri wa miaka 38. Alizaliwa mwaka 1954, Machi 16. Hadi kifo kinamkuta, alikuwa na rafiki wa kike na watoto wawili kwa mke wake wa zamani.

Baada ya kifo cha Valkendorff huko San Antonio, Mexico City, CS-Copenhagen ilisambaratishwa rasmi na WPD. WPD (“WODEC Police Department”) ni Idara ya Polisi ya Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya, yenye mamlaka ya kikatiba katika nchi 143 za WODEA. WODEA (“World Drugs Enforcement Administration”) ni Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya na Ugaidi wa Kimataifa Duniani.

Tuesday, 24 October 2017

CS-Bissau

Bissau, mji maarufu katika bara la Afrika, kitovu kikuu cha biashara ya madawa ya kulevya katika bara la Ulaya, makao makuu ya CS-Bissau.

CS-Bissau, Tawi la Kolonia Santita la Ginebisau na nchi zote za Afrika ya Magharibi na Kaskazini isipokuwa Moroko ambayo iko katika kanda ya Ulaya, inaongozwa na jambazi sugu wa Ginebisau Aregado Midana. Midana ana umri wa miaka 51. Alizaliwa Jumapili ya tarehe 8/3/1941. Ana wake watatu, watoto tisa na wajukuu wawili.

Aregado Midana alikamatwa na kufungwa maisha nchini Ginebisau mwaka 1993, baada ya operesheni ya kung’oa mizizi ya Kolonia Santita duniani kote kukamilika.

Sunday, 22 October 2017

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Benito JuĂĄrez, Mexico City

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Benito JuĂĄrez wa Mexico City ni uwanja wa ndege mkubwa kuliko vyote Mexico City, na uwanja wa ndege wa nyumbani wa Kolonia Santita. Maelfu ya vidae (‘mules’) wa Kolonia Santita hupitia hapo kila mwezi kusafirisha madawa na fedha – kwenda na kurudi nje na ndani ya Mexico City.
 
Kolonia Santita, kwa kutumia wasafirishaji wadogowadogo wa madawa ya kulevya wanaojulikana kwa lugha ya kigeni isiyo rasmi kama ‘mules’ (vidae – Kamusi ya Enock Maregesi), husafirisha maelfu ya kilo za madawa ya kulevya kila mwezi; kila kidae akiwa na kilo moja au zaidi tumboni mwake (au ndani ya sanduku lake).
 
Saa arobaini na nane kabla ya Vijana wa Tume ‘kutua’ Mexico City, viwanja vyote vya ndege vya Mexico City – vikiwemo vyote viwili vya Benito JuĂĄrez – vilidhibitiwa vikali na majeshi haramu ya Kolonia Santita ya ‘autodefensa’ na ‘sicarios’, hadi waliposhtuliwa na simu ya katibu muhtasi wa Panthera Tigrisi Maria Cosillas Ortega. Mtu mmoja ‘aliyefanana’ na John Murphy alikuwa ofisini kwa El Tigre akitafuta nyaraka za siri, katika mazingira ambayo Maria hakuyaelewa.
 
Sehemu nyingi za Mexico City zikiwa zimedhibitiwa vikali kwa bunduki hatari za Kirusi za AK-74 na AK-47, na za Kibelgiji za FNP90 zenye uwezo wa kutoboa kinga ya risasi, wanajeshi wa Kolonia Santita walikuwa wakijidanganya (sana) kuwasubiri Vijana wa Tume katika viwanja vya ndege. Kwa mbinu za WODEC-Intelligence na FAM, Vijana wa Tume waliingia Mexico City usiku wa manane – kama wagonjwa mahututi kutoka Guadalajara.

Thursday, 19 October 2017

Manukato Kutoka Ufaransa

Manukato kutoka Ufaransa aliyotumia Mtoto wa Rais wa Meksiko Debbie Patrocinio Abrego katika chumba chake cha kifahari katika Ikulu ya Meksiko ya Los Pinos, Paloma Picasso, Mpelelezi wa Tume ya Dunia John Murphy Ambilikile alipomtembelea, baada ya kutoka katika Jangwa la Simba la Desierto de Los Leones la Mexico City pamoja naye, ni manukato kwa ajili ya wanawake makini duniani kote.

Tuesday, 17 October 2017

Mgogoro wa Palestina na Israeli Ulianzishwa na Israeli Mwenyewe

Eneo la kihistoria la vita visivyokwisha kati ya Wayahudi na Waarabu, kati ya Israeli na Palestina, Ukanda wa Gaza, Mpelelezi wa Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya Daniel Yehuda kutoka Kidon (Kitengo cha Mauti na Utekaji Nyara cha Shirika la Kijasusi la Mossad la Israeli) alipokuwa akitekeleza operesheni maalumu ya Jeshi la Israeli katika mji wa Khan Younis – faksi ya Oslo ilipofika Givat Ram, katika ofisi za Tume ya Dunia jijini Jerusalem.

Ukanda wa Gaza ni jimbo lenye miji minne na kambi mbalimbali za wakimbizi za Umoja wa Mataifa – lenye urefu wa kati ya kilometa 41 au maili 25 na lenye upana wa kati ya kilometa 6 mpaka 12 au maili 3.7 mpaka 7.5, pamoja na eneo la jumla la kilometa za mraba 365 au maili za mraba 141.

Jimbo hili liliwahi kutawaliwa na Wamisri, Wakanaani, Waisraeli, Wasiria, Wababelonia, Wagiriki, Warumi, Waturuki, Waingereza, na Wapalestina, na limekuwa uwanja wa vita kwa karne nyingi kwa sababu za kidini na kihistoria. Ukanda wa Gaza uko chini ya Palestina. Uko chini ya serikali ya Hamas.

Mpelelezi wa Tume ya Dunia Daniel Yehuda kutoka Israeli alikuwa Khan Younis (ambako alikwenda kutuliza ghasia) wakati faksi ya Oslo kutoka kwa Kamishna U Nanda ilipofika ofisini kwake Givat Ram, Jerusalem, ikimtaka aondoke haraka ilivyowezekana kwenda Rangoon na Copenhagen; kuonana na Kamishna Meja Jenerali U Nanda wa Asia-Australia na Rais wa Tume ya Dunia Boidin Versnick, kwa mfuatano huo. Alisafiri. Lakini kwa sababu ya uzembe alioufanya huko Rangoon, Yehuda alisababisha watu wengi (wenye hatia na wasiokuwa na hatia) kufa katika Machafuko ya Sheraton jijini Copenhagen.

Kama ilivyo Alaska kwa Marekani au Kaliningrad kwa Urusi ndivyo ilivyo Gaza kwa Palestina, katikati ya Mto Yordani na Bahari ya Mediterania.

Palestina ni nchi ya Waisraeli waliyopewa na Mungu wa Yakobo. Hata hivyo, hawakutimiza masharti. Mungu aliwaagiza kuua kila mtu katika nchi ya Kanaani na miji yake yote. Waisraeli, wakiongozwa na Yoshua, waliua watu wengi katika nchi ya Kanaani. Hawakuua kila mtu katika miji ya Ashdodi, Gathi na Ukanda wa Gaza kama walivyoagizwa.

Mungu alimwambia Ibrahimu kuwa angempa yeye na uzao wake nchi ya Kanaani kuwa milki yao ya milele, na kuwa Yeye ndiye angekuwa Mungu wao daima. Vita ya Israeli na Palestina itamalizwa na Mungu. Itamalizwa na hekima.

Mungu alilibariki taifa la Israeli katika misingi ya kidini na si katika misingi ya kisiasa au misingi ya kihistoria; na asili ya dini ya Kikristo ni kutoka katika taifa hilo ambalo Biblia imelitaja kama Taifa Teule la Mwenyezi Mungu.

Lakini mgogoro wa Palestina na Israeli ulianzishwa na Israeli mwenyewe. Yakobo (Israeli) alipokea baraka iliyokuwa si ya kwake kwa kutumia hila ya Rebeka. Baraka ya Yakobo ilikuwa ya Esau.

Jitihada za Kizionisti za kuifanya Palestina kuwa Kanaani ya zamani hazitafanikiwa bila hekima!

Friday, 13 October 2017

Jiji la Jerusalem

Mpelelezi wa Tume ya Dunia kutoka Jerusalem, Israeli, Kanali Daniel ‘Yehuda Ben-Asher’ Ebenezer, Daniel Yehuda, alikuwa komandoo wa kitengo cha mauti na utekaji nyara cha Shirika la Kijasusi la Mossad la Israeli (Kidon) kabla ya kujiunga na Kikosi Maalumu cha Kikomandoo cha Tume ya Dunia (EAC) huko Oslo, kwa makubaliano maalumu kati ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) na Shirika la Kijasusi la Mossad la Israeli.

Mpelelezi wa Tume ya Dunia kutoka Israeli Daniel Yehuda Ben-Asher Ebenezer, Mhebrania aliyeishi Givat Ram, Jerusalem, na mke wake mrembo Hadara na mtoto wake mzuri Navah Ebenezer, alikuwa Ukanda wa Gaza siku alipopigiwa simu na Kiongozi wa Kanda ya Asia-Australia ya Tume ya Dunia U Nanda – kutoka Copenhagen kuhusiana na wito wa haraka wa kuonana na Rais wa Tume ya Dunia.

Yehuda aliondoka usiku huo kwenda Yangon, Myama, ambapo alionana na U Nanda na kupewa maelekezo yote ya kikazi aliyotakiwa kuyafuata. Mbali na maelekezo hayo, Nanda alimkabidhi Yehuda kachero wa Kolonia Santita Mandi Dickson Santana (bila kujua kama Mandi ni kachero wa Kolonia Santita) ili amsindikize mpaka stendi ya mabasi ya Maubin, nje ya jiji la Yangon.

Baada ya hapo Yehuda alisafiri mpaka Copenhagen ambapo yeye na wenzake walikabidhiwa Operation Devil Cross, operesheni ya kung’oa mizizi ya Kolonia Santita duniani kote.

Yehuda alifanya kosa kubwa kuonana na kachero wa Kolonia Santita Mandi Santana! Kwa sababu hiyo, sauti na picha ya Yehuda vilichukuliwa, watu wengi walikufa katika miji ya Copenhagen na Mexico City.

Wednesday, 11 October 2017

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mingaladon-Yangon

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mingaladon-Yangon, Myama. Kamishna Jenerali U Nanda wa Kanda ya Tume ya Dunia ya Asia-Australia aliondokea hapo kuelekea Copenhagen, ambapo alikwenda kuhudhuria Kikao cha Dharura cha Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya.

U Nanda (Nanda kwa sababu alizaliwa siku ya Jumamosi pembezoni mwa mto huko Bama), Kamishna wa Kanda ya Asia-Australia ya Tume ya Dunia na kachero wa zamani wa KGB aliyeasi, ndiye aliyekuwa wa mwisho kufika Copenhagen kabla ya Kikao cha Dharura cha Tume ya Dunia kuanza.

Nanda ana historia kubwa kulinganisha na makamishna wengine wa tume, kwani yeye ni mhanga mkubwa wa madawa ya kulevya; hususan baada ya kumpoteza binti yake mpendwa Ma Nang Nyi, na ‘mkwe’ wake kipenzi Ko San Pe, kwa dawa ya kulevya ya heroini (shumuya – Kamusi ya Enock Maregesi) mwaka 1980 na 82 kwa mpangilio huo, na kutafutwa na KGB (shirika la zamani la ujasusi la Urusi) kwa usaliti wa shirika hilo dhidi ya Umoja wa Mataifa.

Wednesday, 4 October 2017

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Guadalajara, Jalisco, Meksiko

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Guadalajara, Jalisco, Meksiko. Ndege ya Vijana wa Tume, Grumman Gulfstream IV, ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Guadalajara saa saba usiku CST kutokea Copenhagen; Vijana wa Tume wakaingia Mexico City saa kumi alfajiri CST, katika mazingira ya kutatanisha.

Kamanda wa Jeshi la Polisi la Tume ya Dunia Kanda ya Amerika ya Kaskazini Meja Jenerali Sebastian Alejandro, na maafisa sita wa WODEC-Intelligence kutoka Mexico City, alikuwepo na wenzake katika Uwanja wa Ndege wa Guadalajara huko Jalisco kuwapokea Vijana wa Tume, kwa amri ya Jeshi la Anga la Meksiko (‘Fuerza AĂ©rea Mexicana’) na Idara ya Usalama ya Tume ya Dunia, alipewa jukumu la kuwaingiza Vijana wa Tume jijini Mexico City kwa magari ya SUV na ‘ambulance’ kama wagonjwa mahututi.

Katika nyumba yao ya siri waliyopewa na Jeshi la Anga la Meksiko, Calle Gante, CuauhtĂ©moc (tamka ‘Kwauteimak’), katikati ya Mexico City, Vijana wa Tume walipata ugeni wa ghafla kama walivyoelezwa na Mkurugenzi wa Usalama wa Tume ya Dunia Christoffer Sortevik huko Copenhagen.

Mmoja wa wageni hao (Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Meksiko (PGR) Virgilio Santo Graciano, Mkuu wa Jeshi la Polisi Meksiko (PJF) Demetrio Vega del Castilo, Kiongozi wa Kanda ya Amerika ya Kaskazini ya Tume ya Dunia Kamishna Profesa Randall Buchanan Ortega wa Marekani, Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya Marekani (DEA) Baxter Salvatore Sincere, na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu (CNDH) Daktari Santiago Luis-Fernando) alikuwa kibaraka wa Kolonia Santita, ingawa alikuwa kibaraka wa Kolonia Santita kwa shingo upande.

Wageni hao (viongozi wakubwa katika vita dhidi ya madawa ya kulevya duniani) walikwenda kuwajulia hali Vijana wa Tume na kuwapa hali halisi ya usalama ya Mexico City na ya Kateli ya Kolonia Santita; lakini miadi ya Vijana wa Tume na Debbie na Lisa (mtoto wa rais na mtoto wa naibu mwanasheria mkuu wa Meksiko kwa mpangilio huo) kesho yake katika Baa ya Desierto de Los Leones huko San Ángel, ilibadili kabisa historia ya Kolonia Santita na ya Tume ya Dunia.

Friday, 29 September 2017

Toyota Corolla

Gari jipya la Kiongozi wa Kanda ya Afrika ya Kusini ya Tume ya Dunia Kamishna Profesa Justin Mafuru wa Tanzania – Bosi wa John Murphy – Toyota Corolla, lililotumika kumbeba profesa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi Barabara ya Samora, katika ofisi za Kanda ya Afrika ya Kusini ya Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya jijini Dar es Salaam.

Mohammed Nafi, Mkurugenzi wa Sekretarieti ya Kanda ya Afrika ya Kusini ya Tume ya Dunia, alikuwa na faksi yenye utata mkubwa kutoka Oslo; iliyomtaka kamishna asafiri usiku huo kwenda Copenhagen kuonana na Kamishna Mkuu wa Tume ya Dunia.

Kamishna Profesa Justin Mafuru, profesa wa fizikia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kinara wa mionzi ya gama, ‘gamma rays pioneer’, aliyekuwa akiiwakilisha Tanzania katika shirika la utafiti wa kinyukilia la bara la Ulaya (CERN) nchini Uswisi, alikuwa mlemavu. Mguu wake wa kushoto ulikuwa mwembamba na mfupi kulinganisha na wa kulia, kwa sababu ya ugonjwa wa polio alioupata katika mwongo wa kwanza wa maisha yake akiwa na umri wa miaka saba. Kwa hiyo alitembea akichechemea.

“Kamishna … karibu,” alisema Nafi huku akisimama na kutupa gazeti mezani na kuchukua karatasi ya faksi, iliyotumwa.

“Ahsante. Kuna nini …”

“Kamishna, imekuja faksi kutoka Oslo kama nilivyokueleza – katika simu. Inakutaka haraka, kesho, lazima kesho, kuwahi kikao Alhamisi mjini Copenhagen,” alisema Nafi huku akimpa kamishna karatasi ya faksi.

“Mjini Copenhagen!” alisema kamishna kwa kutoamini.

“Ndiyo, kamishna … Sidhani kama kuna jambo la hatari lakini.”

“Nafi, nini kimetokea!”

“Kamishna … sijui. Kwa kweli sijui. Ilipofika, hii faksi, kitu cha kwanza niliongea na watu wa WIS kupata uthibitisho wao. Nao hawajui. Huenda ni mauaji ya jana ya Meksiko. Hii ni siri kubwa ya tume kamishna, na ndiyo maana Oslo wakaingilia kati.”

“Ndiyo. Kila mtu ameyasikia mauaji ya Meksiko. Ni mabaya. Kinachonishangaza ni kwamba, jana niliongea na makamu … kuhusu mabadiliko ya katiba ya WODEA. Hakunambia chochote kuhusu mkutano wa kesho!”

“Kamishna, nakusihi kuwa makini. Dalili zinaonyesha hali si nzuri hata kidogo. Hawa ni wadhalimu tu … wa madawa ya kulevya.”

“Vyema!” alijibu kamishna kwa jeuri na hasira. Halafu akaendelea, “Kuna cha ziada?”

“Ijumaa, kama tulivyoongea wiki iliyopita, nasafiri kwenda Afrika Kusini.”

“Kikao kinafanyika Alhamisi, Nafi, huwezi kusafiri Ijumaa …”

“Binti yangu atafukuzwa shule, kam …”

“Nafi, ongea na chuo … wambie umepata dharura utaondoka Jumatatu; utawaona Jumanne … Fuata maadili ya kazi tafadhali. Safari yako si muhimu hivyo kulinganisha na tume!”

“Sawa! Profesa. Niwie radhi, nimekuelewa, samahani sana. Samahani sana.”

Kwa nini Mohammed Nafi alitaka kusafiri kwenda Afrika Kusini wakati akitoa taarifa za kikao cha dhararu kwa Justin Mafuru? Pata jawabu la swali hilo hapa:

Tuesday, 26 September 2017

Maabara ya Methi

Maabara ya kutengenezea madawa hatari ya kulevya kuliko yote duniani yaitwayo methamfetamini au hielo. Mwaka 2013 wale wanawake wawili wa Kitanzania waliokamatwa nchini Afrika Kusini kwa tuhuma za kusafirisha methamfetamini, hawakuwa na methamfetamini, walikuwa na dawa inayotumika kutengeneza methamfetamini.

Methamfetamini (methi) huweza kutengenezwa nyumbani. Mbolea ya amonia (‘ammonium fertilizer’ ), na lithi (‘lithium’), kutoka ndani ya betri za kawaida kwa mfano, huwekwa ndani ya chupa ya kawaida ya soda na kuifunika. Kemikali zinapofanya kazi hutoa si tu methi, lakini pia fukizo (‘fumes’); lakini ambazo zina uwezo wa kulipuka.

Hielo ni tofauti na kokeini kwa sababu inaunguza. Humfanya mtumiaji ajisikie raha ya kupindukia, nguvu, na makini! Mtumiaji huweza kukaa kwa saa ishirini na nne kwa siku bila lepe la usingizi, anaweza kufanya kazi kwa wiki nzima au wiki mbili bila kupumzika.

Methi huvutwa kwa kutumia buruma (‘pipe’) inayomlewesha mtumiaji kwa haraka na vizuri zaidi.

Matokeo mabaya ya baadaye ya utumiaji wa madawa haya ya ajabu ni pamoja na matatizo makubwa ya afya ya akili, na ukosefu kabisa wa hamu ya kula na kulala. Unaweza kujisikia kama vile unataka kuurarua uso wako wote! Kujikinga na dalili za namna hiyo, waathirika hulazimika kuvuta hielo zaidi.

Kukosa usingizi ni kubaya. Ukizidi kukaa kwa muda mrefu bila kulala, mwishowe utaugua ugonjwa unaitwa ‘matatizo ya akili ya wasiwasi’ (‘severe paranoid psychosis’).

Kama shumuya (heroini), ukitumia hielo utajisikia raha ya kupindukia. Raha unayoipata kwa kukuvuta hielo ni zaidi ya asilimia 1200 ya raha unayoipata kwa kuvuta bangi, heroini na kokeini kwa pamoja.

Kwa kawaida watu huanza kuvuta hielo baada tu ya saa sita za usiku, muda ambao watu wengi wamelala. Ukishavuta, au kujidunga, utataka buruma nyingine, utataka tena kujidunga. Kisha utafanya mambo ya ajabu kama kusafisha nyumba hadi asubuhi.

Dozi kubwa ya hielo huweza kusababisha kiharusi, maruweruwe, ugonjwa wa moyo, na hata kifo.

Soma zaidi hapa: http://bit.ly/methamfetamini

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...