Friday, 29 September 2017

Toyota Corolla

Gari jipya la Kiongozi wa Kanda ya Afrika ya Kusini ya Tume ya Dunia Kamishna Profesa Justin Mafuru wa Tanzania – Bosi wa John Murphy – Toyota Corolla, lililotumika kumbeba profesa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi Barabara ya Samora, katika ofisi za Kanda ya Afrika ya Kusini ya Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya jijini Dar es Salaam.

Mohammed Nafi, Mkurugenzi wa Sekretarieti ya Kanda ya Afrika ya Kusini ya Tume ya Dunia, alikuwa na faksi yenye utata mkubwa kutoka Oslo; iliyomtaka kamishna asafiri usiku huo kwenda Copenhagen kuonana na Kamishna Mkuu wa Tume ya Dunia.

Kamishna Profesa Justin Mafuru, profesa wa fizikia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kinara wa mionzi ya gama, ‘gamma rays pioneer’, aliyekuwa akiiwakilisha Tanzania katika shirika la utafiti wa kinyukilia la bara la Ulaya (CERN) nchini Uswisi, alikuwa mlemavu. Mguu wake wa kushoto ulikuwa mwembamba na mfupi kulinganisha na wa kulia, kwa sababu ya ugonjwa wa polio alioupata katika mwongo wa kwanza wa maisha yake akiwa na umri wa miaka saba. Kwa hiyo alitembea akichechemea.

“Kamishna … karibu,” alisema Nafi huku akisimama na kutupa gazeti mezani na kuchukua karatasi ya faksi, iliyotumwa.

“Ahsante. Kuna nini …”

“Kamishna, imekuja faksi kutoka Oslo kama nilivyokueleza – katika simu. Inakutaka haraka, kesho, lazima kesho, kuwahi kikao Alhamisi mjini Copenhagen,” alisema Nafi huku akimpa kamishna karatasi ya faksi.

“Mjini Copenhagen!” alisema kamishna kwa kutoamini.

“Ndiyo, kamishna … Sidhani kama kuna jambo la hatari lakini.”

“Nafi, nini kimetokea!”

“Kamishna … sijui. Kwa kweli sijui. Ilipofika, hii faksi, kitu cha kwanza niliongea na watu wa WIS kupata uthibitisho wao. Nao hawajui. Huenda ni mauaji ya jana ya Meksiko. Hii ni siri kubwa ya tume kamishna, na ndiyo maana Oslo wakaingilia kati.”

“Ndiyo. Kila mtu ameyasikia mauaji ya Meksiko. Ni mabaya. Kinachonishangaza ni kwamba, jana niliongea na makamu … kuhusu mabadiliko ya katiba ya WODEA. Hakunambia chochote kuhusu mkutano wa kesho!”

“Kamishna, nakusihi kuwa makini. Dalili zinaonyesha hali si nzuri hata kidogo. Hawa ni wadhalimu tu … wa madawa ya kulevya.”

“Vyema!” alijibu kamishna kwa jeuri na hasira. Halafu akaendelea, “Kuna cha ziada?”

“Ijumaa, kama tulivyoongea wiki iliyopita, nasafiri kwenda Afrika Kusini.”

“Kikao kinafanyika Alhamisi, Nafi, huwezi kusafiri Ijumaa …”

“Binti yangu atafukuzwa shule, kam …”

“Nafi, ongea na chuo … wambie umepata dharura utaondoka Jumatatu; utawaona Jumanne … Fuata maadili ya kazi tafadhali. Safari yako si muhimu hivyo kulinganisha na tume!”

“Sawa! Profesa. Niwie radhi, nimekuelewa, samahani sana. Samahani sana.”

Kwa nini Mohammed Nafi alitaka kusafiri kwenda Afrika Kusini wakati akitoa taarifa za kikao cha dhararu kwa Justin Mafuru? Pata jawabu la swali hilo hapa:

No comments:

Post a Comment

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...