Thursday, 22 June 2017

Simama Juu ya Mabega ya Mapandikizi ya Watu

Msamaha si kwa ajili ya watu wenye mabawa ya kuku, ni kwa ajili ya watu wenye macho ya tai.

Macho ya tai yana nguvu mara nne zaidi ya macho ya mwanadamu. Tai ana uwezo wa kuona hadi umbali wa kilometa themanini bila matatizo yoyote. Ana uwezo wa kuruka hadi futi elfu kumi, na ana uwezo wa kukimbia hadi mwendokasi wa kilometa mia moja na ishirini kwa saa.

Kihekima, wale tu wanaoweza kuona mbali kama tai ndiyo watakaouweza msamaha. Lakini wale wenye mabawa ya kuku, wale ambao hawawezi kuruka wala kuona mbali, watapata taabu sana kuijua radhi. Kwa hiyo, wanapaswa kukua. Ukiwa mnyenyekevu wa moyo hutamchukia adui yako.

Msamaha si jambo dogo. Watu wadogo, watu wenye uwezo mdogo wa kufikiri, hawawezi kupambana na changamoto za msamaha. Msamaha ni kwa ajili ya watu wenye macho kama ya tai wanaoweza kuona mbali ambao wako tayari kushindwa vita ili washinde vita.

Hewa inaingia ndani ya mapafu na kutoka; chakula kinaingia ndani ya mwili na kutoka; mwanamasumbwi anapigana bila kugombana; injini ya gari haiwezi kusukuma gari mbele au nyuma bila kutoa hewa katika paipu ya ekzosi. Lakini kile kinachoingia moyoni mwako hakitoki! Maumivu yanapoingia ndani ya moyo yanapaswa kutoka nje kama yalivyoingia kwa sababu, yasipotoka yatatengeneza sumu ndani ya moyo wako na yatatengeneza sumu ndani ya roho yako pia.

Sumu hiyo itahatarisha safari yako ya mbinguni na Mungu hatakusamehe tena. Badala ya yule aliyekukosea kuumia, utaumia wewe uliyekosewa. Yesu anaposema samehe saba mara sabini hatanii. Usiposamehe, hutasamehewa.

Tuesday, 20 June 2017

African Potential

Kitabu cha KOLONIA SANTITA kilisomwa juzi huko Japani katika mkutano wa AFRICAN POTENTIAL katika Chuo Kikuu cha Osaka. Shukrani tele zimfikie Onoda Fuko.

Monday, 19 June 2017

Neema ya Mwenyezi Mungu


230. CV yako si maisha yako. Shahada yako si maisha yako. Maisha ni magumu kuliko mtu yeyote anavyoweza kufikiria.

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe anasemekana kuwa rais msomi zaidi kuliko wote duniani. Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini anasemekana kuwa rais asiye msomi zaidi kuliko wote duniani. Lakini wote ni marais wa nchi. Kusoma sana si kubaya, lakini hakuna mtu atakayefanikiwa katika maisha yake mpaka Mungu aamue. Mafanikio katika maisha hayategemei umesoma mpaka wapi, mafanikio katika maisha yanategemea neema ya Mwenyezi Mungu.

Kukosa elimu lisiwe jambo la kukukatisha tamaa; kukosa elimu si mwisho wa maisha. Mike Kidima alisema, “Nakata tamaa kukata tamaa.” Usikate tamaa, hata pale utakapokuwa umechoka, kabisa. Usitarajie kabisa kukata tamaa katika maisha, utakapokata utakata baraka.

Sunday, 18 June 2017

Mapazia ya Dhahabu ya Taffeta

Mapazia ya dhahabu ya Taffeta kutoka Italia, katika chumba cha Mtoto wa Rais wa Meksiko Debbie Patrocinio Abrego, pamoja na samani za Gianni Versace na mapambo ya Frida Kahlo, ni miongoni mwa vitu vilivyomfurahisha John Murphy katika Nyumba ya Debbie katika Ikulu ya Meksiko ya Los Pinos.

Chumba cha kulala cha Debbie Patrocinio kilikuwa na thamani ya dola za Kimarekani milioni moja. Kilikuwa na samani za wabunifu wa kimataifa. Kilikuwa na jumla ya vyumba vinne! Kilikuwa na kitanda kikubwa cha hadhi ya kifalme, makochi ya kumeremeta, kompyuta, zulia nene jipya jeupe, mapazia ya dhahabu ya Taffeta, kofia ya taa ya dhahabu (‘chandelier’, ‘shandalia’) ya Baccarat, na kadhalika.

Vitu vyote vya ndani ya Nyumba ya Debbie vilikuwa vya Debbie, alivyonunuliwa na wazazi wake. Samani zote zilizokuwemo kabla baba yake Debbie hajawa Rais, mwaka 1988, ziliondolewa kwa ajili ya Debbie.

Babaye Debbie alipomaliza muda wake kama Rais wa Meksiko mwaka 1994 mapazia ya Debbie ya Taffeta yaliondolewa ikulu kwa ajili ya familia nyingine ya Rais wa Meksiko, aliyefuata baada ya Patricinio Abrego.

Mapazia ya Taffeta yanapatikana hadi leo hii. Ya Debbie, hata hivyo, yalishabadilishwa.

Wednesday, 14 June 2017

Sikujui

Sikujui. Lakini naamini hungependa kuishi maisha yako hapa duniani bila kuacha urithi au kumbukumbu ya aina yoyote katika jamii. Zifuatazo ni ngazi tano muhimu zitakazofanya uache dunia katika hali nzuri kuliko ulivyoikuta: Tambua vitu vya muhimu katika maisha yako ijapokuwa unaweza kuacha alama katika dunia bila kujitambua baada ya kuondoka; tumia kipaji ulichopewa na Mungu; fanya kazi kwa bidii na maarifa; shindana na wenzako kuwa juu zaidi katika tasnia uliyojichagulia; kuwa makini na kila kitu unachofanya kwa maana ubongo ni kitu cha ajabu, ubongo una uwezo wa kukupotosha.

Ukitambua vitu vya muhimu katika maisha yako hapa duniani na kuvipa kipaumbele cha kwanza, ukatumia kipaji ulichopewa na Mungu na ukafanya kazi kwa bidii na maarifa, halafu ukashindana na wenzako kuwa juu zaidi katika tasnia uliyojichagulia, ukafanya kila kitu kwa makini ukihofia maamuzi ya ubongo wako, utaacha urithi kwa faida ya vizazi vijavyo. Kuwa na akili, kuwa na uwezo wa kujiwekea malengo, kuwa mchapakazi hodari. Namna hiyo, hakuna kitakachoweza kushindikana.

Tuesday, 13 June 2017

CALLE GANTE, CUAUHTÉMOC, DISTRITO FEDERAL, MEXICO CITY

Calle Gante (Mtaa wa Gante), Cuauhtémoc (‘kwauteimak’), Mexico City, ndipo Vijana wa Tume walipofikia kutokea Uwanja wa Ndege wa Guadalajara; wakiwa na magari makubwa matatu, SUV, ya WODEC-Intelligence, na gari la wagonjwa la Jeshi la Anga la Meksiko (FAM – ‘Fuerza Aérea Mexicana’).

Nyumba ya Vijana wa Tume (‘safe house’; miongoni mwa nyumba nne sehemu mbalimbali za Mexico City) namba 1081 – iliyokuwa na vyumba vinne vya kulala, mabafu sita, chumba cha silaha, chumba cha mazoezi, jiko, sebule, bwawa la kuogelea, na ukuta mrefu mweupe kuzunguka nyumba nzima – ilikuwa kubwa ya ghorofa mbili mali ya FAM.

Nyumba ya siri ya Vijana wa Tume ilipaswa kuwa ya siri, lakini siku ya kwanza Murphy na Mogens walipoonana na Lisa Graciano – katika Baa ya Los Leones huko San Ángel – nyumba yao iligundulika.

Lisa ndiye aliyesababisha nyumba ya Vijana wa Tume kugundulika, na gari lao kupigwa kombora, licha ya gari lake kubadili historia ya Tume ya Dunia.

Monday, 12 June 2017

Tujivunie Kiswahili Chetu

229. Kiingereza kilipanda meli na ndege kutoka Uingereza kuja Afrika Mashariki. Tujivunie Kiswahili chetu.

Kiingereza kililetwa na wakoloni wa Kiingereza kutoka Uingereza na walikitumia katika masuala yote ya kiutawala ya Afrika Mashariki. Kililetwa pia na wamisionari waliojenga shule na kuwafundisha Kiingereza wanafunzi na walimu na watu wengine wa kawaida, kwa lengo la kuwasaidia katika kazi yao ya kueneza dini kama wakalimani, hivyo kufanya Kiingereza kienee zaidi kuliko Kiswahili.

Lakini Kiswahili kilizaliwa Afrika Mashariki. Kwa nini hatuithamini lugha yetu? Kwa nini hatuzithamini lugha zetu za makabila? Kwa nini hatuipendi na kuitetea lugha yetu ya taifa ambayo ndiyo lugha ya biashara na mawasiliano ya Afrika Mashariki? Kwa nini hatuvitetei vizazi vijavyo kwa kuvitetea vizazi vya leo?

Wajerumani, hata hivyo, wakati wa utawala wao waliruhusu Kiswahili kiwe lugha halisi ya taifa nchini Tanzania kwa vile hawakukiongea Kiingereza wala hawakukipenda. Ndiyo maana Kiswahili kinazungumzwa zaidi nchini Tanzania kuliko Kenya au Uganda.

Hata wamisionari, hasa wamisionari wa Kiprotestanti, hawakukitumia Kiingereza katika kueneza dini kwa sababu hadhira yao isingewaelewa. Badala yake walitumia lugha za makabila ya Kiswahili, hivyo kujikuta wakieneza zaidi utamaduni wa Kiswahili kuliko wa Kiingereza au Kijerumani.

Hutaweza kukamilika kama hujui utamaduni wa kwenu. Lazima tujifunze kuipenda na kuitetea lugha yetu kwa faida ya vizazi vijavyo.

Saturday, 10 June 2017

Jitambue Uishi

Siri ya mafanikio yako ni chumba chako. Dali linasema anga ndicho kipimo cha kufikiria. Dirisha linasema utazame nje uone fursa zilizopo ulimwenguni.

Feni linasema uwe mtulivu usikurupuke kufanya lolote. Kalenda inasema uwe mtu anayekwenda na wakati.

Kioo kinasema ujitazame na ujiamini kabla ya kutenda lolote. Kitabu cha dini kinasema unapaswa kumwamini Mungu ili uishi.

Kitanda kinasema ujifunze kuwa na mapumziko. Mlango unasema usipitwe na fursa ya aina yoyote ile hapa ulimwenguni.

Saa inasema kila sekunde ina thamani sana katika maisha yako hivyo tumia muda wako vizuri.

Amka, fumbua macho, uujue ukweli.

Friday, 9 June 2017

Milima ya Sierra Madre Occidental


Milima ya Sierra Madre Occidental iliyoko Tijuana, Baja California, Meksiko, ndipo Kiongozi wa Kolonia Santita Panthera Tigrisi alipokuwa amejificha kabla na baada ya mauaji ya Meksiko. Baadaye Panthera Tigrisi alihamishwa kutoka Baja California hadi Oaxaca, katika kasri la Mkurugenzi wa Usafirishaji wa Kolonia Santita Eduardo Chapa de Christopher, ambapo aliendesha kikao cha dharura cha Bodi ya Wakurugenzi ya Kolonia Santita, kilichohusu udhibiti wa Tume ya Dunia nchini Meksiko na duniani kwa jumla.

Thursday, 8 June 2017

Kafara ya Maombi

Ukitaka kujua maana halisi ya maisha yako kuwa tayari kufanya vitu vikubwa vitakavyohitaji nguvu ya Mungu kuvikamilisha - na kudumu katika maisha hayo kwa kafara ya maombi.

Vitu vikubwa kabisa katika maisha uhitaji nguvu ya Mungu kuvikamilisha - kwa kujifunza kushukuru badala ya kuomba wakati wa matatizo. Kushukuru wakati wa matatizo ni kafara ya maombi.