Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mingaladon-Yangon, Myama. Kamishna Jenerali U Nanda wa Kanda ya Tume ya Dunia ya Asia-Australia aliondokea hapo kuelekea Copenhagen, ambapo alikwenda kuhudhuria Kikao cha Dharura cha Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya.
U Nanda (Nanda kwa sababu alizaliwa siku ya Jumamosi pembezoni mwa mto huko Bama), Kamishna wa Kanda ya Asia-Australia ya Tume ya Dunia na kachero wa zamani wa KGB aliyeasi, ndiye aliyekuwa wa mwisho kufika Copenhagen kabla ya Kikao cha Dharura cha Tume ya Dunia kuanza.
Nanda ana historia kubwa kulinganisha na makamishna wengine wa tume, kwani yeye ni mhanga mkubwa wa madawa ya kulevya; hususan baada ya kumpoteza binti yake mpendwa Ma Nang Nyi, na ‘mkwe’ wake kipenzi Ko San Pe, kwa dawa ya kulevya ya heroini (shumuya – Kamusi ya Enock Maregesi) mwaka 1980 na 82 kwa mpangilio huo, na kutafutwa na KGB (shirika la zamani la ujasusi la Urusi) kwa usaliti wa shirika hilo dhidi ya Umoja wa Mataifa.
No comments:
Post a Comment