Showing posts with label Mengineyo. Show all posts
Showing posts with label Mengineyo. Show all posts

Friday, 16 March 2018

COSOTA

Nimekamilisha usajili wa Kolonia Santita katika idara mbalimbali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; kama vile BASATA, COSOTA, COSTEC, Maktaba ya Kihistoria ya Makumbusho ya Taifa, Maktaba Kuu ya Taifa, na Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, kwa ajili ya utafiti na vizazi vijavyo.
 
Wasilisha nakala ya kazi yako kwa mujibu wa sheria. Taifa ni mataifa. Ukitambuliwa na taifa utatambulika kimataifa.
 
Kabla hawajakupiga kwa sheria wapige kwa kujisajili.

Friday, 9 March 2018

Taabu ya Yakobo

Irani itakapoipiga Israeli, kama ambavyo imeshaahidi, Israeli itajibu mapigo. Kwa vile Israeli ina nguvu zaidi kuliko Irani, itaipiga Irani kwa silaha za kawaida. Itaipiga hata kwa silaha za kinyukilia pia.

Kutunisha misuli, Irani itaomba msaada wa kijeshi kutoka katika nchi za Kiarabu; ambazo zitakubali kuingilia kati na kuisaidia Irani. Kwa silaha za kawaida, bado nchi zote za Kiarabu zitakazokubali kuisaidia Irani hazitakuwa na uwezo wa kuishinda Israeli. Kuishinda itabidi zitumie silaha za kinyukilia.

Silaha za kinyukilia zitakapoanza kutumika, Marekani itaingilia kati kuisaidia Israeli. Marekani itakapoingilia kati kuisaidia Israeli, Urusi itaingilia kati kuisaidia Irani. Ufaransa, Uingereza na Ujerumani zitaingilia kati kuisaidia Israeli; huku China ikiingilia kati kuisaidia Irani. Hapo Vita Kuu ya Tatu ya Dunia itaanzishwa rasmi.

Katika vita hiyo ya kinyukilia na mbaya kuliko vita zote zilizowahi kupiganwa, Israeli itashinda vita na itaanzisha utawala wa Mpinga Kristo duniani kote. Kutakuwa na dini moja. Kutakuwa na serikali moja. Kutakuwa na sarafu moja. Watu watapungua hadi kufikia milioni 500, kama ilivyokuwa mwaka 1650, asilimia 7 ya idadi ya watu wote ya leo.

Wafuasi wa Yesu Kristo watapata taabu kubwa ambayo haijawahi kutokea. Yeyote atakayempinga Mpinga Kristo, yeyote atakayepinga utawala wa Mpinga Kristo, atakiona cha mtema kuni. Watu wengi watauwawa kwa sababu ya ufuasi wao kwa Masihi. Wale watakaokuwa na talanta ya kuhubiri watauwawa kinyama, hadharani, ili liwe fundisho kwa wafuasi wengine wa Yesu Kristo.

Miongoni mwa wale watakaokuwa wanahubiri injili ya kweli ya ufalme wa Mungu bila woga wa aina yoyote ile, atakuwemo Eliya na Enock. Eliya na Enock Mungu aliwachukua bila kuonja mauti, kama akiba, kwa sababu ya kipindi hicho cha Taabu ya Yakobo.

Eliya na Enock wataibuka ghafla jijini Yerusalemu na kuanza kuhubiri injili ya kumpinga Mpinga Kristo. Kwa vile hawataogopa chochote, wala hawatamwogopa yeyote, serikali ya Israeli itawakamata na kuwatesa lakini hawatanyamaza.

Mpinga Kristo atakapoona imeshindikana kuwanyamazisha, Eliya na Enock, huku akitamba kwamba yeye ndiye Yesu Kristo ambaye kila mtu ndiye aliyekuwa akimsubiri arudi kwa mara ya pili; na kwamba yeye anatoka katika ukoo wa mfalme Daudi, ili watu waamini kama kweli yeye ndiye Yesu Kristo, ataamuru Eliya na Enock wauwawe hadharani kama wahubiri wengine.

Eliya na Enock watakapouwawa, Mungu atawafufua na watarudi mbinguni wakiwa wameonja mauti kama binadamu mwingine yeyote yule. Hapo mlango wa rehema utakuwa umefungwa. Muda wowote kuanzia hapo Yesu atarudi, kwa mara ya pili, na kwa ajili ya ufufuo wa kwanza.

Watakatifu wote watanyanyuliwa na wataondoka pamoja na Yesu kuelekea mbinguni, kwa ajili ya ziara ya miaka 1000 katika ulimwengu wa roho; kuanzia dunia ya kwanza ya ulimwengu huo iitwayo Asiyah hadi ya mwisho iitwayo Adam Kadmon, katika mji mpya wa Yerusalemu.

Baada ya milenia, kipindi hicho huku duniani Ibilisi akiwa kifungoni na malaika wake, binadamu wote wenye dhambi wakiwa wamekufa, Yesu na watakatifu wote atarudi kwa ajili ya ufufuo wa pili; na kama mfalme wa ulimwengu wote milele.

Wenye dhambi watafufuliwa na wataungana na Ibilisi kuipiga Yerusalemu Mpya itakayokuwa inang'inia hewani, huku Yesu na watakatifu wote wakiwa hawana silaha yoyote; lakini vilevile wakiwa hawapigwi kwa silaha yoyote.

Shetani atakapoonekana kushindwa, Yesu atawasha ‘kibiriti cha kiroho’. Mafuta yote yaliyopo ardhini dunia nzima yatalipuka na kugeuza ardhi yote kuwa ziwa la moto, na hivyo wenye dhambi wote kupata aibu ya milele.

Katika Biblia kuna tabiri 333 kuhusu maisha ya Yesu Kristo, na kuhusu kurudi kwake kwa mara ya pili. Kati ya hizo, 332 zilitimia! Bado mmoja tu: Kurudi kwa Yesu Kristo kwa mara ya pili.

Unadhani huo wa kurudi kwa Yesu Kristo kwa mara ya pili hautatimia? Muda umefika. Jitathmini katika maisha yako na uchague lililo jema.

Enock Maregesi

Saturday, 4 November 2017

Taabini ya Bibi Martha Maregesi: 2017

Taabini hii ni ngumu sana kwangu kuandika pamoja na kwamba ni miaka mitatu kamili toka giza liingie. Mwaka 2014, Novemba 4, nilimpoteza bibi yangu mpendwa, Martha Maregesi, aliyefariki dunia kutokana na ukongo wa kiharusi, na tutamkumbuka daima.

Alikuwa na roho ya kipekee; na kifo chake kiliwagusa wengi, pamoja na kwamba aliishi maisha kamili, zaidi ya siku 25550, siku 5110 zaidi, ambazo ndizo tulizopangiwa na Mungu.

Mapenzi ya mtu kwa bibi yake ni mapenzi ya kipekee. Nadhani Mungu aliwapa mabibi wote uwezo maalumu wa kuwapenda wajukuu zao, na kufanya maisha yao yatimie, kuwafanya wawe binadamu wazuri na wenye maadili mema.

Alichangia pakubwa katika malezi yangu ya utotoni; na aghalabu naweza kukumbuka nikiwa naye jikoni akipika, huku mimi nikifanya kazi nyingine, lakini wakati huohuo akinifundisha mambo kadha wa kadha ya kunikomaza kimaisha. Bibi hakuwa tu bibi. Alikuwa mlezi, rafiki na mtu aliyenihamasisha sana katika maisha.

Kifo kinaleta huzuni lakini kinaleta tumaini. Naamini bibi yangu atakwenda mbinguni, kwa sababu naamini alitubu dhambi zake akisaidiwa na wachungaji. Wachungaji hao walimtembelea kila siku, nyumbani au hospitalini, akiwa kitandani kwake akiugua. Bibi yangu alitimiza wajibu wake. Alizaliwa, aliishi, na alikufa katika toba.

Siku nitakapokufa ningependa kuzikwa jirani na alipozikwa bibi yangu, ili Yesu atakaporudi tufufuke pamoja.

Tuesday, 20 June 2017

African Potential

Kitabu cha KOLONIA SANTITA kilisomwa juzi huko Japani katika mkutano wa AFRICAN POTENTIAL katika Chuo Kikuu cha Osaka. Shukrani tele zimfikie Onoda Fuko.

Saturday, 13 May 2017

UHAKIKI WA KITABU CHA IF ALL YOU HAVE IS ONE SONG SING IT LOUD CHA NYAMAGESA LABAN

If All you Have is One Song, Sing it Loud, kama ulichonacho ni wimbo mmoja uimbe wimbo huo kwa sauti kuu, chenye kutuhamasisha kujua sisi ni nani, kilichoandikwa na mwandishi-mhamasishaji Nyamagesa Laban, kinatusaidia kujua sisi ni nani na kwa nini tulizaliwa.

Kinatufundisha upekee, kwamba kila mtu ni wa kipekee, na ukishaijua talanta inayokufanya uwe tofauti na wengine ipiganie talanta hiyo kwa nguvu zako zote, na kupitia upekee huo wasaidie na wengine.

Kwa jumla kitabu hiki kinahusu fursa. Una bahari ya fursa ya kuwa kitu chochote unachotaka kuwa katika dunia hii. Kama unataka furaha, furaha iko ndani yako. Kama unataka utajiri, utajiri uko ndani yako. Kama unataka amani, amani iko ndani yako. Kama wewe ni tone na fursa ni bahari, wewe ni bahari ndani ya tone. Ni jukumu lako sasa kutafuta ndani kile kilichowekwa na Mungu kwa ajili ya maisha yako.

If All you Have is One Song, Sing it Loud ni kitabu cha uhamasishaji chenye jumla ya sura 9, faslu 33 na kurasa 60 zinazotuhimiza kubadilika iwapo tunataka kufika kwenye kadari za maisha yetu.

Zinatuhimiza kubadilika kifikra, kitabia, kimyenendo, kiimani na kimtazamo, lakini hapohapo kinatukanya kwamba mabadiliko hayo si kazi rahisi; kwani yana changamoto zake, lakini changamoto hizo ndizo zitakazotukomaza na kutukamilisha. Hivyo hatuna budi kuzigundua changamoto zetu na kupambana nazo, huku tukijua kuwa bila changamoto hizo hatutaweza kufanikiwa.

Kitabu hiki kimefanikiwa kwa mambo mengi. Kimefanikiwa kufikisha ujumbe wake kwa hadhira. Kwamba sababu mojawapo inayofanya watu wasifanikiwe ni woga wa kushindwa na kwamba dawa ya woga huo ni kukabiliana na woga wenyewe kwa ukweli na uwazi juu ya tatizo lililokupata, huku ukiendelea na maisha yako pamoja na kwamba umeumia.

Kimefanikiwa katika sura ya tano kutukumbusha kuwa maono ya taswira chanya za ndani katika fikra huweza kumsaidia mtu kufanikiwa katika maisha yake na kwamba sura ya tano ndiyo siri kubwa ya mafanikio kuliko zote katika kitabu hiki.

Usiseme huwezi kufanya jambo kwa sababu unaweza. Furahia maisha ya sasa usingoje ya kesho na ya jana yalishapita; na mafanikio si pesa, mafanikio ni utimizaji wa malengo yako pesa itafuata baadaye. Katika sura ya saba kitabu hiki kimefanikiwa pia kuhimiza mawasiliano na ushirikiano katika kazi.

Lakini hakuna kitabu chochote cha kilimwengu kilichokamilika hapa duniani. Kitabu chochote cha kwanza kina changamoto nyingi. Hiki, kwa mfano, kina changamoto nyingi mno za kiuhariri na kiupangaji wa chapa. Ni maoni yangu kuwa kitabu hiki kinapaswa kuhaririwa na kuchapishwa upya.

Halafu katika mafanikio kuna kupanda na kushuka. Katika kitabu hiki tumeoneshwa kupanda zaidi kuliko kushuka. Tunahitaji kujifunza kutokana na mafanikio na tunahitaji kujifunza kutokana na makosa.

Hata hivyo, pamoja na mapungufu yote yaliyomo ndani ya kitabu hiki, ujumbe uliomo ndani ya If All you Have is One Song, Sing it Loud ni ujumbe wa thamani kubwa. Na binafsi, nitakitetea kitabu hiki kwa sababu kinastahili.

Nyamagesa Laban anajua maji yalipo na analeta kiu kwenye maji. Maarifa anayoyajua anataka nasi tuyajue.

Wednesday, 22 March 2017

UHAKIKI WA KITABU CHA PENZI LA DAMU CHA ANNA SAMWEL MANYANZA

Penzi la Damu ni kitabu kinachohusu maumivu ya mapenzi na upendo kati ya Mzee Kayeba Mirambo na familia yake na kati ya Joyce Rodriguez, Amina, Bi Hawa, Mwajabu na Haruna mfanyabiashara wa Mombo. Kinahusu maumivu ya mapenzi kati ya Huseni na Odette, Mama Msimbazi na mumewe, Jane na Benja na Malaika na Ben. Kinahusu maumivu ya mapenzi na upendo miongoni mwa jamii nzima ya wahusika wa Penzi la Damu.

Mwaka 1983 Malaika Mirambo alivunja ungo. Maisha yake yalikuwa na mchanganyiko wa asali na nyongo. Asali kwa sababu alifaulu kujiunga na kidato cha kwanza, ijapokuwa familia yake haikuwa na fedha za kumuendeleza kimasomo, na nyongo kwa sababu dada yake mkubwa Maida alimpa taarifa za usaliti wa baba yao kwa mama yao na kwa familia yao nzima.

Taarifa hizo ndani ya moyo wa Malaika zilizusha vita kati ya penzi la damu na penzi halali, vita iliyoendeshwa kwa zaidi ya miaka thelathini hadi kifo cha mpenzi wake Ben. Ben aliuwawa, katika mazingira ya kutatanisha, huko Moshi mwaka 2015.

Riwaya hii iliyojaa matatizo kuliko raha, nadhani ndiyo maana ikaitwa Penzi la Damu, imesimuliwa katika nafsi mbili zinazochanganya. Nafsi ya kwanza na nafsi ya tatu. Inaanza na nafsi ya kwanza kisha inaendelea na nafsi ya tatu halafu ya kwanza tena kisha ya tatu tena, hivyohivyo hadi mwisho wa riwaya.

Nafsi ya kwanza ina matatizo yake, hasa pale inaposimulia hadithi yenye wahusika wengi na visa vingi. Kisa cha Joyce kule Mombo isingewezekana kusimuliwa na Malaika aliyekuwa Tanga kipindi hicho na ambaye hakuwa na darubini ya kuona kila alichokifanya Joyce na Haruna na wakeze na mama yake Haruna Bi Hawa kwa usimulizi wa nafsi ya kwanza.

Hakuna sababu kutumia nafsi ya tatu kuanzia ukurasa wa 160-163 kama hadithi ilipangwa kusimuliwa na Malaika katika nafsi ya kwanza. Ukurasa wa 183 umechanganya nafsi zote mbili kwa pamoja na katika ukurasa wa 189: “Hakusema kitu” badala ya “Sikusema kitu” pamechanganywa nafsi zote mbili hali kadhalika.

Nafsi ya tatu ingetosha kusimulia hadithi hii vizuri na kwa ufasaha kabisa.

Lugha imepata changamoto pia katika riwaya hii ya Penzi la Damu. Mazungumzo ya Khurmanjee na mkewe katika ukurasa wa 38 yalipaswa kutafsiriwa kwa Kiswahili ili wasomaji wasiojua Kiingereza nao wafaidi, kama ilivyofanyika katika ukurasa wa 60.

Katika ukurasa wa 39 lafudhi ya Kihindi ya Mzee Khurmanjee imepotea ghafla. Ghafla anaongea Kiswahili fasaha! Hii inaonyesha kuwa Mzee Khurmanjee alikuwa akiigiza tu kuongea lafudhi ya Kihindi na alikuwa akikijua vizuri sana Kiswahili fasaha.

Pia, katika ukurasa wa 148, Wahindi Bwana Juzar na mkewe Bi Tassim wa Arusha ghafla wanaongea Kiswahili fasaha. Lakini ghafla tena katika ukurasa wa 149, wanaongea tena Kiswahili chenye lafudhi ya Kihindi.

Mojawapo ya kanuni za fasihi ni kutokumdanganya msomaji. Atajua tu.

Aidha, hapa duniani hakuna nchi inaitwa ‘Burma’ kwa Kiswahili. Kuna nchi inaitwa Bama. Wala hakuna nchi inaitwa ‘Poland’. Kuna nchi inaitwa Polandi. Ukurasa wa 1 na 29.

Wahusika kama Mzee Omari Makongoro, Mzee Kayeba Mirambo, Macha mdogo wake Lema, Nasoro Abdulseif rafikiye Antonio Rodriguez, Jambazi Godi, Jombi na wengineo wanasukuma hadithi mbele kama inavyotakiwa. Lakini wahusika kama Magugu Kayeba Mirambo na Mreno Carlos Fereira visa vyao haviisukumi hadithi mbele, kiasi kwamba hata kama wataondolewa hawataathiri mlolongo wa hadithi kwa vyovyote vile. Kila mhusika katika hadithi lazima awe na umuhimu wake mdogo au mkubwa, katika mlolongo wa hadithi yenyewe.

Katika ukurasa wa 73 Daktari Mwapachu anatoa kauli ambayo binafsi nadhani madaktari wote ulimwenguni hawapaswi kuitoa. Baada ya Odette na Estela kufariki katika chumba cha upasuaji, Mwapachu anatoa taarifa kwa ndugu wa marehemu inayofanya Edna (mama yake Odette) na Huseni (mume wa Odette na baba wa Estela) wachanganyikiwe kabisa.

Anasema, “Nesi mkuu atakuja kuwaona na kuwaeleza juu ya taratibu za kuchukua miili yao.” Kwa Edna na Huseni wale hawakuwa ‘miili’. Walikuwa watoto!

Labda angesema, “Nesi mkuu atakuja kuwaona na kuwaeleza juu ya taratibu zote zilizobakia.” Lakini haya ni mawazo yangu tu. Daktari angeweza kuzungumza lolote.

Pamoja na changamoto hizo ambazo binafsi naziona za kawaida lakini zirekebishwe sanasana kwa ajili ya usumbufu wa vizazi vijavyo, hadithi hii imeandikwa kwa upeo wa hali ya juu. Utafiti umechanganywa vyema na hadithi kiasi cha kuifanya hadithi ipendeze kusoma, na ionekane halisi zaidi kuliko hadithi ya kubuni.

Utafiti wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia umenikumbusha mbali kidogo. Umenikumbusha nilipokuwa nafanya utafiti wa shujaa wa kitabu cha Kolonia Santita, John Murphy Ambilikile. Babu yake Murphy, Ambilikile Makojo, aliishi maisha aliyoishi Mzee Kayeba Mirambo alipokuwa vitani ughaibuni.

Historia ya kitibegi cha Mzee Kayeba Mirambo inatupa historia kwa ufupi ya ushiriki wa Tanzania (Tanganyika) katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia huko Bama na kwingineko, na imechanganywa vizuri katika hadithi kiasi cha kumfanya Mzee Kayeba anase kisawasawa katika akili ya msomaji.

Tunafundishwa kuwa wavumilivu katika mapenzi. Tunafundishwa maisha halisi ya watu wa daraja la chini na la juu katika jamii. Tunafundishwa uaminifu. Tunafundishwa heshima. Tunafundishwa kusaidiana katika shida na raha. Tunafundishwa upendo.

Julius Idrissa Shemashi alikuwa mgumba na basha aliyemwoa Bernadina, dada mkubwa wa Joyce na Odette, mtoto wa Antonio Rodriguez, aliyekuwa akiishi Horohoro pamoja na pacha wa mume wake aliyeitwa Justus Idrissa Shemashi. Kwa siri kubwa Justus alizaa na mke wa kaka yake, hivyo kumfichia kaka yake siri ya ugumba iliyomsumbua sana. Hivyo, kitabu hiki kimegusa watu wa kila aina.

Kitabu hiki kimegusa pia harakati za ukombozi wa Mwafrika dhidi ya ukoloni mamboleo. Kimegusia pia suluhisho la tatizo hilo kwamba ni kujikomboa sisi wenyewe kisaikolojia, kifalsafa, kielimu na kifikra.

Penzi la Damu inaanza na upendo wa damu na inaisha na penzi la damu. Anna Samwel Manyanza ni malaika.

Friday, 10 March 2017

UHAKIKI WA KITABU CHA HUMAN POACHERS CHA ELIAS MUTANI

Master Lwanga na Joan ni mashujaa waliookoa maisha ya Jasiri, kijana mdogo mwenye ulemavu wa ngozi, katika kijiji cha kufikirika cha Saanane kilichoko mkoani Shinyanga. Lakini Lwanga na Joan hawakuwa peke yao. Walisaidiwa na watu wengi wakiwemo wanafunzi, walimu, wanakijiji, dereva wa teksi, na jeshi la polisi la Mkoa wa Shinyanga.

Kutokana na juhudi za watu wote hawa maisha ya Jasiri yalibadilika kichanya, huku ya msaliti mkuu wa watu wa Saanane mwenyekiti wa kijiji yakibadilika kihasi.

Human Poachers inatufundisha mambo mengi. Inatupa maarifa kuhusu ulemavu wa ngozi na dhana potofu zinazojitokeza kutokana na ulemevu huo. Vilevile inatufundisha kuwa kumbe mbinu za kiskauti zinaweza kusaidia kutatua matatizo sugu yanayolikumba taifa letu kwa kuzifundisha hasa vijijini ambako tatizo la ulemavu wa ngozi limekithiri. Inatufundisha pia ushirikiano, na inatufundisha jinsi ya kuandika vizuri.

Hata hivyo, kama ilivyo hadithi nyingine yoyote, Human Poachers ina mapungufu yake. Hatujui kwa mfano lugha waliyokuwa wakitumia watu wa Saanane. Hatujui kama walikuwa wakitumia Kiswahili, Kisukuma, Kiingereza, lugha yao wenyewe kwa vile Saanane ni kijiji cha kufikirika, au zote kwa pamoja.

Hatujui muda hasa wa mandhari ya hadithi licha ya kujua ilitokea katika kizazi hiki, ambapo tunaona hata baadhi ya wahusika wakiwa na simu za mikononi.

Aidha, kwangu mimi sikuupenda sana mwisho wa hadithi. Ningependa hadithi iishe kwa furaha au huzuni lakini wale wote wabaya wafikishwe katika vyombo vya dola kujibu mashtaka yaliyowakabili.

Wale wauaji wawili ambao Joan na Jasiri kwa nyakati tofauti waliwaona msituni wakijadiliana jinsi ya kumteka nyara Jasiri na kutengeneza pesa kutokana na viungo vya mwili wake, ijapokuwa yule mrefu hatujui kama alikufa au alizimia baada ya kupigwa na Joan na hata yule mfupi ambaye naye hatujui kama alikufa au alizimia baada ya kupigwa na Sunga, kadhalika ningependa kuona wakiadabishwa mahakamani.

Watu kama wale waheshimiwa wanasiasa wa Shinyanga waliokuwa wakivitaka viungo vya mwili wa Jasiri ili wapate pesa na madaraka, na hata mwenyekiti wa kijiji ambaye katika sura ya kumi alipotea nyumbani kwake alfajiri na hatukumwona tena hadi aliposhushwa na gari la mheshimiwa mmoja katika pango la Kilimanjaro, nao ningependa kuona wakiadabishwa.

Mwenyekiti wa kijiji asingeruhusiwa kufa. Angebakishwa hai ili ajibu mashtaka yote yaliyomkabili, na ataje wale wote waliohusika na mtandao wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, ili liwe fundisho kwa wananchi wote.

Pikipiki aliyochukua Joan na Omari kuwafukuzia majambazi ilitokea ghafla mno. Palitakiwa pawepo na kitu kinachoitwa foreshadowing, kitu ambacho kingetuonyesha kabla kwamba Joan na Omari wangekutana na msaada wa pikipiki ambayo ingewasaidia kumwokoa Jasiri.

Lugha katika ukurasa wa sabini na saba imekosewa kidogo. Badala ya “Do not return it to me” imeandikwa “Do not to return it to me”. Mhusika anaruhusiwa kukosea. Kwani katika mazungumzo ya kawaida watu hukosea. Lakini sidhani kama Joan alizungumza hivyo kwa makusudi alipokuwa akimkabidhi Salu kipenga.

Makosa haya hata kwenye kitabu changu Kolonia Santita yapo. Lakini si busara kwa makampuni ya uchapishaji kufanya makosa ya wazi kama hayo.

Licha ya makosa hayo madogomadogo hadithi ya Human Poachers ni hadithi nzuri sana, na Mwandishi Elias Mutani ni mwandishi bora. Ni rahisi kujua kwa nini kitabu hiki kilishinda Tuzo ya Burt mwaka 2016. Kwa sababu kimeandikwa kwa utaalamu na weledi wa hali ya juu na mwandishi ameunganisha vyema ubunifu, taharuki na uhalisia. Lakini swali langu ni moja: Master Lwanga ndiye Elias Mutani?

Serikali yetu isikie. Labda mbinu za kiskauti zilizotumika katika kitabu hiki zitasaidia kutokomeza tatizo la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi Tanzania.

Wednesday, 8 March 2017

Siku ya Wanawake Duniani

Chanzo cha Siku ya Wanawake Duniani ni harakati za wanawake katika miaka ya 1900 kujitafutia sauti yao katika jamii. Mwaka 1908 wanawake 15,000 waliandamana huko New York wakitaka haki yao ya kupiga kura, haki yao ya kufanya kazi na haki yao ya mishahara minono kama wanaume. Mwaka 1975 Siku ya Wanawake Duniani ikaadhimishwa rasmi kwa mara ya kwanza duniani kote chini ya Umoja wa Mataifa.

Walioanzisha Siku ya Wanawake Duniani ni wanawanke wa New York wa ILGWU, waliokuwa na lengo la haki sawa kwa wote.

Katika siku hii wanakumbukwa wanawake wa chama cha wanawake cha wafanyakazi cha International Ladies Garment Worker’s Union ambao, inasemekana, tarehe 8/3/1908 walisitisha maandamano.

Wanaosherehekea leo wanaijua thamani ya mwanamke ndiyo maana wanasherehekea.

NINAWATAKIA WANAWAKE WOTE DUNIANI HERI YA SIKU YA WANAWAKE!

Monday, 6 March 2017

Mh. Jacob Kassema


Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Mh. Jacob Kassema naye amejipatia nakala yake ya Kolonia Santita leo katika duka la vitabu la Soma Book Café, pamoja na Lilian Soma wa Soma. Mheshimiwa huyu ni mdau mkubwa wa Kolonia Santita toka miaka ya tisini, hata kabla hakijachapishwa.

Saturday, 4 March 2017

Clever Zulu

Jana mhamasishaji maarufu na mwandishi wa vitabu kutoka St Lucia, Visiwa vya Karibiani, Clever Zulu, alijipatia nakala yake ya Kolonia Santita katika duka la vitabu la Ujuzi Books Ltd; nami nikijipatia nakala ya kitabu chake kipya Absolute Abundance.

Thursday, 9 February 2017

IJUE TUME YA DUNIA YA KUDHIBITI MADAWA YA KULEVYA (WODEC) ILIYOKO CHINI YA MAMLAKA YA KUDHIBITI MADAWA YA KULEVYA NA UGAIDI WA KIMATAIFA DUNIANI (WODEA)

WODEA (‘World Drugs Enforcement Administration’) ni shirika la kujitegemea la kimataifa – linalofanya kazi kwa niaba ya Umoja wa Mataifa – lenye nia/shabaha ya kukomesha (katika dunia) madawa haramu ya kulevya, ya madaraja yote, pamoja na ugaidi wa kimataifa wa aina zote – hasa wa kimadawa, kisiasa na kinyukilia; kwa ajili ya amani, afya na usalama wa kimataifa.

WODEA ilianzishwa chini ya Mkataba wa Kisheria wa Kimataifa wa WODEA (‘WODEA Statute’) uliosimamiwa kwa kipindi cha siku tatu mfululizo na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, UNSC, Novemba 1975. Tofauti na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Nyukilia, IAEA, ambalo huwajibika kwa UNSC na kwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa; WODEA huwajibika kwa UNSC na kwa Baraza la Uchumi na Ustawi wa Jamii la Umoja wa Mataifa ECOSOC.

WODEC, Chombo Kikuu cha WODEA, ambayo hutumika kama kongamano la majadiliano ya masuala ya madawa na ugaidi ya kimataifa; huundwa na vyombo vingine vidogo vitatu: Bodi ya Makamishna ya Tume ya Dunia (WBC – ‘WODEC Board of Commissioners’), Mkutano Mkuu wa Tume ya Dunia (WGC – ‘WODEC General Conference’) na Sekretarieti ya Tume ya Dunia. WBC ni Chombo cha Sera cha Tume ya Dunia. Kina wajumbe 12 wanaoteuliwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na 26 wanaochaguliwa na Mkutano Mkuu wa Tume ya Dunia. Wajumbe 12 (watano wa kudumu wa UNSC na saba viongozi wa kanda za WODEA) huteuliwa na UNSC kwa kipindi cha miaka mitano, wakati 26 huchaguliwa na WGC kwa kipindi kimoja cha miaka miwili. WBC hutoa mapendekezo kwa WGC kuhusu bajeti na shughuli zote za WODEA.

Rais wa WODEA huchaguliwa na WGC kwa mapendekezo ya UNSC. WBC hupendekeza majina sita kwa UNSC ambayo huchagua majina matatu kati ya hayo sita na kuyapeleka katika Mkutano Mkuu wa WODEA – kupigiwa kura ya Kamishna Mkuu wa WODEC na Rais wa WODEA kwa kipindi cha miaka mitano. Kamishna Mkuu wa WODEC ni Rais wa WODEA. Wakati WBC hukutana mara nne kwa mwaka mjini Copenhagen kuanzia Novemba, WGC (nchi wanachama 143) hukutana mara moja kwa mwaka katika mwezi wa Novemba kuidhinisha bajeti na mapendekezo ya WBC – kwa ajili ya Sekretarieti ya Tume ya Dunia.

Sekretarieti ya Tume ya Dunia huwajibika na utekelezaji wa mapendekezo yote yaliyopitishwa na WBC na WGC kwa niaba ya WODEA. Huchaguliwa na WBC na kuidhinishwa na WGC kwa kipindi cha marudio cha miaka mitano. Sekretarieti ya Tume ya Dunia huwajibika pia na nguvukazi ya watu zaidi ya 7,000 duniani kote na bajeti ya wastani wa dola za Kimarekani milioni 400 kwa mwaka mzima.

Mbali na WBC, WGC na Sekretarieti ya Tume ya Dunia, WODEC ina vyombo vikubwa vitatu vya dola: Idara ya Polisi ya Tume ya Dunia (WPD), Idara ya Usalama ya Tume ya Dunia (WIS) na Kikosi Maalumu cha Kikomandoo cha Tume ya Dunia (EAC). EAC iliundwa kwa makubaliano maalumu ya Azimio la Copenhagen kati ya WODEA na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa – Novemba 1980.

WODEC ina maabara tatu za kikemia, ofisi tatu za mahusiano mema (Vienna, Pretoria na New York), kliniki saba za madawa ya kulevya na kanda sita katika mabara sita ya dunia nzima. Kila kanda ina bodi ya wakurugenzi, idara ya polisi, usalama, sekretarieti, maabara na kliniki za madawa ya kulevya. Kanda ya Afrika ya Kusini ya Tume ya Dunia huanzia Somalia mpaka Kameruni mpaka Afrika Kusini. Kanda ya Afrika ya Kaskazini ya Tume ya Dunia huanzia Eritirea mpaka Nijeria mpaka Tunisia, isipokuwa Moroko ambayo iko katika kanda ya Ulaya.

“Kama viongozi wenu wa kanda walivyowahabarisha tuna kazi kubwa mbele yetu inayohitaji moyo mkubwa wa kujitolea na ujasiri wa hali ya juu kujaribu tu hata kuifanya. Kazi ya Tume ya Dunia ni kupambana na aina yoyote ya uhalifu wa madawa ya kulevya kwa makusudi kutetea afya na amani ya dunia yote kwa watu wote ulimwenguni. Hii ni vita tuliyokula kiapo sisi wote kuipigana – vita ya sheria na udhalimu, wa madawa ya kulevya, na ugaidi wa kimataifa, tutakayopigana mpaka sheria ishinde na kufuata mkondo wake.” – Boidin Tony Versnick (Rais, Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya, 1985 – 1992)

Watu wananiuliza: “Je, Paul Makonda atashinda vita ya madawa ya kulevya katika mkoa wake bila kufuata mfumo wa Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya?” Jibu lake ni ndiyo na hapana. Hapana kwa sababu Mungu mwenyewe ndiye anayejua. Ndiyo kwa sababu Makonda ana ulinzi.

Paul Makonda ataweza kushinda vita ya madawa ya kulevya kwa sababu rais na waziri mkuu hawajihusishi na madawa ya kulevya. Nao watamlinda kwa gharama yoyote.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam anaposema vita hii iwe ya wazi na ya kila mtu wakati yeye ana ulinzi wengine watalindwa na nani? Vita dhidi ya madawa ya kulevya inapaswa kupiganwa kiintelijensia zaidi kuliko kipolisi, kisiasa, au sifa binafsi.

Friday, 9 December 2016

Siku ya Uhuru wa Tanzania

Tanganyika na Zanzibari ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tanzania ikisambaratika Watanganyika watabaki na Tanganyika yao, na Wazanzibari watabaki na Zanzibari yao. Tarehe 26/4/1964 hatukupata uhuru. Tulishaupata tayari. Tuliungana Zanzibari na Tanganyika na kutengeneza Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibari, na miezi sita baadaye (tarehe 29/10/1964) nchi ikaitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Makubaliano yakafanyika kuifanya tarehe 9/12/1961 kuwa tarehe, mwezi na mwaka rasmi wa uhuru wa taifa, na nchi zote zikataharifiwa, na kuanzia hapo kila tarehe 9/12 ya kila mwaka yakawa maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanzania kuanzia tarehe 9/12/1965. Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akawa rasmi rais wa kwanza wa jamhuri hiyo, na Hayati Abeid Amani Karume akawa rasmi makamu wa kwanza wa rais wa jamhuri hiyo. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Shehe Abeid Amani Karume walikuwa bendera ya taifa letu. Walikuwa alama ya amani, haki, uhuru, ujamaa, uzalendo, na Tanzania.

Tuesday, 11 October 2016

Kisiwa cha Saltholm


Saltholm ni kisiwa cha 21 kwa ukubwa kuliko vyote 406 vya Denmaki. Kipo katika Ukanda wa Bahari wa Øresund, unaoiunganisha Bahari ya Baltiki katika Bahari ya Atlantiki kupitia Kattegat, Skagerrak na Bahari ya Kaskazini; Daniel Yehuda, mpelelezi wa Tume ya Dunia kutoka Israeli, alipopelekwa na magaidi wa Kolonia Santita baada ya kutekwa katika Uwanja wa Ndege wa Copenhagen.

Daniel Yehuda, mpelelezi mashuhuri wa Tume ya Dunia kutoka Kidon (kitengo cha mauti na utekaji nyara cha shirika la kijasusi la Mossad la Israeli) alipotekwa na magaidi wa Kolonia Santita alipelekwa Saltholm kupitia Ghuba ya Køge na Dragør katika Manispaa ya TÃ¥rnby. Pembeni mwa kisiwa, kiasi cha meta kama mia nne hivi kutoka ufukoni – maadui walipoegesha boti yao – kulikuwa na nyumba ya kawaida ya vyumba viwili vikubwa vya kulala, choo, bafu, sebule na sehemu kubwa ya kuhifadhia vitu; iliyokuwa na ukuta wa rangi ya njano, kama nyumba nyingi za Dragør. Ilikuwa na vigae vikuukuu vya kijani. Haikuwa na ukuta wa ua. Ilikuwa na seng’enge na miti mingi (nje na ndani ya seng’enge hiyo) na geti kubwa la chuma kwa upande wa kusini, ambako ndiko maadui walikuwa wakitokea na Yehuda. Nje kulikuwa na zizi kubwa la ng’ombe, na hifadhi ya ndege (kama kinega, kubo, mpasuasanda na kinegwa – jamii ya mbayuwayu), na nyumba nyingine kwa mbali (kama kilometa moja au zaidi kidogo) ya mwangalizi wa kisiwa, na miamba michache (hasa karibu na ufuko) na miti mirefu ya njano (inayoteleza) ya hapa na pale ya miparamuzi. Matatizo aliyoyapata Yehuda yalikuwa makubwa. Lakini bila matatizo hayo Radia Hosni angeuwawa usiku wa siku hiyo bila kukosa, na John Murphy angeuwawa na magaidi wasiojulikana. Vijana wa Tume wasingejua kama Kolonia Santita ndiyo waliyohusika na ulipuaji wa ndege ya shirika la ndege la Ufaransa, kama Daniel Yehuda asingetekwa na magaidi wa Kolonia Santita. Kutekwa kwa Yehuda kulikuwa na faida.

Sunday, 9 October 2016

Hiroglifu ya Kolonia Santita

Hiroglifu ya Kolonia Santita ni alama inayotumiwa na vituo vya udhibiti wa magonjwa (CDC) na taasisi za afya za kitaifa (NIH) duniani kote. Hutumiwa na Kolonia Santita kwa sababu Panthera Tigrisi au El Tigre (jambazi mkuu wa Kolonia Santita na mfalme wa madawa ya kulevya duniani) anamiliki makampuni ya kikemia na ujenzi katika mabara yote ya Amerika na katika bara la Asia. Rangi nyeusi inawakilisha nguvu za giza, rangi nyekundu inawakilisha hatari, vichwa vitatu vya sururu vinawakilisha biashara, na chembe tatu za bunduki zinawakilisha halafa. Katika hiroglifu (hieroglifu) vichwa vitatu vya sururu na chembe tatu za bunduki za Kalashnikov; na alama ya bahati, mafanikio, udhalimu na mwanzo mpya ya msalaba wa swastika, hutumika kama alama ya ujenzi na halafa ya Kolonia Santita. Alama hii inatumika hata katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, na inatambuliwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wednesday, 14 September 2016

Money

“God made man; man made money and money made man mad, that’s why everybody is mad about money.” –Unknown

http://www.enockmaregesi.wordpress.com

Sunday, 11 September 2016

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...