Master
Lwanga na Joan ni mashujaa waliookoa maisha ya Jasiri, kijana mdogo
mwenye ulemavu wa ngozi, katika kijiji cha kufikirika cha Saanane
kilichoko mkoani Shinyanga. Lakini Lwanga na Joan hawakuwa peke yao.
Walisaidiwa na watu wengi wakiwemo wanafunzi, walimu, wanakijiji, dereva
wa teksi, na jeshi la polisi la Mkoa wa Shinyanga.
Kutokana
na juhudi za watu wote hawa maisha ya Jasiri yalibadilika kichanya,
huku ya msaliti mkuu wa watu wa Saanane mwenyekiti wa kijiji
yakibadilika kihasi.
Human Poachers
inatufundisha mambo mengi. Inatupa maarifa kuhusu ulemavu wa ngozi na
dhana potofu zinazojitokeza kutokana na ulemevu huo. Vilevile
inatufundisha kuwa kumbe mbinu za kiskauti zinaweza kusaidia kutatua
matatizo sugu yanayolikumba taifa letu kwa kuzifundisha hasa vijijini
ambako tatizo la ulemavu wa ngozi limekithiri. Inatufundisha pia
ushirikiano, na inatufundisha jinsi ya kuandika vizuri.
Hata hivyo, kama ilivyo hadithi nyingine yoyote, Human Poachers
ina mapungufu yake. Hatujui kwa mfano lugha waliyokuwa wakitumia watu
wa Saanane. Hatujui kama walikuwa wakitumia Kiswahili, Kisukuma,
Kiingereza, lugha yao wenyewe kwa vile Saanane ni kijiji cha kufikirika,
au zote kwa pamoja.
Hatujui
muda hasa wa mandhari ya hadithi licha ya kujua ilitokea katika kizazi
hiki, ambapo tunaona hata baadhi ya wahusika wakiwa na simu za mikononi.
Aidha,
kwangu mimi sikuupenda sana mwisho wa hadithi. Ningependa hadithi iishe
kwa furaha au huzuni lakini wale wote wabaya wafikishwe katika vyombo
vya dola kujibu mashtaka yaliyowakabili.
Wale
wauaji wawili ambao Joan na Jasiri kwa nyakati tofauti waliwaona
msituni wakijadiliana jinsi ya kumteka nyara Jasiri na kutengeneza pesa
kutokana na viungo vya mwili wake, ijapokuwa yule mrefu hatujui kama
alikufa au alizimia baada ya kupigwa na Joan na hata yule mfupi ambaye
naye hatujui kama alikufa au alizimia baada ya kupigwa na Sunga,
kadhalika ningependa kuona wakiadabishwa mahakamani.
Watu
kama wale waheshimiwa wanasiasa wa Shinyanga waliokuwa wakivitaka
viungo vya mwili wa Jasiri ili wapate pesa na madaraka, na hata
mwenyekiti wa kijiji ambaye katika sura ya kumi alipotea nyumbani kwake
alfajiri na hatukumwona tena hadi aliposhushwa na gari la mheshimiwa
mmoja katika pango la Kilimanjaro, nao ningependa kuona wakiadabishwa.
Mwenyekiti
wa kijiji asingeruhusiwa kufa. Angebakishwa hai ili ajibu mashtaka yote
yaliyomkabili, na ataje wale wote waliohusika na mtandao wa mauaji ya
watu wenye ulemavu wa ngozi, ili liwe fundisho kwa wananchi wote.
Pikipiki aliyochukua Joan na Omari kuwafukuzia majambazi ilitokea ghafla mno. Palitakiwa pawepo na kitu kinachoitwa foreshadowing, kitu ambacho kingetuonyesha kabla kwamba Joan na Omari wangekutana na msaada wa pikipiki ambayo ingewasaidia kumwokoa Jasiri.
Lugha
katika ukurasa wa sabini na saba imekosewa kidogo. Badala ya “Do not
return it to me” imeandikwa “Do not to return it to me”. Mhusika
anaruhusiwa kukosea. Kwani katika mazungumzo ya kawaida watu hukosea.
Lakini sidhani kama Joan alizungumza hivyo kwa makusudi alipokuwa
akimkabidhi Salu kipenga.
Makosa haya hata kwenye kitabu changu Kolonia Santita yapo. Lakini si busara kwa makampuni ya uchapishaji kufanya makosa ya wazi kama hayo.
Licha ya makosa hayo madogomadogo hadithi ya Human Poachers ni hadithi nzuri sana, na Mwandishi Elias Mutani
ni mwandishi bora. Ni rahisi kujua kwa nini kitabu hiki kilishinda Tuzo
ya Burt mwaka 2016. Kwa sababu kimeandikwa kwa utaalamu na weledi wa
hali ya juu na mwandishi ameunganisha vyema ubunifu, taharuki na
uhalisia. Lakini swali langu ni moja: Master Lwanga ndiye Elias Mutani?
Serikali
yetu isikie. Labda mbinu za kiskauti zilizotumika katika kitabu hiki
zitasaidia kutokomeza tatizo la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi
Tanzania.
No comments:
Post a Comment