Wednesday, 22 March 2017

UHAKIKI WA KITABU CHA PENZI LA DAMU CHA ANNA SAMWEL MANYANZA

Penzi la Damu ni kitabu kinachohusu maumivu ya mapenzi na upendo kati ya Mzee Kayeba Mirambo na familia yake na kati ya Joyce Rodriguez, Amina, Bi Hawa, Mwajabu na Haruna mfanyabiashara wa Mombo. Kinahusu maumivu ya mapenzi kati ya Huseni na Odette, Mama Msimbazi na mumewe, Jane na Benja na Malaika na Ben. Kinahusu maumivu ya mapenzi na upendo miongoni mwa jamii nzima ya wahusika wa Penzi la Damu.

Mwaka 1983 Malaika Mirambo alivunja ungo. Maisha yake yalikuwa na mchanganyiko wa asali na nyongo. Asali kwa sababu alifaulu kujiunga na kidato cha kwanza, ijapokuwa familia yake haikuwa na fedha za kumuendeleza kimasomo, na nyongo kwa sababu dada yake mkubwa Maida alimpa taarifa za usaliti wa baba yao kwa mama yao na kwa familia yao nzima.

Taarifa hizo ndani ya moyo wa Malaika zilizusha vita kati ya penzi la damu na penzi halali, vita iliyoendeshwa kwa zaidi ya miaka thelathini hadi kifo cha mpenzi wake Ben. Ben aliuwawa, katika mazingira ya kutatanisha, huko Moshi mwaka 2015.

Riwaya hii iliyojaa matatizo kuliko raha, nadhani ndiyo maana ikaitwa Penzi la Damu, imesimuliwa katika nafsi mbili zinazochanganya. Nafsi ya kwanza na nafsi ya tatu. Inaanza na nafsi ya kwanza kisha inaendelea na nafsi ya tatu halafu ya kwanza tena kisha ya tatu tena, hivyohivyo hadi mwisho wa riwaya.

Nafsi ya kwanza ina matatizo yake, hasa pale inaposimulia hadithi yenye wahusika wengi na visa vingi. Kisa cha Joyce kule Mombo isingewezekana kusimuliwa na Malaika aliyekuwa Tanga kipindi hicho na ambaye hakuwa na darubini ya kuona kila alichokifanya Joyce na Haruna na wakeze na mama yake Haruna Bi Hawa kwa usimulizi wa nafsi ya kwanza.

Hakuna sababu kutumia nafsi ya tatu kuanzia ukurasa wa 160-163 kama hadithi ilipangwa kusimuliwa na Malaika katika nafsi ya kwanza. Ukurasa wa 183 umechanganya nafsi zote mbili kwa pamoja na katika ukurasa wa 189: “Hakusema kitu” badala ya “Sikusema kitu” pamechanganywa nafsi zote mbili hali kadhalika.

Nafsi ya tatu ingetosha kusimulia hadithi hii vizuri na kwa ufasaha kabisa.

Lugha imepata changamoto pia katika riwaya hii ya Penzi la Damu. Mazungumzo ya Khurmanjee na mkewe katika ukurasa wa 38 yalipaswa kutafsiriwa kwa Kiswahili ili wasomaji wasiojua Kiingereza nao wafaidi, kama ilivyofanyika katika ukurasa wa 60.

Katika ukurasa wa 39 lafudhi ya Kihindi ya Mzee Khurmanjee imepotea ghafla. Ghafla anaongea Kiswahili fasaha! Hii inaonyesha kuwa Mzee Khurmanjee alikuwa akiigiza tu kuongea lafudhi ya Kihindi na alikuwa akikijua vizuri sana Kiswahili fasaha.

Pia, katika ukurasa wa 148, Wahindi Bwana Juzar na mkewe Bi Tassim wa Arusha ghafla wanaongea Kiswahili fasaha. Lakini ghafla tena katika ukurasa wa 149, wanaongea tena Kiswahili chenye lafudhi ya Kihindi.

Mojawapo ya kanuni za fasihi ni kutokumdanganya msomaji. Atajua tu.

Aidha, hapa duniani hakuna nchi inaitwa ‘Burma’ kwa Kiswahili. Kuna nchi inaitwa Bama. Wala hakuna nchi inaitwa ‘Poland’. Kuna nchi inaitwa Polandi. Ukurasa wa 1 na 29.

Wahusika kama Mzee Omari Makongoro, Mzee Kayeba Mirambo, Macha mdogo wake Lema, Nasoro Abdulseif rafikiye Antonio Rodriguez, Jambazi Godi, Jombi na wengineo wanasukuma hadithi mbele kama inavyotakiwa. Lakini wahusika kama Magugu Kayeba Mirambo na Mreno Carlos Fereira visa vyao haviisukumi hadithi mbele, kiasi kwamba hata kama wataondolewa hawataathiri mlolongo wa hadithi kwa vyovyote vile. Kila mhusika katika hadithi lazima awe na umuhimu wake mdogo au mkubwa, katika mlolongo wa hadithi yenyewe.

Katika ukurasa wa 73 Daktari Mwapachu anatoa kauli ambayo binafsi nadhani madaktari wote ulimwenguni hawapaswi kuitoa. Baada ya Odette na Estela kufariki katika chumba cha upasuaji, Mwapachu anatoa taarifa kwa ndugu wa marehemu inayofanya Edna (mama yake Odette) na Huseni (mume wa Odette na baba wa Estela) wachanganyikiwe kabisa.

Anasema, “Nesi mkuu atakuja kuwaona na kuwaeleza juu ya taratibu za kuchukua miili yao.” Kwa Edna na Huseni wale hawakuwa ‘miili’. Walikuwa watoto!

Labda angesema, “Nesi mkuu atakuja kuwaona na kuwaeleza juu ya taratibu zote zilizobakia.” Lakini haya ni mawazo yangu tu. Daktari angeweza kuzungumza lolote.

Pamoja na changamoto hizo ambazo binafsi naziona za kawaida lakini zirekebishwe sanasana kwa ajili ya usumbufu wa vizazi vijavyo, hadithi hii imeandikwa kwa upeo wa hali ya juu. Utafiti umechanganywa vyema na hadithi kiasi cha kuifanya hadithi ipendeze kusoma, na ionekane halisi zaidi kuliko hadithi ya kubuni.

Utafiti wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia umenikumbusha mbali kidogo. Umenikumbusha nilipokuwa nafanya utafiti wa shujaa wa kitabu cha Kolonia Santita, John Murphy Ambilikile. Babu yake Murphy, Ambilikile Makojo, aliishi maisha aliyoishi Mzee Kayeba Mirambo alipokuwa vitani ughaibuni.

Historia ya kitibegi cha Mzee Kayeba Mirambo inatupa historia kwa ufupi ya ushiriki wa Tanzania (Tanganyika) katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia huko Bama na kwingineko, na imechanganywa vizuri katika hadithi kiasi cha kumfanya Mzee Kayeba anase kisawasawa katika akili ya msomaji.

Tunafundishwa kuwa wavumilivu katika mapenzi. Tunafundishwa maisha halisi ya watu wa daraja la chini na la juu katika jamii. Tunafundishwa uaminifu. Tunafundishwa heshima. Tunafundishwa kusaidiana katika shida na raha. Tunafundishwa upendo.

Julius Idrissa Shemashi alikuwa mgumba na basha aliyemwoa Bernadina, dada mkubwa wa Joyce na Odette, mtoto wa Antonio Rodriguez, aliyekuwa akiishi Horohoro pamoja na pacha wa mume wake aliyeitwa Justus Idrissa Shemashi. Kwa siri kubwa Justus alizaa na mke wa kaka yake, hivyo kumfichia kaka yake siri ya ugumba iliyomsumbua sana. Hivyo, kitabu hiki kimegusa watu wa kila aina.

Kitabu hiki kimegusa pia harakati za ukombozi wa Mwafrika dhidi ya ukoloni mamboleo. Kimegusia pia suluhisho la tatizo hilo kwamba ni kujikomboa sisi wenyewe kisaikolojia, kifalsafa, kielimu na kifikra.

Penzi la Damu inaanza na upendo wa damu na inaisha na penzi la damu. Anna Samwel Manyanza ni malaika.

1 comment:

  1. Kama ni nyota nitaipa nyota nne (4) na kuipendekeza kwa wasomaji wote.

    ReplyDelete

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...