Friday 9 March 2018

Taabu ya Yakobo

Irani itakapoipiga Israeli, kama ambavyo imeshaahidi, Israeli itajibu mapigo. Kwa vile Israeli ina nguvu zaidi kuliko Irani, itaipiga Irani kwa silaha za kawaida. Itaipiga hata kwa silaha za kinyukilia pia.

Kutunisha misuli, Irani itaomba msaada wa kijeshi kutoka katika nchi za Kiarabu; ambazo zitakubali kuingilia kati na kuisaidia Irani. Kwa silaha za kawaida, bado nchi zote za Kiarabu zitakazokubali kuisaidia Irani hazitakuwa na uwezo wa kuishinda Israeli. Kuishinda itabidi zitumie silaha za kinyukilia.

Silaha za kinyukilia zitakapoanza kutumika, Marekani itaingilia kati kuisaidia Israeli. Marekani itakapoingilia kati kuisaidia Israeli, Urusi itaingilia kati kuisaidia Irani. Ufaransa, Uingereza na Ujerumani zitaingilia kati kuisaidia Israeli; huku China ikiingilia kati kuisaidia Irani. Hapo Vita Kuu ya Tatu ya Dunia itaanzishwa rasmi.

Katika vita hiyo ya kinyukilia na mbaya kuliko vita zote zilizowahi kupiganwa, Israeli itashinda vita na itaanzisha utawala wa Mpinga Kristo duniani kote. Kutakuwa na dini moja. Kutakuwa na serikali moja. Kutakuwa na sarafu moja. Watu watapungua hadi kufikia milioni 500, kama ilivyokuwa mwaka 1650, asilimia 7 ya idadi ya watu wote ya leo.

Wafuasi wa Yesu Kristo watapata taabu kubwa ambayo haijawahi kutokea. Yeyote atakayempinga Mpinga Kristo, yeyote atakayepinga utawala wa Mpinga Kristo, atakiona cha mtema kuni. Watu wengi watauwawa kwa sababu ya ufuasi wao kwa Masihi. Wale watakaokuwa na talanta ya kuhubiri watauwawa kinyama, hadharani, ili liwe fundisho kwa wafuasi wengine wa Yesu Kristo.

Miongoni mwa wale watakaokuwa wanahubiri injili ya kweli ya ufalme wa Mungu bila woga wa aina yoyote ile, atakuwemo Eliya na Enock. Eliya na Enock Mungu aliwachukua bila kuonja mauti, kama akiba, kwa sababu ya kipindi hicho cha Taabu ya Yakobo.

Eliya na Enock wataibuka ghafla jijini Yerusalemu na kuanza kuhubiri injili ya kumpinga Mpinga Kristo. Kwa vile hawataogopa chochote, wala hawatamwogopa yeyote, serikali ya Israeli itawakamata na kuwatesa lakini hawatanyamaza.

Mpinga Kristo atakapoona imeshindikana kuwanyamazisha, Eliya na Enock, huku akitamba kwamba yeye ndiye Yesu Kristo ambaye kila mtu ndiye aliyekuwa akimsubiri arudi kwa mara ya pili; na kwamba yeye anatoka katika ukoo wa mfalme Daudi, ili watu waamini kama kweli yeye ndiye Yesu Kristo, ataamuru Eliya na Enock wauwawe hadharani kama wahubiri wengine.

Eliya na Enock watakapouwawa, Mungu atawafufua na watarudi mbinguni wakiwa wameonja mauti kama binadamu mwingine yeyote yule. Hapo mlango wa rehema utakuwa umefungwa. Muda wowote kuanzia hapo Yesu atarudi, kwa mara ya pili, na kwa ajili ya ufufuo wa kwanza.

Watakatifu wote watanyanyuliwa na wataondoka pamoja na Yesu kuelekea mbinguni, kwa ajili ya ziara ya miaka 1000 katika ulimwengu wa roho; kuanzia dunia ya kwanza ya ulimwengu huo iitwayo Asiyah hadi ya mwisho iitwayo Adam Kadmon, katika mji mpya wa Yerusalemu.

Baada ya milenia, kipindi hicho huku duniani Ibilisi akiwa kifungoni na malaika wake, binadamu wote wenye dhambi wakiwa wamekufa, Yesu na watakatifu wote atarudi kwa ajili ya ufufuo wa pili; na kama mfalme wa ulimwengu wote milele.

Wenye dhambi watafufuliwa na wataungana na Ibilisi kuipiga Yerusalemu Mpya itakayokuwa inang'inia hewani, huku Yesu na watakatifu wote wakiwa hawana silaha yoyote; lakini vilevile wakiwa hawapigwi kwa silaha yoyote.

Shetani atakapoonekana kushindwa, Yesu atawasha ‘kibiriti cha kiroho’. Mafuta yote yaliyopo ardhini dunia nzima yatalipuka na kugeuza ardhi yote kuwa ziwa la moto, na hivyo wenye dhambi wote kupata aibu ya milele.

Katika Biblia kuna tabiri 333 kuhusu maisha ya Yesu Kristo, na kuhusu kurudi kwake kwa mara ya pili. Kati ya hizo, 332 zilitimia! Bado mmoja tu: Kurudi kwa Yesu Kristo kwa mara ya pili.

Unadhani huo wa kurudi kwa Yesu Kristo kwa mara ya pili hautatimia? Muda umefika. Jitathmini katika maisha yako na uchague lililo jema.

Enock Maregesi

No comments:

Post a Comment

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...