Friday, 15 June 2018

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu.

Kila mtu kabla ya kuzaliwa roho yake iliumbwa na Mwenyezi Mungu na kupangiwa nchi itakapozaliwa na kuishi. Katika nchi hiyo Mungu akatanguliza malaika mwema ambaye kazi yake ni kumsaidia mtu mwenye roho hiyo tangu kuzaliwa kwake hadi kufa kwake hadi baada ya hapo.

Lakini Shetani atakapoinasa roho hiyo, kabla mwenye nayo hajazaliwa, ataibadilisha ili izaliwe sehemu nyingine tofauti na pale alipopanga Mungu; ili imtumikie yeye badala ya kumtumikia Mungu.

Kujua uraia halisi wa roho yako, hivyo kuujua uraia wako, lazima ujitambue; lazima ujue kwa nini ulizaliwa.

Mungu akikuweka mahali unapostahili kuwa, kulingana na takdiri ya maisha yako, hakuna mtu mwenye uwezo wa kushindana na kipaji chako.

Ishi mahali unapostahili kuishi.

Kiburi

288. Kiburi ni kiwango cha juu kabisa cha umimi au ubinafsi, na ni sumu ya mahusiano.

Kuwa na kiasi. Usiwe mjinga sana wala usiwe mjanja sana. Ukiwa mjinga sana utapata matatizo, kwa Mungu na kwa wanadamu, na ukiwa mjanja sana utapata matatizo pia, ambayo ni kiburi, kwa sababu mtu mwenye kiburi hawezi kamwe kuridhika na heshima na unyenyekevu anaoupata kutoka kwa watu.

Watu wenye kiburi ni wabinafsi, watu wanaopenda kuheshimiwa na kunyenyekewa, na wanajiona bora zaidi kuliko wengine, wanaopata taabu sana kuomba msamaha. Kiburi si upendo na upendo si kiburi. Dawa ya kiburi si kiburi kingine. Dawa ya kiburi ni upendo na hekima.

Hata hivyo, kuna tofauti kati ya kutokujiamini na kiburi. Mtu anaweza asijiamini na asiwe na kiburi, na anaweza asijiamini na akawa na kiburi.

Wengine wanasema kiburi ni kizuri, kwamba ili umshinde Shetani lazima uwe na kiburi. Lakini kiburi dhidi ya Shetani unakishinda kwa hekima.

Kibiritingoma

287. Umewahi kutongoza mwanamke akajishauri kukukubali badala ya kujishauri kukukataa? Umewahi kutongoza mwanamume akajishauri kukukataa badala ya kujishauri kukukubali? Ndugu yangu, yashinde majaribu.

Sababu kubwa inayofanya mwanamke au mwanamume ajishauri kumkubali mwanamume au mwanamke badala ya kujishauri kumkataa ni nguvu ya uchumi aliyonayo mwanamume au mwanamke anayetongoza. Kumkataa mtu mwenye nguvu ya uchumi ni vigumu sana hata awe mbaya kiasi gani. Maana nguvu ya uchumi haiangalii sura wala umbile la mtu.

Mwanamke anayejishauri kumkubali mwanamume yeyote mzuri au mwenye pesa, au mbaya na mwenye pesa, au mzuri na mwenye pesa, ni kibiritingoma. Yule anayejishauri kukataa ni muungwana.

Mwanamume anayejishauri kumkataa mwanamke yeyote mzuri au mwenye pesa, au mbaya na mwenye pesa, au mzuri na mwenye pesa, ni muungwana. Yule anayejishauri kukubali ni kibiritingoma.

Kuna tamaa ya ngono na kuna tamaa ya pesa. Mwanamume ana tamaa ya ngono na mwanamke ana tamaa ya pesa, na kinyume chake.

Yashinde majaribu yako, kwani nguvu kubwa ya Shetani imejificha katika mafanikio.

Mwanamume kumtongoza mwanamke au mwanamke kumtongoza mwanamume akakubali au akakataa kirahisi, au vinginevyo, ni jaribu ambalo kila mtu anapaswa kulishinda kwa hekima ya Mungu.

Kiungo cha binadamu kinachofanya watu waongezeke hatukupewa ili tukitumie kwa anasa za ulimwengu huu. Tulipewa kwa ajili ya kuongezeka tukiwa katika taasisi rasmi ya ndoa, kama upendo wa Yesu Kristo na Kanisa, na kwa ajili ya starehe ya macho kama ilivyorekodiwa katika kitabu cha mapenzi cha Biblia kiitwacho Wimbo Ulio Bora.

Mungu alipomuumba Adamu na Hawa amri ya kwanza aliyowapa ni kufanya mapenzi, ili waijaze dunia, wakiwa katika taasisi ya ndoa. Hivyo, mapenzi nje ya taasisi ya ndoa ni dhambi inayostahili aibu.

Kitu Kigumu Kuliko Vyote

286. Kitu kigumu kuliko vyote usikikatie tamaa, hasa kile unachojua kikifanikiwa kitasaidia watu wengi, kwani kuna uwezekano kikawa kizuri na chenye manufaa zaidi kuliko vyote.

Unapokuwa unafukuzia ndoto, njia ya kuifikia ndoto hiyo aghalabu huwa ngumu sana; lakini pale inapotimia, ndoto hiyo huwa kitu kizuri kuliko vyote.

Kama kwako msamaha ni kitu kigumu kuliko vyote ni kizuri kuliko vyote ukiumudu, kwani kigumu kuliko vyote ni kizuri kuliko vyote.

Wachawi Huroga Watu Waliolaaniwa na Mungu

285. Wachawi huroga watu waliolaaniwa na Mungu. Ukijiondoa katika laana ya Mungu maana yake ni kwamba umebarikiwa na Mungu. Hakuna mchawi, yeyote, atakayekuroga ukarogeka.

Kujiondoa katika laana ya Mungu ni kuwa rafiki wa kweli wa msalaba wa Yesu Kristo; na Biblia. Kwani Biblia na msalaba havirogeki. Ukiwa msomaji mzuri wa Biblia utajiepusha na balaa zote za laana ya Mungu; zilizogongomolewa msalabani huko Kalvari, Yesu alipolipa gharama ya maisha yake kutununua kutoka kwa Shetani.

Maisha Mkebe wa Hesabu

284. Maisha ni kama mkebe wa hesabu. Ndani yake kuna talanta saba. Rula hutusaidia kuweka mambo kwenye mstari. Penseli hutusaidia kuwa na malengo katika maisha. Pembetatu hutukumbusha haki na usawa kwa wote. Kipimapembe hutusaidia kujiheshimu na hutusaidia kupata maarifa. Kifutio hutukumbusha kuanza upya pale tunapokuwa tumekosea. Kichongeo hutusaidia kunoa penseli ili tuendelee kuwa na uwezo wa kujiwekea malengo katika maisha. Bikari hutukumbusha kuwa na mipaka katika maisha yetu. Angalia Shetani ameiba talanta gani katika mkebe wa maisha yako, na uirudishe talanta hiyo kwa gharama yoyote ile.

Bikari ikipotea utagombana na watu kila siku, hutakuwa na hekima ya kutenda jambo, kwani hutakuwa na mipaka katika kila jambo utakalolifanya. Kichongeo kikipotea hutafanikiwa katika maisha, kwa sababu hutakuwa na penseli ya kukuwezesha kuweka malengo katika maisha yako. Kifutio kikipotea, ukifanya kosa hutakuwa na uwezo wa kulisahihisha. Kipimapembe kikipotea hutapata maarifa na hutaheshimika.

Pembetatu ikipotea utaandamwa sana na watu wa haki za binadamu na watu wengine wote wanaopenda haki na usawa popote utakapokuwa. Penseli ikipotea hutakuwa na uwezo wa kujiwekea malengo katika maisha yako. Rula ikipotea ujue mambo yako hayatanyooka kamwe. Mkebe mzima ukipotea, hutakuwa na uwezo tena wa kuuona ufalme wa Mungu.

Hivyo, ni jukumu lako kuona ni talanta gani imechukuliwa na Shetani katika mkebe wa maisha yako na uirudishe kabla mlango wa rehema haujafungwa. Kwani mlango wa rehema ukifungwa, huku bado talanta zako hazijarudishwa, roho yako itaandikwa katika daftari la kuzimu na pengine usiokolewe kamwe.

Kufanikiwa Lazima Ushindikane

283. Kufanikiwa lazima ushindikane.

Kufanikiwa lazima umshinde Shetani. Wale waliofanikiwa kupitia nguvu za giza wamemshinda Shetani, kwa sababu Mungu ameruhusu wafanikiwe. Bila Mungu kuruhusu, hakuna atakayefanikiwa.

Wapo watu nomi waliobobea katika mambo ya giza lakini hawajafanikiwa; wamekwenda kwa wachawi na waganga wa jadi dunia nzima; na wapo watu wengi waliobobea katika mambo ya nuru lakini hawajafanikiwa; wamekwenda kwa wachungaji, mapadri na mashehe dunia nzima. Kwa nini? Kwa sababu Mungu hajaruhusu wafanikiwe. Lazima kuna sehemu wanakosea ndiyo maana Mungu hajawafungulia milango ya baraka.

Mungu anaweza kutumia mafanikio ya Shetani kwa faida ya watu wake. Mathalani, jambazi anaweza kujenga kanisa kwa ajili ya watu wa Mungu na Mungu akalibariki na akambariki jambazi, kwa sababu sifa kuu ya Mungu ni upendo. Jambazi anaweza kwenda kuiba akafanikiwa, wakati mchungaji anaweza kwenda kuhubiri akapata matatizo.

Mamafia wa Amerika ya Kusini na Kaskazini wanafanikiwa katika mambo yao, kwa sababu wanasaidia watu waliosahauliwa na serikali zao. Wanatoa upendo kwa Mungu, kwa kutoa upendo kwa wengine, ijapokuwa walifanikiwa kupitia nguvu za giza.

Katika giza lazima ushindikane, na katika nuru lazima ushindikane pia. Katika giza lazima ushindikane dhidi ya hila za Shetani, kwa kuwa mshirikina kwelikweli; na katika nuru lazima ushindikane dhidi ya hila za Shetani, kwa kuwa mlokole kwelikweli.

Kufanikiwa lazima ushindikane ama katika nuru au katika giza. Ukishindikana katika nuru umemshinda Shetani, ukishindikana katika giza umemshinda Shetani, lakini kwa ruhusa ya Mwenyezi Mungu.

Kubarikiwa, hata hivyo, si ishara ya kusamehewa dhambi. Kubarikiwa ni ishara ya kuwasaidia wengine.

Imani ya Wakristo Wengi Haina Macho

282. Imani ya Wakristo wengi haina macho. Wanaamini watu. Wanaamini kile watu wanachokisema, na kukiandika, badala ya kumwamini Mungu. Kumwamini mtu, au kuamini maandishi, badala ya kumwamini Mungu, ni sawa na kuabudu miungu wengine.

Weka akili yako pembeni kwa muda. Usiamini kile mtu anachokwambia, au usiamini kile unachokisoma kwenye vitabu. Lakini yachukue mawazo yao kisha yajaribishe katika mafundisho yako ya kiroho, ambayo tayari unayo, ili ujue kama kweli kile kilichosemwa au kuandikwa kinaleta maana katika maisha yako. Kama kinaleta, uko huru kumwamini Mungu. Lakini kama hakileti, ukimwamini Mungu umemwamini mungu mwingine.

Yesu na waandishi wote wa Biblia waliongea na kuandika kimafumbo, ili Neno la Mungu lijidhihirishe lenyewe kiroho katika mawazo ya mtu. Unaposikia Neno la Mungu kutoka kwa mtu acha lijidhihirishe lenyewe katika mawazo yako, kabla ya kumwamini au kutokumwamini Mungu.

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...