Sunday, 28 May 2017

Mpaka wa Kimataifa wa San Ysidro

Mpaka wa Kimataifa wa San Ysidro, Tijuana-San Diego, ambao ni mkubwa kuliko mipaka yote duniani, hadithi ya Kolonia Santita ilipoanzia.

Kolonia Santita si tu shabaha ya Tume ya Dunia kwa sababu ya madawa ya kulevya na maanguko ya kijamii. Ni shabaha ya Tume ya Dunia kwa sababu ya ugaidi na amani ya dunia hali kadhalika.

Mauaji ya Meksiko, yaliyotokea katika mpaka wa Tijuana na San Diego kwa sababu ya uhasama wa siku nyingi wa Kolonia Santita na Guanajuato wa himaya ya Sinaloa, hayakusababishwa na husuma au mgogoro wa Sinaloa peke yake.

Kilo 400 za kokeini, ambazo Kolonia Santita ilitaka kuziingiza San Diego kupitia San Ysidro lakini ikashindwa, na kilo 78 za bangi na methamfetamini ilizoziingiza San Diego kupitia Mto Tijuana, Baja California, Meksiko; na Ufuko wa Bahari wa Imperial, San Diego, California, Marekani; ndizo zilizosababisha mauaji ya kidhalimu ya Tijuana-San Diego – kwa kutupiana risasi, na silaha nyingine, kati ya ‘autodefensa’ (jeshi binafsi la Kolonia Santita) na polisi wa Tume ya Dunia (WPD) na maafisa wa polisi wa pande zote mbili za mpaka na ‘sicarios’ (wauaji wa kulipwa) wa Guanajuato.

Mbali na uhasama na madawa hayo hata hivyo, ambayo wengi huamini ndiyo pekee yaliyosababisha mauaji ya Meksiko, kuna kitu kingine cha hatari na kibaya zaidi kwa amani ya dunia kilichoyasababisha hali kadhalika, ambacho wengi hawajui na ambacho kwacho Tume ya Dunia ‘haikutaka’ kushirikiana na jumuiya ya kimataifa. Kolonia Santita ilikuwa na malighafi ya nyukilia, ‘Plutonium-239’, katika msitu mkubwa wa Amazoni nchini Kolombia; iliyoibwa na mwanafizikia wa Kolonia Santita (Martin Turner Smith, Ph.D.) kwa kiongozi wa Guanajuato (Roberto Mosquera Portocarrero ‘El Padrino’) miezi mitatu iliyokuwa imepita katika jiji la New Mexico nchini Marekani.

Vita iliyotokea San Ysidro kati ya Tume ya Dunia, Kolonia Santita na polisi wa Meksiko na Marekani ilisababisha watu zaidi ya 100 wasiokuwa na hatia wapoteze maisha yao; zaidi ya 200 walijeruhiwa vibaya na mali nyingi ziliharibiwa. Baina ya waliopoteza maisha ni askari 26 wa Tume ya Dunia (WPD). Kwa sababu ya kuzuia madawa kuingia Marekani na kuwakamata wahalifu, waliuwawa kwa risasi na hata kuchinjwa.

1 comment:

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...