Friday 26 May 2017

Sitakudharau Kwa Sababu Sikujui

Sipendi dharau: mimi kumdharau mtu au mtu kunidharau mimi. Sitakudharau kwa sababu sikujui. Hupaswi kunidharau kwa sababu hunijui.

Mzazi hamjui mtoto wake na mtoto hamjui mzazi wake. Kila mtu hapa duniani ni wa kipekee na wanasayansi wanatuambia kuwa tuko peke yetu hapa ulimwenguni. Lazima tujifunze kupendana na kuheshimiana.

Mama mmoja alimpenda sana mtoto wake hata akatoa jicho lake moja na kumpa mwanaye ambaye alipata ajali ya gari akiwa mdogo na kupofuka jicho moja. Mama na mtoto na mume wake walikuwa wakitokea Dumila, Morogoro, lakini walipofika Gairo gari lao dogo lilipinduka, lakini baadaye mume akafariki alipokuwa hospitalini Dodoma. Mama alikuwa na mapenzi yasiyokuwa na masharti yoyote kwa mtoto wake, na mtoto alionyesha mapenzi yasiyokuwa na masharti yoyote kwa mama yake.

Baada ya kumaliza masomo, kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Mazengo iliyokuwa pembezoni kidogo mwa mji wa Dodoma, mtoto alikwenda Ulaya kwa masomo zaidi. Akiwa huko akaoa lakini akamsahau kabisa mama yake pamoja na ndugu zake wote. Si kwa simu, si kwa barua, si kwa pesa! Miaka mingi baadaye mama akawa amemkumbuka sana mtoto wake hata akaamua kujichanga na akafanikiwa kupata hati ya kusafiria na viza kwenda Ulaya kumtafuta mwanaye.

Ulaya kuna Watanzania ambao huyo mama aliwafahamu, kupitia kwa waumini wenzake wa kanisa la Wasabato la Dodoma. Watanzania hao walimsaidia kusafiri kwa maana ya udhamini na tiketi ya ndege, kwani hata wao hawakupendezwa na tabia ya Mtanzania mwenzao.

Alipofika Lasembagi, ambapo ndipo mwanaye alikuwa akiishi na mke wa Kifaransa na watoto wao wawili, mama alielekezwa nyumbani kwa mwanaye na akachukuliwa teksi ambayo ilimpeleka moja kwa moja mpaka kwenye anuani ya nyumba yake. Cha kushangaza, yule mtoto akamkana mama yake na akamfukuza kama mbwa na mama akaondoka huku machozi yakimtoka katika jicho lake moja.

Miaka mitatu baadaye yule mtoto alikuja Tanzania kutalii akiwa na mke na watoto wao wawili. Wakiwa Dar es Salaam, watu wakampa taarifa za msiba wa mama yake. Nafsi ilimsuta. Hata mke wake nafsi ilimsuta pia! Walipotoka Manyara, ambapo walikwenda kuangalia wanyama, mke akamsihi mume wakahani msiba wa mama yake. Hivyo, wakasafiri kwenda Dodoma. Walipofika Area C, nyumbani kwa mama yake, walikutana na majirani. Mama mmoja akamkabidhi yule mtoto barua aliyopewa na marehemu ili amkabidhi palipo majaaliwa.

Barua ilikuwa na ujumbe mzito na wa kusikitisha. Mama alimwomba radhi mtoto wake kwa makosa yoyote ambayo labda aliwahi kumfanyia. Hakukumbuka kama aliwahi kumfanyia mwanaye makosa ya aina yoyote ile licha ya kumchapa, kwa faida ya mtoto mwenyewe ya baadaye. Barua ilikuwa ndefu. Lakini ilimalizia kwa kusema, “Nilikupenda mwanangu, nakupenda hata sasa, na nitakupenda daima. Siku yoyote Mungu atakapokupa neema ya kurudi, kama nitakuwa hai, nitakuchinjia kuku; kama nitakuwa nimekufa, nitatumia mifupa yangu kukukumbatia.”

Yule mama hakuwa na makosa. Mtoto alikuwa na makosa. Lakini hawa walikuwa ni watu wawili tofauti, kabisa! Mama hakumjua mtoto wake, na mtoto hakumjua mama yake. Mama hakujua kama mtoto wake alikuwa na akili ya kumgeuka. Mtoto hakujua kama mama yake alimpenda kwa dhati!

Kuna nguzo saba ambazo hazina budi kuzingatiwa kama unataka kuheshimiwa na kuwaheshimu wengine. Kwanza kabisa jitambue: wewe ni nani na unafanya nini hapa duniani. Halafu, kabla ya kusema jambo lolote kwa mtu yoyote fikiria kwanza maana au madhara ya hilo unalotaka kulisema. Kisha jifunze tamaduni mbalimbali na watendee wengine kama vile unavyotaka kutendewa au kama vile wanavyotaka kutendewa. Jifunze kusamehe na kusuluhisha migogoro katika jamii unamoishi huku ukidumisha heshima na utu kwa binadamu wenzako. Jijengee imani kwa watu, punguza upendeleo, fanya kazi kama timu kwani hakuna ‘mimi’ katika umoja ila kuna ‘sisi’, na jitahidi kwa kadiri ya uwezo wako WOTE kwa manufaa ya wote. Kuwa kiongozi katika kila jambo unalofanya na katika kila kitu unachofanya. Jitahidi kufanya jambo au kitu kwa usahihi kwa kadiri utakavyoweza.

Migogoro inatokea kwa sababu watu wameshindwa kuheshimiana. Ukijiheshimu na ukaheshimu wengine, utaacha dunia katika hali nzuri kuliko ulivyoikuta.

2 comments:

  1. Ukitaka kuwa na mahusiano mema na watu wa muhimu katika maisha yako, waheshimu. Heshima yako itakulipa!

    ReplyDelete
  2. Tuko peke yetu ulimwengu mzima halafu bado tunagombana na kudharauliana!

    ReplyDelete

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...