Redio, sawa na ile iliyotumika kuangusha ndege ya Pan Am mwaka 1988 huko Uskochi nchini Uingereza, Toshiba RT-SF 16, sawa na ile iliyotumika kuangusha ndege ya Air France mwaka 1992 huko Sittard nchini Uholanzi.
Paris nchini Ufaransa kikao cha CS-Paris kilikuwa kikiendelea nyumbani kwa Roger Prideux (‘The Dynamite’) Saint Germain saa kumi na mbili jioni, karibu na ukingo wa kushoto wa Mto Seine (La Sorbonne, Chuo Kikuu cha Paris) na kanisa kongwe kuliko yote mjini Paris la Saint Germain-des-Pres.
Katika nyumba hiyo ya kona, juu kabisa ghorofa ya tatu, watu kumi walikuwa sebuleni wakiongelea kifo cha John Murphy: Roger Prideux, Marie Pessin Payan, Monique Desmarais, Raymond Marse, Bernadette Kirouac Santere, Colette Nageotte, Giovanna Garcia, Sebastian Garnier, Patricia Boicourt na Gaston Pierre Bastarache (‘The Circuit’).
“Hatuwezi kwenda Amsterdam kwa gari au treni au kitu kingine chochote isipokuwa ndege – kuna hatari ya kukamatwa,” alisema Circuit.
“Sanduku halitakuwa na kitu …” alisema Prideux.
“Sanduku lazima liwe na kitu! Hatuna muda! Ndege inafika saa 1:05 asubuhi Amsterdam, utapata wapi muda Prideux?” Garnier alipinga vikali.
“Hii ni saa kumi na mbili, jamani. Tuna kila kitu. Tuhangaike mpaka saa nne halafu Prideux aondoke saa sita kwenda Le Bourget,” alisema Monique.
“Naam. Ili afike Amsterdam saa nane, au tisa na kwenda moja kwa moja uwanjani,” Circuit aliunga mkono.
“Kwa hiyo tunakodi ndege?” Giovanna aliuliza.
“Ndiyo njia pekee, Giovanna,” Circuit alijibu.
“Circuit, kama ni ndege tutachelewa,” Marie alilalamika.
“Hatuwezi kuchelewa ... Cha msingi tumtengeneze huyo ‘mtoto’ haraka kisha tumkimbize Prideux Le Bourget akachukue Cessna. Nina watu katika kampuni ya ndege,” alisema Circuit.
Juu ya meza kulikuwa na redio tatu kubwa: Sony, JVC na Toshiba. Toshiba RT-SF 16 ya spika moja Prideux alikuwa ameikongoloa yote na kila mtu alikuwa akiangalia ufundi wake. Pamoja na redio, juu ya meza kulikuwa na vitu vingine mbalimbali: vitambulisho kadha wa kadha na pasipoti za bandia, lundo la silaha, nyaya, vyuma, sanduku, saa na baruti.
Roger Predeaux alipomaliza kutengeneza bomu na kulitegesha ndani ya redio ya Toshiba (Toshiba RT-SF 16) alisafiri mpaka Amsterdam ambapo alipanda Air France na kusafiri nayo mpaka Paris, Ufaransa.
Akihakikisha John Murphy hashuki kutoka katika ndege, Roger Predeaux alisubiri kwa nje mpaka Air France iliponyanyuka tena na kuondoka kuelekea Copenhagen, yeye na wenzake wakijua John Murphy hangepata nafasi ya kuishi tena.
No comments:
Post a Comment