Los Pinos, ndani ya msitu mkubwa wa Chapultepec, inayofanana sana na Ikulu ya Marekani ya White House, si nyumba moja ya kawaida. Ni mkusanyiko wa nyumba nyingi maridadi; zilizopewa majina ya marais wa zamani wa Meksiko kama vile, Lázaro Cárdenas, Benito Juárez, Miguel Alemán na Adolfo Ruiz Cortinez.
Nyumba ya Debbie ilikuwa kando ya nyumba ya Adolfo Ruiz Cortinez; karibu na ziwa dogo la kutengenezwa, masanamu ya shaba ya marais wa zamani wa Meksiko, chemchemi ya maji ya bomba, nyumba za wafanyakazi (wa Rais wa Meksiko) na nyumba ya Rais wa Meksiko. Nyumbani kwa Debbie Patrocinio Abrego.
Nani alijua kama mtu kutoka Tanzania angeweza kupendwa Meksiko na mtoto wa rais? Los Pinos (Mikadi), Ikulu ya Mexico City, ndani ya msitu mkubwa wa hekta 686 wa Chapultepec (kilima cha panzi), ilichangia kwa kiasi kikubwa kubadilisha historia ya Tume ya Dunia; pamoja na kwamba Murphy na Mogens walifanya kosa (kubwa) kuonana na Debbie na Lisa katika Baa ya Desierto de Los Leones, San Ángel, kusini-magharibi mwa Mexico City.
Nyumba ya Debbie ilikuwa na vyumba viwili vya kulala, sehemu ya kulia chakula, sebule, maktaba, ukumbi wa sinema na mabafu manne na nusu. Chumbani (chumba cha kulala cha Debbie) kulikuwa na kitanda kikubwa cha hadhi ya kifalme, makochi ya kumeremeta, televisheni, zulia nene jipya jeupe, mapazia ya dhahabu ya Taffeta, kofia ya taa ya dhahabu (‘chandelier’, shandalia - Kamusi ya Enock Maregesi) ya Baccarat; na vitu vingine vingi vya kibunifu.
Sebuleni, miongoni mwa vitu vingi, kulikuwa na picha tatu kubwa alizozipenda Debbie kuliko zingine zote: Frida Kahlo, msanii maarufu wa picha za rangi wa karne ya ishirini wa Meksiko, shujaa wa maisha ya Debbie; Marciano Moreno Herrera, mchumba wa Debbie aliyeuwawa huko Tijuana na ‘autodefensa’ ya Kolonia Santita; na Wanda Castellanos, mtoto wa Panthera Tigrisi, El Tigre, aliyekuwa akisoma na Debbie katika Chuo Kikuu cha Guadalajara huko Jalisco. Chumba cha Debbie (mbali na nyumba) kilikuwa na thamani ya dola za Kimarekani milioni moja na ushei.
No comments:
Post a Comment