Thursday, 16 February 2017

Москва-река

Mto Moscow, Москва-река, mto wa magharibi mwa Urusi unaopita katikati ya jiji la Moscow kutokea magharibi kwenda mashariki na kumwaga maji yake katika Bahari ya Kaspi, ulitumiwa na magaidi wa Kolonia Santita kumsafirisha Mpelelezi wa Tume ya Dunia John Murphy Ambilikile (wa Tanzania) kutoka Smolenskaya Prospekt mpaka katika ‘dacha’ ya Kolonia Santita ya Yugo Zapadnaya.

Wakati teksi ya Murphy ikisimama Teatralny Proezd, upande wa kusini wa Hoteli ya Metropol – karibu na mojawapo ya minara ya mwanzo ya Kitay-gorod, kitovu kikuu cha biashara cha Moscow ya kale – kwa matatizo ya injini, magaidi waliendelea mbele na kusimama mkabala na Jumba la Maonyesho ya Tamthilia la Bolshoy; halafu wawili kati yao wakashuka na kuingia ndani ya kioski. CS-Moscow walijua Murphy alishawahisi. Kusimama kwake Metropol alikuwa akitafuta uthibitisho wa wao walikuwa akina nani. Ndani ya Bentley, wawili waliposhuka, wawili kati yao walibaki. Walimchunguza Murphy kila nukta ili asiwapotee.

Murphy hakuwajali. Wala hakushtuka chochote. Aliendelea tu kutembea na sanduku lake, mpaka alipokutana na njia mbili: moja chini ya ardhi na nyingine juu ambayo ndiyo aliyoamua kuifuata. Chini kulikuwa na watu wengi. Hakutembea sana akawa amefika Krasnaya Ploshchad (Uwanja Mwekundu – ‘Red Square’), eneo la shughuli za kiserikali na kitovu cha biashara cha Moscow ya leo – ambapo ndipo utapata njia ya mkato kirahisi kwenda WODEC.

Mbele kidogo ya ‘Red Square’, Murphy alikamata barabara nyembamba ya kushoto na kuendelea kutembea kwa hasira huku sasa akiziona ofisi za tume meta kama mia nne hivi mbele yake kushoto. Alipofika Smolenskaya Ploshchad (Uwanja wa Smolenskaya), kabla hajavuka barabara kuingia Smolenskaya Prospekt – katika ofisi za Tume ya Dunia – kitu ambacho Murphy alikitegemea kilitokea! Bentley, ile gari ya majambazi, ilifunga breki ghafla. Watu watatu wakashuka, chapuchapu, na kumrusha Murphy ndani ya gari. Halafu wakaondoka kwa mwendo mkali, bila kujali theluji, wakielekea Yugo Zapadnaya.

Majambazi wale, walioshikilia bastola kikakamavu na kwa ufundi, walimzunguka Murphy upesiupesi: mmoja akikamata sanduku kwa hali ya unyang’anyi na kutangulia nalo kwa fujo ndani ya gari; wengine wakimsukuma kwa nguvu mpaka katika viti vya nyuma vya gari yao – na dereva kuendesha, kwa mwendo mkali ambao kwa vyovyote haukufaa kuendeshwa katika barabara za Moscow!

Ndani ya Bentley, magaidi walimpekua Murphy na kukuta alikuwa na bastola moja kubwa. Zingine hawakuziona. Murphy alipojaribu kuuliza walipokuwa wakimpeleka na kwa nini walimteka, walimwangalia kwa dharau na hasira na kuendelea kuendesha; bila ya kusema chochote. Murphy aliona atulie. Wangeweza hata kumuua kama angeendelea kuwasumbua.

Baada ya dakika kama ishirini hivi kutoka Mto Moscow, Москва-река, Murphy na watekaji wake walikutana na uwanja mkubwa wa michezo wa kumbukumbu ya Lenin (Kiongozi wa Mapinduzi ya Oktoba na Rais wa kwanza wa Sovieti aliyekufa Januari 21 mwaka 1924; na ambaye mpaka leo mwili wake bado umehifadhiwa, kwa madawa maalumu, mkabala na duka la serikali la kujihudumia mwenyewe la GUM, mbele ya ukuta wa Ikulu; hivyo kuvutia watu, malaki ya watu, kila mwaka kutoa heshima zao za mwisho – kwa mmojawapo wa viongozi wakuu duniani wa karne ya ishirini) kabla ya kuuvuka na kuungana na Yugo Zapadnaya. Katika Hosteli za Chuo Kikuu cha Lumumba, Miklukho-Maklaya, Bentley ilisimama mbele ya ‘dacha’ (nyumba ya nje ya mji) iliyozungukwa na miti mingi kama Uwanja wa Lenin wa Michezo ya Olimpiki.

Milango ya Bentley ilifunguliwa, halafu dereva na kijana mwingine wakateremka kwanza na kuanza kucheki usalama. Kwa amri kali Murphy alishushwa halafu wote kwa pamoja wakaingia ndani ya ‘dacha’ mpaka sebuleni; ambako hata hivyo hapakupendeza sana.

No comments:

Post a Comment

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...