Gari
 la Vijana wa Tume walilopewa na Jeshi la Anga la Meksiko kwa 
makubaliano maalumu na Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya, 
Mercedes Benz, lilivyosambaratishwa na kombora la magaidi wa Kolonia 
Santita katika barabara ya Mexico City ya Gobernador Ignacio Esteva, 
karibu na Ubalozi wa Urusi, lilipokuwa njiani kuelekea Álvaro Obregón 
katika makao makuu ya Kolonia Santita ya Kiwanda cha Dongyang 
Pharmaceuticals. Vijana wa Tume walikuwa na mtoto wa Rais wa Meksiko, 
Debbie Patrocinio Abrego. 
Mkurugenzi
 wa Usalama wa Tume ya Dunia Christoffer Sortevik aliwaagiza Vijana wa 
Tume wafuate maelekezo yake watakapokuwa Mexico City. Mojawapo ya 
maagizo hayo ni kwenda San Ángel, Álvaro Obregón, kupitia Lazaro 
Cardenas, Pedro Moreno, Paseo de la Reforma, Manuel Avila Camacho katika
 Baraste Kuu ya Anillo Periférico, Adolfo Lopez Mateos, Barranca del 
Muerto, Avenida Insurgentes Sur, na Avenida de la Paz; lakini wao 
wakakaidi agizo hilo na kuchukua njia ya mkato ya kupitia 16 de 
Septiembre, ili wafike Amargura dakika ishirini kabla ya muda waliopanga
 kufika huko. Amargura ni barabara iliyoko ndani ya kitongoji cha San 
Ángel, iliyoko katika wilaya ya Álvaro Obregón, kusini-magharibi mwa 
Mexico City. 
Gari
 lao aina ya Mercedes Benz lilipofika Gobernador Ignacio Esteva, 
barabara nyembamba iliyokuwa na mitaro ya maji machafu kwa pembeni na 
taa za kuongozea magari, karibu na Hospitali ya Mocel na Ubalozi wa 
Urusi, lilisimamishwa na askari wawili wa barabarani. Vijana wa Tume 
walikuwa na kibali cha kuvunja sheria cha wiki mbili; lakini bado 
Mogens, aliyekuwa akiendesha, akasimamisha gari. 
Mogens
 alifungua kioo kumsikiliza askari mmoja kati ya wale wawili; huku 
Murphy, Yehuda na Radia wakiwa makini kwa lolote lakini Debbie akiwa 
hashangai sana. Vijana wa Tume walishangaa. Tangu waingie Meksiko 
walikuwa hawajaona askari wa barabarani hata mmoja. Lakini Debbie 
akawahakikishia ya kuwa hicho hakikuwa kitu cha kushangaza sana kwa 
Mexico City. 
Murphy
 alimsihi Mogens waondoke kwani walikuwa na kibali cha serikali cha kuwa
 juu ya sheria kwa angalau majuma mawili, kilichotolewa pamoja na 
‘D-Notice’ ya kuwazuia wahariri wa vyombo vya habari nchi nzima 
kuchapisha taarifa za Vijana wa Tume katika kipindi chote cha Operation 
DC, lakini Mogens akabisha na kusema haikuwa busara kutumia ubabe katika
 nchi ya watu. 
Bila
 kujua Mogens alikuwa amefanya kosa. Alikuwa amefanya kosa kubwa la 
tatu. La pili lilikuwa kukiuka njia ya Sortevik. La kwanza lilikuwa 
kudharau ratiba ya tume na Murphy na Mogens kuondoka na Debbie na Lisa 
katika Baa ya Desierto de Los Leones! Wale hawakuwa askari wa barabarani
 wa kawaida. Zilikuwa njama hatari za magaidi wa Kolonia Santita 
waliosambaa kila kona ya Barabara ya Ignacio Esteva, mpaka Hospitali ya 
Mocel na Ubalozi wa Urusi. 
Gari
 la Vijana wa Tume liliposimama, na Mogens kuongea na askari polisi wa 
barabarani, kitu cha hatari kilifanyika katika gari lao bila wao wenyewe
 kujua. Askari mmoja, mwenzake na yule mwingine, alipenya harakaharaka 
na kupachika kitu katika chasisi ya gari la Vijana wa Tume; halafu 
akatoka na kuelekea upande wa pili wa barabara, ambako aliingia ndani ya
 gari na kuondoka. 
Dereva
 wa gari moja la nyuma ya gari la Vijana wa Tume hata hivyo, aliona 
picha yote lakini akaogopa kusema au kufanya chochote. Alijua walikuwa 
majambazi, na hakutaka shida. Lakini nafsi ilimsuta. Hakuvumilia kuona 
alichoona. Hivyo, aliamua kuwapa taarifa Vijana wa Tume; bila majambazi 
kumwona, kwa sababu hakujua walikokuwa wamejificha. 
Baada
 ya wale askari wawili wa Kolonia Santita kufanya uchunguzi wao wa 
mwisho katika gari la Vijana wa Tume na magari mengine, waliondoka na 
kuruhusu magari yaendelee na safari zake. Wakati huohuo gaidi mwingine, 
pembeni ya barabara, ndani ya gari ndogo nyeusi, alikamata kidhibiti cha
 kulipulia mabomu akiwa na wasiwasi mno na kuchomoa waya wa mawasiliano.
 Wakati huo Mogens alikuwa ndiyo kwanza anaondoa gari bila kujua 
kilichokuwa chini ya gari lao, wala kilichokuwa kikiendelea hata katika 
magari ya watu wengine. 
Gari
 la nyuma lilivuta mwendo kuwa sawa na gari la Vijana wa Tume. Sambamba 
kabisa na gari lao, msamaria mwema wa lile gari lingine alishusha kioo 
na kuwapa ishara ya kufungua kioo. Lakini Mogens akasita. Alidhani 
ulikuwa mtego. Wote walikuwa makini ghafla na kujiuliza nini kilikuwa 
kikiendelea! Yule bwana alivyozidi kuwatupia ishara, Radia alimwambia 
Mogens afungue kioo. Kama ni kushambuliwa wangeshambuliwa tu; kwani gari
 la Vijana wa Tume lilikuwa na inchi mbili tu za vioo vya kuzuia risasi.
 Harakaharaka Mogens alishusha kioo na kumsikiliza msamaria, ambaye sasa
 alikuwa amechomoza kichwa nje kwa wasiwasi mkubwa. 
“Bomu chini ya gari yenuu!” msamaria mwema alipiga kelele na kurudisha kioo upesi, halafu akaongeza mwendo na kupotea. 
Kelele
 ya msamaria mwema iliwaachia Vijana wa Tume maswali mengi. Hawakujua 
kwa nini yule mtu alisema vile na wala hawakujua bomu alilosema 
lilivyowekwa chini ya gari lao wala muda wenyewe wa kuliweka. Murphy 
alimshika Debbie, kwa nguvu zake zote, na kufungua mlango. 
Yule
 gaidi wa kidhibitimbali alirekebisha antena halafu akakunja uso. Kwa 
hasira alibonyeza kitufe cha kulipulia, mambo yakawa mengine kabisa 
katika gari la Vijana wa Tume. 
Ulisikika
 mlio wa moja kwa moja chini ya gari la Vijana wa Tume, kabla ya 
Mercedes kulipuka vibaya, vibaya sana na kutawanyisha vyuma kila mahali 
mithili ya volkano! Kama vitu visivyokuwa na uzito Vijana wa Tume 
walirushwa juu hali kadhalika, na kuangukia barabarani, kila mtu 
akianguka vibaya na kulala sehemu yake.

No comments:
Post a Comment