Heroini hutokana na mmea wa maua uitwao mbaruti-afyuni, ‘oppium 
poppy’, jamii ya mimea ya mibaruti (‘poppy’) inayopatikana katika sehemu
 mbalimbali za dunia hususan katika bara la Asia. Mbaruti-afyuni ni mmea
 mrefu wenye kirungu kidogo kwa juu kama tunda hivi, lenye maua kidogo 
kwa juu yake. Tunda hilo ambalo hujulikana kama tumba au jicho la ua au 
‘poppy pod’ au ‘bud’ kwa utaalamu zaidi, linapokomaa hupasuka na kutoa 
maua mazuri mekundu ambayo baadaye hutumika kama mapambo katika nyumba 
za watu.
Licha ya kutumika kama mapambo katika nyumba za watu na katika 
sherehe mbalimbali za kimila, mbaruti-afyuni hutumika kwa kutengenezea 
chakula na madawa ya kulevya hali kadhalika; kwa sababu za kiuchumi na 
kiutabibu. Kabla tunda halijaiva na kupasuka, wakulima – kwa kutumia 
nyembe maalumu – hulikata kwa kulichanja na kutoa afyuni (au utomvu au 
kasumba au ‘latex sap’ au ‘opium’) au ‘machozi ya mbaruti’.
Ndani ya afyuni (utomvu unaotumika kutengenezea heroini) kuna 
asilimia 12 ya morfini na kemikali zingine za kialkaloidi zinazojulikana
 kitaalamu kama ‘opiates’, kama vile thebaini (‘paramorphine’) na kodini
 (‘3-methylmorphine’). Morfini hiyo baadaye hushughulikiwa kikemia na 
kutengeneza heroini na madawa mengine kwa ajili ya sayansi na utabibu. 
Kwa hiyo afyuni inatengeneza morfini na morfini inatengeneza heroini.
Aidha, baada ya kutoa afyuni yote ama kwa mikono au kwa mashine, 
tunda hupasuliwa na kutoa mbegu nyingi ndogondogo zilizokuwemo ndani. 
Mbegu hizo zenye mafuta huweza kuliwa kama chakula, au huweza kukamuliwa
 na kutoa mafuta kwa ajili ya kupikia na kwa ajili ya matumizi mengine.
Afyuni huzalishwa katika maeneo manne tu ya dunia nzima: 
Afuganistani, Kusini-Mashariki mwa Asia – ikiwemo Bama na Tailandi, 
Amerika ya Kusini hasa Kolombia, na Sinaloa nchini Meksiko. Afuganistani
 ndiyo inayoongoza duniani kwa kuzalisha afyuni, kuliko nchi nyingine 
yoyote ile, ikiwa imefikia hadi kiwango cha asilimia 90.
Kutengeneza heroini si kazi ngumu hata kidogo. Unachohitaji ni 
kemikali tu za kawaida pamoja na maji mengi. Baada ya kuvunwa, afyuni 
huchemshwa na chokaa au kalisi na kutengeneza morfini inayoweza 
kuyeyushwa na maji. Kisha morfini hiyo huchujwa na kuchemshwa tena, 
lakini sasa na madini ya shabu, ili kupata morfini ya poda iliyokauka. 
Mamafia hupakia poda hiyo katika vifurushi na kuipeleka katika maabara 
za mafichoni katika milima ya Afuganistani, ambako morfini 
hushughulikiwa kitaalamu na kutengeneza heroini. Kutoka Afuganistani 
heroini husafirishwa mpaka Irani na Pakistani. Huko husafirishwa kwa 
njia ya anga, maji na ardhi; mpaka Urusi, Ulaya ya Mashariki, Uturuki, 
China na Afrika ya Magharibi. Uturuki na Afrika ya Magharibi ni vituo 
vikuu vya usafirishaji wa madawa yanayokwenda Afrika, Ulaya na mabara 
yote ya Amerika.
Chokaa ni ‘slaked lime’, kalisi ni ‘calcium’ lakini kalisi 
inayotengeneza heroini ni ‘calcium hydroxide’; na madini ya shabu ni 
‘ammonium chloride’.
Mtumiaji wa heroini huweza kuivuta kwa mdomo, kwa pua, kwa kujidunga 
kwa sindano katika mishipa ya damu au kwa kujidunga kwa sindano katika 
sehemu za siri. Wale wanaochanganya bangi na heroini huwa wanavuta 
heroini kwanza kwa msokoto wa bangi, ambao haujawashwa, kisha, baada ya 
heroini kwisha, ndipo wanawasha msokoto na kuvuta bangi kama sigara ya 
kawaida. Hivyo, heroini haivutwi kama sigara.
Sindano katika vena inalewesha kwa ufanisi zaidi kuliko njia zingine 
za utumiaji wa heroini. Njia ya pili kwa ufanisi ni njia ya sehemu za 
siri ikifuatiwa na kuchemua. Sindano huchukua sekunde chache kumlewesha 
mtu, wakati kuvuta kwa pua (kuchemua) huchukua mpaka dakika 15. Mtu 
anapojidunga heroini, heroini husafiri katika mkondo wa damu hapohapo na
 kupenya kinga ya damu na ubongo kichwani. Inapoingia katika ubongo 
heroini hubadilika kikemia na kuwa morfini, na kufurika katika sehemu 
yote ya mfumo wa ubongo inayoshughulika na furaha, na kumfanya mtumiaji 
ajisikie raha ya kupindukia. Tabia hiyo ikiendelezwa kwa muda mrefu 
heroini hubadili muundo na kazi ya ubongo na kumwingiza mtumiaji katika 
utegemezi na uraibu usio na kifani wa madawa ya kulevya. Ukishakuwa teja
 umejitia kifungoni. Usipo’kita’ (usipo’fix’), usipopata dozi ya 
heroini, utaugua kitu kinaitwa ‘ugonjwa wa heroini’ (au ‘dope 
sickness’). Utajisikia homa, kutetemeka, kutapika na maumivu ya misuli.
Ma Nang Nyi, binti mpendwa wa Kamishna-mlezi wa Kanda ya 
Asia-Australia ya Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya U Nanda, 
alipojidunga sindano ya heroini na kuzidisha dozi bila kujua huko Bama, 
alianza kufifia na kuishiwa na nguvu. Kiasi kikubwa cha heroini 
kinapofurika katika ubongo wa mtumiaji mfumo wa kupumua huathirika kwa 
kiasi kikubwa na mwili husahau kupumua. Mtumiaji anakuwa mahututi. 
Asipofanyiwa huduma ya kwanza haraka, heroini itashinda vita na moyo 
wake utasimama kupiga.
Miaka miwili baadaye, baada ya Nang Nyi kufa kwa kuzidisha dozi ya 
heroini bila kujua huko Rangoon; mpenzi wake (Ko San Pe) alipelekwa 
katika kliniki ngumu kuliko zote duniani ya Tham Krabot, inayomilikiwa 
na watawa katika milima ya Tailandi, kwa ajili ya tiba ya heroini na 
ulevi sugu wa pombe. Lakini mwaka 1982 naye akafariki dunia, kama mpenzi
 wake Ma Nang Nyi. Hiyo ikawa sababu ya U Nanda kuisaliti KGB na 
kujiunga na Tume ya Dunia ili apambane na madawa ya kulevya kwa nguvu 
zake zote.
Watumiaji wengi wa heroini huanza na dawa za kupunguza maumivu kama 
vile ‘oxycodone’ (‘oxys’) ambazo hupatikana kwa wingi katika maduka ya 
dawa. Miezi minne hivi daktari anapositisha utoaji wa ‘oxys’ kwa 
mgonjwa, mgonjwa anakuwa tegemezi wa dawa hizo na kujenga uraibu. 
Mgonjwa anaposhindwa kupata dawa hizo kihalali kwa maagizo ya daktari 
huzipata kwa walanguzi wa mitaani na kuzinunua, lakini kwa bei ya juu.
Kidonge kimoja cha ‘oxys’ huuzwa kwa Tsh. 120,000 mpaka Tsh. 200,000 
na mtu huweza kutumia hata vidonge vitano kwa siku. Uraibu wa ‘oxys’ 
unapoongezeka, na mgonjwa hana tena hela ya kununulia vidonge, mgonjwa 
uhamia katika kuiba kwa ndugu, jamaa na marafiki kukidhi haja ya 
‘oxycodone’. Huko Marekani kumekuwa na matukio mengi ya watu kuvamia 
maduka ya dawa na kuiba ‘oxys’ kwa unyang’anyi; na hivyo wengi kukamatwa
 na kushtakiwa na kufungwa jela.
Tofauti kati ya ‘oxycodone’ na heroini ni kwamba heroini hupatikana 
kwa urahisi, ina nguvu zaidi, na hugharimu kiasi kidogo tu cha pesa. 
Hata hivyo, zote hizo zina madhara sawa katika ubongo na uridhishaji 
wake hautofautiani. Kadiri utakavyotumia ndivyo utakavyohitaji na ndivyo
 utakavyoumia.
Morfini, thebaini na kodini ni alkaloidi zinazopatikana ndani ya 
afyuni – kutoka kwenye mmea unaojulikana kitaalamu kama ‘Papaver 
somniferum’. Kwa jumla hujulikana kama ‘opiates’. Morfini hutengeneza 
heroini, thebaini hutengeneza ‘oxycodone’, kodini hutengeneza ‘naproxen’
 ambayo ni dawa ya homa. Heroini hubadilikia ndani ya ubongo kuwa 
morfini, wakati kodini hubadilikia ndani ya ini kuwa morfini hali 
kadhalika.
Watu hutumia vibaya ‘opiates’ kuliko kokeini, eksitasi na methi kwa 
pamoja. ‘Opiates’ zingine ni kama ‘hydrocodone’ (ambayo ni dawa ya 
maumivu), ‘xanax’ (ambayo ni dawa ya msongo wa mawazo) na ‘percocet’ 
(ambayo pia ni dawa ya maumivu).
Uraibu wa heroini si rahisi kupona katika kliniki za kawaida. Watu 
walioathiriwa na dawa hiyo wanapaswa kujaribu kupelekwa katika kliniki 
bora zaidi kama vile Betty Ford Center (iliyoko Rancho Mirage, 
California, inayojihusisha zaidi na ulevi sugu wa pombe) au Tham Krabok 
ambapo waathirika huishi kama watawa na kutumia dawa za ajabu kwa muda 
wa majuma manne mfululizo, ambapo kila mtawaliwa lazima ale kiapo cha 
‘sajja’ (nadhiri) kabla ya kuanza matibabu. Unaambiwa na mkuu wa watawa 
uachane kabisa na dawa za kulevya. Hutakiwi kuvunja kiapo hicho hadi 
mwisho wa matibabu yako.
Watawaliwa wengi wa madawa ya kulevya katika nyumba ya Tham Krabot 
(iliyoko Saraburi, Tailandi) huwa hawamalizi dozi, kwa sababu ya ugumu 
wa dozi yenyewe na ugumu wa maisha kwa jumla. Lakini ukimaliza dozi 
LAZIMA upone.
Kadiri unavyozidi kupanda juu ndivyo utavyoanguka vibaya. Kadiri 
unavyozidi kutumia madawa ya kulevya ndivyo madhara yake yatakavyokuwa 
makubwa. Hivyo acha, wakati bado mapema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Roho Yako
289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...
- 
KITENDAWILI CHA KOLONIA SANTITA Shilingi milioni moja za Kitanzania kushindaniwa ndani ya miezi sita kuanzia leo Swali: Kila namba ...
 - 
Mpelelezi wa Tume ya Dunia kutoka Jerusalem, Israeli, Kanali Daniel ‘Yehuda Ben-Asher’ Ebenezer, Daniel Yehuda, alikuwa komandoo wa kit...
 

Wazazi wapelekeni watoto wenu Tham Krabot au Betty Ford Center, wakapone uraibu wa heroini na pombe. Tham Krabot chakula, dawa na matibabu ni bure! Lakini maisha ni ya ustahamilivu.
ReplyDelete