Friday 30 December 2016

Ijue Dawa ya Kulevya Hatari Zaidi Kuliko Madawa Yote Duniani Iitwayo Methamfetamini – Yenye Kiwango cha Kustarehesha cha Asilimia 1200 Zaidi ya Kokeini, Heroini na Bangi kwa Pamoja – Inayoweza Kusababisha Kiharusi, Ugonjwa wa Moyo, na Hata Kifo

Methamfetamini (methi) ni dawa hatari inayodumu mwilini kwa muda mrefu na yenye gharama ndogo kuliko eksitasi na kokeini ya mawe. Inaweza kuingia mwilini kwa kudungwa, kuvutwa, au kuchemuliwa, na mkito mmoja huweza kumlewesha mtu kwa kadiri ya masaa manne hadi manane bila kupungua. Methi inalewesha zaidi kuliko konyagi au kokeini. Wale wanaotumia ‘oxycodone’ mara nyingi uhamia kwenye heroini. Wale wanaotumia kokeini uhamia kwenye methi.

Wauzaji wadogowadogo wa methi – ‘Pet dealers’ – inayojulikana kwa majina ya mtaani kama ‘crank’, ‘crystal’, ‘glass’, ‘hielo’, ‘tik’ au ‘ice’, huuza madawa mitaani kwa ajili ya viongozi wa magenge yao. Ukifanya kazi yako vizuri unaweza kupanda cheo kutoka muuzaji wa mtaani mpaka msafirishaji wa kimataifa. Ukishakuwa msafirishaji wa kimataifa, unaweza kwenda Meksiko na kufanya biashara na mamafia wa mashirika ya madawa ya kulevya ya huko wewe binafsi. Unaweka oda na kutuma pesa kwenda Meksiko, ambako mamafia hupika methi kwa ajili yako, katika maabara kubwa za methi za mafichoni. Unaweza kulipa Tsh. 76,500,000 kwa kilo 6 za methi. Oda ya kilo 6 ina thamani ya mtaani ya Tsh. 810,000,000. Mamafia husafirisha methi kutoka porini hadi kwenye mpaka wa California na Meksiko, ambako wasafirishaji huipokea na kuvuka mpaka kuingia Amerika.

San Ysidro (San Sidro, hadithi ya Kolonia Santita ilipoanzia) ni eneo lililoko katikati ya Tijuana, Meksiko na San Diego, California. Hapo kuna mpaka mkubwa na wenye mishughuliko mingi kuliko yote ya kimataifa duniani; na ni eneo ambalo Marekani imelipa kipaumbele kikubwa katika vita yake dhidi ya madawa ya kulevya.

Wasafirishaji mara nyingi huwa na magari yenye vyumba vingi vya siri. Wana njia nyingi za kuondoa harufu ya madawa ili mbwa wa kipolisi wasiyanuse. Vyumba vya siri huweza kuzibwa kabisa (‘vacuum sealed’) kuondoa harufu ya madawa ilimradi mbwa wasinuse chochote.

Wanaposubiri kwenye foleni za magari kwa masaa mengi, wasafirishaji hukatisha mpaka na kuelekea kwenye maghala kadha wa kadha ya madawa ya kulevya (‘stash houses’) katika Jimbo la California. Wanapofika katika majumba yao (baada ya kutoka kwenye maghala) mara nyingi wasafirishaji hao huchanganya methi na kitu kinaitwa SMS, ambacho ni chakula cha farasi. Ukichanganya gramu 227 za SMS utapata asilimia 50 ya methi, yaani iliyochanganywa, na kuwadanganya wateja kama ni methamfetamini safi isiyokuwa na doa.

Methi hununulika sana. Kadiri ilivyoingia (kwa maana ya uharaka) ndivyo itakavyotoka. Wasafirishaji hutakiwa kubeba mzigo wa kutosha wa hata wiki nzima, kukidhi mahitaji ya wateja; labda kilo 2 mpaka 5 hivi. Wasafirishaji hao wakati mwingine wanaweza kuuza hata kilo 25 mpaka 40 kwa mwezi kulingana na jinsi watakavyokwepana na vyombo vya dola.

Katika maabara za methi kule Meksiko kuna madumu makubwa ya bluu yenye mifuniko myeusi. Hapo wafanyakazi wa mamafia hubadilisha kemikali za kutengenezea methi (‘ephedrine’ na ‘pseudoephedrine’) katika chapa ya kwao wenyewe, na kuiuza kama Methi au Glasi ya Meksiko nchini Marekani na duniani kwa jumla. Mfanyabiashara mmoja wa methamfetamini huweza kujiingizia kipato cha mpaka Tsh. 80,000,000 kwa wiki.

Mamafia huzalisha takriban tani 200 za methamfetamini kwa soko la Marekani pekee kila mwaka, zenye mapato ya makadirio ya Tsh. 14,000,000,000,000 (trilioni 14). Biashara ya methi ya Meksiko hutegemea sana mamia ya wafanyabiashara na wasafirishaji wa madawa ya kulevya wa mataifa mengine. Kukidhi haja ya matakwa hayo kunahitajika uingizaji wa kiwango cha juu wa viambato vya kikemikali (‘chemical ingredients’).

Kupata kemikali hizi tangulizi (‘precursors’), mamafia wa Meksiko husafiri mpaka Asia ambako ndiko kuna chanzo kikuu cha ‘ephedrine’ na ‘pseudoephedrine’. China na India, baadhi ya viwanda vya madawa huzalisha maelfu ya tani za ‘pseudoephedrine’ kwa ajili ya matumizi halali. Walanguzi wa kimafia (‘criminal middlemen’) hununua kihalali kiasi kikubwa cha kemikali hizi, na kuziuza baadaye kwa wazalishaji haramu wa methamfetamini huko Meksiko na sehemu zinginezo. Barani Asia kilo moja ya ‘pseudoephedrine’ huuzwa kwa Tsh. 110,210.70, lakini mashirika ya kihalifu ya kimataifa kama mamafia wa Meksiko hulipa mpaka kiasi cha Tsh. 16,000,000 kwa hiyo kilo moja.

Kemikali za ‘pseudoephedrine’ hutumwa kutoka huko Asia mpaka katika maabara kubwa dunia nzima; ambako hupikwa na kutengeneza methamfetamini, na kisha kusambazwa katika maeneo yote ya nchi husika. Biashara hii uhudumia takriban watumiaji milioni 51 duniani kote.

Methi huweza kutengenezwa nyumbani. Mbolea ya amonia (‘ammonium fertilizer’) na lithi (‘lithium’), kutoka ndani ya betri za kawaida kwa mfano, huwekwa ndani ya chupa ya kawaida ya soda na kufunikwa. Kemikali zinapofanya kazi hutoa si tu methi, lakini pia fukizo (‘fumes’); lakini ambazo zina uwezo wa kulipuka.

Methi ni tofauti na kokeini kwa sababu inaunguza. Humfanya mtumiaji ajisikie raha ya kupindukia, nguvu, na makini! Mtumiaji huweza kukaa kwa masaa ishirini na nne kwa siku, anaweza kufanya kazi kwa wiki nzima, au wiki mbili, bila kupumzika.

Methi huvutwa kwa kutumia buruma (‘pipe’) inayomlewesha mtumiaji kwa haraka na vizuri zaidi. Matokeo mabaya ya baadaye ya utumiaji wa dawa hii ya ajabu ni pamoja na matatizo makubwa ya afya ya akili, na ukosefu kabisa wa hamu ya kula na kulala. Unaweza kujisikia kama vile unataka kuurarua uso wako wote! Kujikinga na dalili za namna hiyo, waathirika hulazimika kuvuta methi zaidi. Kukosa usingizi ni kubaya. Ukizidi kukaa kwa muda mrefu bila kulala, mwishowe utaugua ugonjwa unaitwa ‘matatizo ya akili ya wasiwasi’ (‘severe paranoid psychosis’).

Kama heroini, ukitumia methi utajisikia raha ya kupindukia. Kawaida, watu huanza kuvuta methi baada tu ya saa sita za usiku; utataka buruma nyingine, utataka tena kujidunga. Kisha utafanya vitu vya ajabu kama kusafisha nyumba mpaka asubuhi na kadhalika. Dozi kubwa ya methi huweza kusababisha kiharusi, maruweruwe, ugonjwa wa moyo, na kifo.

Ndani ya methi kuna kemikali yenye nguvu sana iitwayo LSD (‘Lysergic acid diethylamide’) inayohusika na maono yote ya kiwendawazimu. Maono ya kiwendawazimu (‘hallucinations’) yanayosababishwa na LSD ya methi huonekana kama taswira za kweli kabisa! Kadiri akili inavyoathirika ndivyo hata mwili unavyoathirika pia.

Dalili kubwa ya waziwazi ya methi ni ugonjwa ujulikanao kama ‘mdomo wa methi’ (au ‘meth mouth’), ambapo waathirika huonekana wakijing’ata meno yao wenyewe. Kemikali za ndani ya dawa hiyo hutafuna meno na fizi; na tezi za mate hukauka mdomoni. Zote hizi husababisha meno kuchakaa na kuoza; na mwishowe kupotea mdomoni. Waathirika wa muda mrefu hujikuta pia wakiwa waoga kupita kiasi na wagomvi, hivyo vurugu majumbani mwao kuongezeka.

Methi husababisha ubongo ufungulie vitarishi vya kikemikali viitwavyo ‘neural transmitters’ ambavyo hutufanya tunuke, tuhisi, na tuishi kulingana na mazingira fulani. Mojawapo ya vitarishi hivyo, ambavyo kimsingi huathiriwa na methi, ni ‘dopamine’. ‘Dopamine’ hujulikana kama kitarishi cha furaha. Madawa mengi ya kulevya huamsha mtiririko wa ‘dopamine’ kwenye ubongo, lakini methi hufurisha ubongo kwa kiasi cha hadi asilimia 1200 cha ‘dopamine’, kuliko ilivyo kawaida. Kuna mafuriko makubwa ya ‘dopamine’ yanayofanya mtu ajisikie raha kubwa ya kupindukia; na ambayo pia humfanya mtumiaji ajisikie kama mtu hodari wa kupindukia.

Lakini sehemu zote za ubongo zinazopokea meseji hizi (‘dopamine receptors’) uharibiwa na sumu iliyomo ndani ya methi. Mtu akiendelea kutumia methi kwa muda mrefu, hivi vyumba (‘receptors’) husimama kufanya kazi. Waathirika wa methi huweza kuwa na ‘dopamine receptors’ chache (kwa hadi asilimia 16) kulinganisha na ubongo wa kawaida wa mtu asiyetumia madawa.

Waathirika wa methi hawana uwezo wa kujidhibiti wenyewe. Wanaweza kukosa mchocheo (au ‘impulse’) wa kuiba, kwa mfano. Yaani wanaweza kuona kuiba ni jambo la kawaida, si kosa la kumpeleka mtu jela. Hupatiwa huduma ya saikolojia ya kimatibabu kwa ajili ya matumizi mabaya ya madawa ya kulevya – mchanganyiko wa maandiko mbalimbali ya kujisomea, vipindi vya matibabu vya kimakundi, na ushauri nasaha kwa kila mmojawao. Hawafanyi kazi, hawachangii chochote katika chumi za nchi zao. Methi huathiri moja kwa moja kituo kikuu cha furaha cha ndani ya vichwa vyao.

Methi ni dawa inayotumiwa (‘abused’) vibaya kuliko yote duniani. Ni dawa hatari kutengeneza, na ni dawa hatari kutumia. Methi hujulikana katika vyombo vya dola kama tatizo namba moja la madawa ya kulevya duniani; kwa sababu huwafanya watu washindwe kabisa kujizuia.

Vidonge vya mafua na aleji vina ‘pseudoephedrine’ ndani yake. Wafamasia hudai kuwa asilimia 80 ya mauzo yote ya ‘pseudoephedrine’ huenda kwenye uzalishaji wa methi. Vidonge vya Tsh. 8,000 huweza kuzalisha methi ya Tsh. 80,000. Kila gramu ina thamani ya Tsh. 162,000, ambayo ni kubwa kuliko kokeini au heroini.

Kuvuta heroini kwa kutumia karatasi ya aluminiamu au balbu au kiko cha kioo au kwenye kijiko, huitwa ‘chasing the dragon’. Kuvuta methamfetamini huitwa ‘chasing the white dragon’. Usimfukuze nyoka, hutampata.

No comments:

Post a Comment

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...