Wednesday, 23 November 2016

Wewe ni Bahari Ndani ya Tone

Kila mtu kabla ya kuzaliwa alipewa na Mwenyezi Mungu unabii na nyota ya ufalme. Una bahari ya fursa ya kuwa kitu chochote unachotaka kuwa katika dunia hii. Kama unataka furaha, furaha iko ndani yako. Kama unataka utajiri, utajiri uko ndani yako. Kama unataka amani, amani iko ndaniyako. Kama wewe ni tone na fursa ni bahari, wewe ni bahari ndani ya tone.

Unabii ni uwezo alionao mtu wa kuongea mambo matakatifu ya Mungu, kuwaongoza wenzake katika njia njema. Mungu humwambia nabii kitu cha kusema na nabii huwambia wenzake kile ambacho Mungu amemwambia aseme. Mungu hawezi kuongea na watu mpaka watu wajue jinsi ya kuongea naye, na wakati mwingine ni rahisi sana kusikia ujumbe kutoka kwa mtu kuliko kuusikia ujumbe huo moja kwa moja kutoka kwa Mungu. Mungu anaweza kukwambia useme kitu fulani kwa mtu au watu fulani. Unaweza usijue kwa nini anakwambia ufanye hivyo, lakini utajisikia msukumo wa hali ya juu wa kutangaza ujumbe uliopewa kuuwasilisha. Mungu hatakulazimisha, lakini atakung’ang’aniza, na ni Mungu pekee anayejua lengo la mawasiliano hayo. Mungu akikwambia ufanye kitu fanya mara moja, usiulize kwa nini. Kazi yako ni kufanya unachotakiwa kufanya, kusema unachotakiwa kusema, si kuuliza maswali. Mtumie rafiki yako wa kiroho kukuongoza katika mema na mabaya, na usitambe – kwamba unaongea maneno uliyoambiwa na Mungu uyaongee. Ukiwa na uwezo mkubwa wa kuongea na Mungu utaleta mabadiliko katika dunia.

Mungu humwambia mtu kitu cha kusema na mtu huwambia wenzake kile ambacho Mungu amemwambia aseme. Lakini utajuaje kama Mungu amekuchagua wewe kusema au kufanya kitu? Mungu atakwambia kupitia Roho Mtakatifu, na utajisikia msukumo mkubwa wa kusema au kufanya kile ambacho Mungu anataka useme au ufanye. Unabii unaweza kumtokea mtu yoyote, mahali popote, anayejua jinsi ya kuwasiliana na Mungu.

Nyota ni kipaji, kipawa, takdiri, karama, au uweza; ni kiashiria cha rohoni kinachoonyesha mtu atakuwa nani baadaye, mafanikio ya mtu, au takdiri ya maisha ya mwanadamu. Unabii na nyota ya ufalme ni kibali cha Mungu katika maisha ya mtu. Kupata kibali hicho, tembea na watu sahihi katika maisha yako (tembea na watu ambao Mungu amekuchagulia kushika funguo za takdiri ya maisha yako). Tamka na kukiri kibali cha Mungu katika maisha yako yote. Panda mbegu za kibali cha Mungu katika udongo wa maisha yako. Jifunze kutenda mema bila malipo, kwani wema ni mbegu ya kibali cha Mungu. Jali mambo ya ufalme wa Mungu.

Wengine hatuishi kama wafalme kwa sababu ya nguvu za giza – zilizopo kati ya Mungu na wanadamu. Nyota zetu zimefunikwa. Una kila kitu unachotafuta, ndani ya moyo wako. Usitafute furaha, utajiri au amani nje ya moyo wako. Tafuta furaha, utajiri au amani ndani ya moyo wako.

3 comments:

  1. Kila mtu ana karama yake mwenyewe itokayo kwa Mungu.

    ReplyDelete
  2. Una kifurushi cha fursa ndani ya moyo wako, kitakachokuwezesha kuishi maisha yoyote utakayoyataka katika dunia hii.

    ReplyDelete
  3. Tayari Mungu ameshakufadhili. Tafuta kibali chake uishi kama anavyotaka. Kibali cha Mungu ndiyo mtaji wa maisha yako.

    ReplyDelete

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...