Monday, 28 November 2016

Kinywaji Kikali cha Asili Chenye Ladha ya Viungo na Mitishamba cha Skandinavia

Kinywaji kikali cha asili chenye ladha ya viungo na mitishamba cha Skandinavia, ‘Aquavit’ au ‘Akvavit’, kilichotumika katika kitabu cha Kolonia Santita kuwaburudisha Vijana wa Tume nyumbani kwa Frederik Mogens, Hellerup, Copenhagen.

Aquavit ni sehemu muhimu sana ya utamaduni wa unywaji wa pombe katika nchi za Skandinavia. Skandinavia aquavit aghalabu hunyweka katika mikusanyiko ya tafrija au sherehe za sikukuu, kama vile harusi na Krismasi. Nchini Swideni, Denmaki na Ujerumani aquavit hupozwa baada ya kupikwa; na hunyweka taratibu kwa kutumia glasi ndogo za mvinyo au vilevi vikali. Hii ni kwa sababu ya mila na desturi za Skandinavia. Nchini Norwe ambako aquavit huchujwa kitaalamu na kuhifadhiwa kwa muda mrefu katika madumu ya miti, kinywaji hicho hutunzwa katika joto la kawaida na hutengwa katika glasi ndogo za vinywaji vikali kwa ajili ya watu kuburudika. Bila ubishi wowote aquavit hutumika kama mbadala wa bia, lakini mara nyingi matumizi yake hutanguliwa na funda la bia. Wengine hunywa bia baada ya funda la aquavit lakini wataalamu hupingana na mazoea hayo, kwa sababu bia itaharibu ladha na utamu wake.

Aquavit, kama ilivyo vodka, huchujwa kitaalamu kutoka kwenye nafaka au viazi. Baada ya mchujo aquavit hupewa ladha ya mitishamba, viungo, au mafuta ya matunda. Ladha inayotumika zaidi hata hivyo katika kutengenezea aquavit ni kisibiti, iliki, bizari, shamari, na limau au ganda la chungwa. Kiwanda cha vinywaji vikali cha Aalborg, Denmaki, hutengeneza aquavit iliyochujwa kwa utomvu wa visukuku vya miti ya kaharabu.

Mapishi na ladha ya aquavit hutofautiana kati ya rajamu na rajamu, lakini kwa kawaida ladha ya kisibiti ndiyo ladha yenye nguvu zaidi. Kwa kawaida, aquavit ina rangi ya manjano. Lakini pia inaweza kubadilika kati ya angavu na kahawia nyepesi; kutokana na muda kiasi gani imehifadhiwa, katika makasiki ya mwaloni, au kiasi cha rangi kilichotumika katika uchakataji wake.

Vijana wa Tume walipofika nyumbani kwa Mogens huko Hellerup kandokando mwa Copenhagen, Radia alipewa kahawa na aquavit wakati wenzake wakinywa ‘Sabor Grants’ na vinywaji vingine vikali. Radia hanywi pombe, wala havuti sigara. Wala havuti bangi. Lakini alikunywa aquavit (kiasi kidogo) kwa sababu ya kuwaridhisha wenzake. Walipomaliza mazungumzo Hellerup Vijana wa Tume walielekea Frederiksberg, manispaa ndani ya manispaa ya Copenhagen, kubomoa kambi ya Kolonia Santita.

No comments:

Post a Comment

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...