Tuesday, 25 October 2016

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sheremetyevo

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sheremetyevo II wa Moscow nchini Urusi – John Murphy alipogunduliwa kwa mara ya kwanza na magaidi wa Kolonia Santita akiwa njiani kuelekea Smolenskaya Prospekt, Ofisi ya Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya jijini Moscow, karibu na ubalozi wa Tanzania.

John Murphy akiwa na hakika ya kutokutambulika kwa majambazi wa Kolonia Santita, na hakika ya kutokutambulika kabla ya wenzake watatu (Radia, Mogens na Yehuda), alipotokeza tu majilio (‘arrivals’) majambazi wanne wa CS-Moscow walimwona na kuanza kumfuatilia kwa kificho mpaka nje ambapo Murphy alichukua teksi ya Mbulgaria ya njano. Murphy hakuwa na hakika kama wale majambazi walikuwa wakimtaka yeye. Lakini teksi yake iliposimama Teatralny Proezd, upande wa kusini wa Hoteli ya Metropol, karibu na mojawapo ya minara ya mwanzo ya Kitey-gorod (kitovu kikuu cha biashara cha Moscow ya kale), Murphy alipata hakika kama ni yeye aliyekuwa akifuatiliwa. Magaidi waliendelea mbele (mbele ya mahali teksi ya Murphy iliposimama) na kusimama mkabala na Jumba la Maonyesho ya Tamthilia la Bolshoi, halafu wawili kati yao wakashuka na kuingia ndani ya kioski, huku wawili wakibaki ndani ya gari (Bentley) na kuchunga kila kitu alichokifanya Murphy nje ya Hoteli ya Metropol. Dakika chache baadaye, sasa akitembea kuelekea Smolenskaya Prospekt, Ofisi ya Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya Nchini Urusi (WODEC Moscow), Murphy alitekwa nyara na kupelekwa Yugo Zapadnaya; katika ‘dacha’ (nyumba) ya Kolonia Santita.

CS-Moscow – Tawi la Kolonia Santita nchini Urusi na nchi za Ulaya ya Mashariki kama vile Belarusi, Moldova na Ukraini; na baadhi ya nchi za Ulaya ya Kusini kama vile Masedonia, Montenegro, Uturuki na Ugiriki, linaloongozwa na mwanajeshi wa zamani wa ‘Red Army’ Dmitri Olegushka – ni miongoni mwa magenge hatari ya kimafia nchini Urusi.

1 comment:

  1. Hapo ndipo John Murphy (mpelelezi wa Tume ya Dunia kutoka Tanzania) alipotekwa nyara akielekea katika ofisi ya Tume ya Dunia ya jijini Moscow; ambapo alitarajia kupumzika kwa masaa manne, kabla ya kuendelea na safari yake.

    ReplyDelete

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...