Monday 11 June 2018

Mungu ni Mkamilifu Milele

281. Mungu ni mkamilifu milele. Anaishi katika ukamilifu wa milele. Hivyo, kabla ya uumbaji, aliishi katika ukamilifu, baada ya uumbaji, ataishi katika ukamilifu.

Ukiichunguza sana hii kauli utajua Mungu ni nani. Mungu ni Muumbaji, aliyekuwepo, aliyepo, na atakayekuwepo.

Hapa duniani kuna watu wawili tu: Mungu na wewe! Wengine wote, vingine vyote, wako au viko kisogoni mwako. Nje ya macho yako kuna Nuru. Nuru hiyo ndiye Mungu. Wengine wote, vingine vyote, ni akisi ya taswira ambazo ziko ndani yako; ambazo unatakiwa kuziona nje ili uone umekosea sehemu gani, na uweze kurekebisha dunia yako ya ndani.

Wale wanasiasa wanaotwambia kila siku kuwa tulete mabadiliko duniani wanajisumbua iwapo hawatatwambia tulete mabadiliko ndani ya dunia zetu za ndani kwanza. Ukibadilisha dunia yako ya ndani, utabadilisha dunia yako ya nje.

Yesu ni Mfalme wa wafalme, kwa sababu baada ya muda fulani atarudisha ufalme kwa Baba yake. Mungu ni Mfalme wa milele asiyeweza kuonekana wala asiyeweza kufa, 1 Timotheo 1:17, na haonekani kwa faida yetu wenyewe.

Kwa nini? Kama Mungu yupo, yuko wapi? Kwa nini asijionyeshe ili nasi tumwone? Kama alituumba, kwa nini hatuonani naye uso kwa uso? Kwani tatizo ni nini? Faida ya yeye kutojionyesha kwetu ni nini?

Mungu hawezi kujionyesha kwetu kwa kuwa asili yetu ya ubinafsi itasababisha mtafaruku na matatizo makubwa dunia nzima. Kila mtu duniani kote atamng’ang’ania, atamtamani sana, na hakuna la maana litakalofanyika. Itakuwa kinyume na kusudi la maisha; na kusudi la maisha ni kuishi naye mbinguni kwa furaha ya milele, na hatutaweza kuishi naye mbinguni iwapo tuliishi naye duniani.

Hewa ipo lakini hatuwezi kuiona wala kuigusa. Hali kadhalika, Mungu yupo lakini hatuwezi kumwona wala kumgusa. Matendo yake makuu kwetu ndiyo yanayofanya tuamini kuwa yupo. Mungu akijionyesha kwetu tutakuwa kama watumwa. Tutakwama ndani ya asili yetu, na hatutaweza kamwe kuwa na upendo.

Mungu aliyeumba mbingu na nchi anaitwa Yehova na anaishi mbinguni juu ya nchi yote (Zaburi 83:18). Mungu anaishi juu zaidi ya sayari zote za ulimwengu wa roho, mahali ambapo muda wa duniani haufanyi kazi, katika kiti chake cha enzi kilichoijaza mbingu nzima.

Mbingu ni mbingu za Bwana, Bali nchi amewapa wanadamu (Zaburi 115:16). Kwa hiyo, sisi tunakaa duniani lakini Mungu anakaa mbinguni ambako ndiko nyumbani kwake.

Kaleb na Yoshua walihitimu madaraja 40 ya ufahamu kufika Kanaani. Kumfikia Mungu unahitaji madaraja 125 ya ufahamu.

Mungu anasema katika Isaya 66:1, “Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuwekea miguu yangu; mtanijengea nyumba ya namna gani? Na mahali pangu pa kupumzikia ni mahali gani?” Anasema tena katika Matendo ya Mitume 7:49-50, “Mbingu ni kiti changu cha enzi, Na nchi ni pa kuwekea miguu yangu; Ni nyumba gani mtakayonijengea? Asema Bwana, Au ni mahali gani nitakapostarehe?”

Kulingana na mafungu hayo Mungu ni mkubwa wa kupindukia. Kiwiliwili chake kiko mbinguni, miguu yake iko duniani.

Lakini Mungu ni nani hasa? Mungu ni Roho (Yohana 4:24) anayeishi katika ukamilifu wa milele, akiwa peke yake katika mbingu ya kwake mwenyewe, huku malaika na viumbe wengine wote wakiwa chini yake.

Kabla ya uumbaji Yehova alikuwa peke yake mbinguni akiishi katika ukamilifu wa milele. Lakini hilo halikumpendeza hata akaamua kuwa na msaidizi kwa ajili ya kazi maalumu ya uumbaji wa malaika na wa ulimwengu mzima. Mzaliwa wa kwanza wa Yehova (Wakolosai 1:15) anaitwa Yesu Kristo; ambaye Mungu alimuumba kwa mfano wako, ili asaidiane naye kumuumba binadamu kwa mfano wao.

Yesu Kristo anaitwa Mwana wa Pekee kwa sababu hiyo, kwa sababu ya kuwa mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote, na anaitwa Neno kwa sababu yeye ndiye Msemaji Mkuu wa Mungu.

Hivyo, Yohana 1:1 inaposema, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu” inamaanisha kuwa Neno ni Yesu Kristo. Yesu Kristo ndiye aliyekuwako hapo mwanzo (kumbuka Mungu hana mwanzo wala mwisho) naye Yesu alikuwako kwa Mungu naye Yesu alikuwa Mungu.

Yesu ni Mungu kwa sababu yeye ndiye mtendaji mkuu wa Mungu (Mithali 8:30). Yeye ndiye aliyemsaidia Yehova katika kazi yote ya uumbaji. Yesu ndiye aliyeumba malaika kwa niaba ya Yehova, na ndiye aliyeumba mbingu na nchi na wanadamu kwa niaba ya Yehova. Kwa sababu hiyo Yesu akapewa sifa ya uungu, naye akawa Mungu kwa sababu hiyo. Kwa hiyo, kuna Mungu na kuna Yehova.

Yehova ni Mungu kwa sababu ana uwezo wa kuumba. Yesu ni Mungu kwa sababu amepewa uwezo wa kuumba na Yehova.

Ndiyo maana sijawahi kusikia Biblia ikimtaja Yesu kama Yehova. Inamtaja Yesu kama Mungu. Kwa sababu Yesu hawezi kuwa Yehova. Hivyo, wale wanaosema Yesu si Mungu wako sahihi ikiwa wanamaanisha kuwa Yesu si Yehova. Lakini kama hawamaanishi kuwa Yesu si Yehova, Yesu ni Mungu.

Mungu alivyoumba ulimwengu miaka bilioni 14 iliyopita kwa mujibu wa sayansi ya roho ya Kiyahudi, sayansi ya uminyaji, jambo la ajabu sana lilitokea. Mungu ni mkamilifu wa milele na anaishi katika ukamilifu wa milele. Kutokana na umilele huo Mungu alitengeneza mwisho. Aliuminya umilele kwa nguvu kubwa ya ajabu, umilele ukagawanyika na kutengeneza mwanzo na mwisho, katika tukio linalojulikana kisayansi kama Big Bang, na kitendo hicho kikamficha Mungu hadi leo hii.

Ni jukumu letu kama wanadamu kumtafuta Mungu popote pale alipo, kupitia ushirikiano wa myoyo yetu, ili tutengeneze nguvu inaitwa Arvut, itakayoitengeneza na kuirejesha upya roho ya Adamu, itakayotuwezesha kumwona Mungu na kuishi naye milele hata milele.

Ukimjua Mungu utapata Arvut. Kutokana na Arvut kila hitaji lako litajibiwa kwa kadiri utakavyoomba. Arvut maana yake ni upendo.

Usikazie macho madhehebu, kazia macho Maandiko.

No comments:

Post a Comment

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...