Historia kwa ufupi ya Kolonia Santita haikuandikwa mpaka zaidi ya
miaka thelathini iliyopita katika Jimbo la Oaxaca nchini Meksiko.
Desemba 1980 (miaka mitano na mwezi mmoja baada ya kuanzishwa kwa Tume
ya Dunia) El Tigre na viongozi 13, wa mashirika 7 ya madawa ya kulevya
ya Americas (Amerika ya Kusini na Kaskazini), waliungana katika Mkutano
wa Oaxaca na kuunda La Familia (Familia) – kwa lengo la kujiimarisha
kibiashara (ndani ya Americas) na kupanua wigo wa biashara yao mpaka nje
ya Hemisifia ya Magharibi.
Kutawala biashara ya madawa ya
dunia, La Familia ikabadilika na kuwa La Federación (Shirikisho)
iliyosambaa kutoka Meksiko mpaka Australia mpaka India mpaka Afrika ya
Kusini – na kuwa na nguvu kuliko Medellín ya Pablo Escobar, na Cali ya
Gilberto Orejuela, na mashirika mengine mengi ya kipindi hicho katika
Amerika ya Kusini na Kaskazini.
Chini ya utawala wa El Tigre
kama kiongozi mkuu msaidizi, La Federación ikafungua matawi makubwa saba
dunia nzima – Saldanha, Paris, Mumbai, Moscow, Miami, Bissau na
Copenhagen – kwa ajili ya ugaidi, wa kimadawa (‘narcoterrorism’), na
usambazaji wa madawa duniani kote kwa niaba ya Federación.
Oktoba 1983, hata hivyo, Tume ya Dunia ilipoanza rasmi kumtafuta El
Tigre na baadhi ya makamanda wake, La Federación ilisambaratika. Jeshi
la Anga la Meksiko (FAM) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (PGR)
vilimuua Kiongozi Mkuu wa Federación (Carlos Pulecio Alcántara) na
kuwafunga makamanda wawili wa juu wa muungano wa shirika hilo katika
gereza la Mexico City, Reclusorio Preventivo Oriente, alikowahi kufungwa
El Tigre na kutoroka katika miaka ya sabini – hivyo kuathiri (kwa kiasi
kikubwa) uongozi na biashara ya Federación, hasa ya kokeini (na
heroini) duniani kote.
Kurudisha imani ya wateja (na
kutambulisha eksitasi na ‘hielo‘ katika soko la dunia la Federación – na
kujipanga upya) La Federación ikabadilika na kuwa jina la sasa la La
Colonia Santita Cartel (CS-14), Shirika la Madawa ya Kulevya la Kolonia
Santita (KS-14), Septemba 1985 katika Mkutano wa Kolombia.
El
Tigre na wenzake wanne: Ignacio Leonardo de la Fuente, Raymundo Escoto
Martinez, José Alberto Araújo na Panceano Nieto (viongozi waanzilishi wa
La Familia; waliokuwa wakitafutwa na Tume ya Dunia na Jeshi la Meksiko
sawa na El Tigre na Alcántara) hawakuhudhuria Mkutano wa Kolombia. ‘Jefe
de Jefes’ (Bosi wa Mabosi) El Tigre, na wenzake wanne walikuwa mbali
kabisa; ng’ambo ya pili ya Pasifiki, wakicheza ‘mariachi’ (muziki wa
asili) na ‘campesinos’ (wakulima) katika milima ya Sierra Madre
Occidental huko Sinaloa – na kulala na wanawake warembo, wenye bikini,
wanaokunywa martini, Acapulco nchini Meksiko.
Watu
wanaohatarisha maisha yao kwa kudharau sheria wakati mwingine hawatakiwi
kudharauliwa. Ni sawa na mtu aliyepoteza kila kitu katika maisha yake.
Wana uwezo wa kufanya chochote. Serikali ya Meksiko ilipokataa kukidhi
matakwa ya El Tigre ya kubadili katiba ya nchi – kuondoa kipengele cha
mkataba wa kubadilishana watuhumiwa na washtakiwa – ili akikamatwa
asipelekwe Marekani ambako atafungwa na kufia gerezani, El Tigre
aliilaani Serikali ya Meksiko.
Kujibu mapigo, ya laana ya
maluuni, Serikali ya Meksiko ikawakabidhi makamanda 7 wa Kolonia Santita
kwa mamlaka za Marekani, na kuongeza juhudi za kumsaka El Tigre mpaka
nje ya Amerika ya Kusini na Kaskazini.
El Tigre, kuikomoa
serikali na kuwalipia kisasi makamanda wote waliouwawa na kufungwa na
shirikisho, akamuua Mwanasheria Mkuu wa Serikali (PGR) na maafisa 7 wa
Jeshi la Polisi la Nchi (PJF) kulinganisha idadi ya makamanda wake
waliopelekwa Marekani – halafu ‘akapotea’, kabisa; baada ya kutangaza
vita na Serikali ya Meksiko.
Tume ya Dunia imekuwa ikimtafuta
Chui wa Siberia kwa zaidi ya miaka tisa. Bila mafanikio. Ulinzi wa
Panthera Tigrisi ni wa kimataifa. Mbali na kulindwa na wananchi wa
Oaxaca (kwa sababu ya kuwajengea shule, hospitali, makanisa, misikiti na
kadhalika), na polisi wa shirikisho (kwa sababu ya vitisho, mauaji na
rushwa); El Tigre analindwa na jeshi binafsi la kujihami (‘autodefensa’)
la wanajeshi wastaafu zaidi ya 1300.
Mbali hali kadhalika na
autodefensa; kiongozi wa Kolonia Santita ana walinzi binafsi makomandoo
(48) akiwemo A. Narochnitskaya Belinsky, mtaalamu wa kutengeneza
nyambizi wa Urusi, na Nicolas Kahima Kankiriho (‘Kahima the Warrior’)
mwanajeshi wa kulipwa wa Uganda – aliyetoroka na El Tigre katika
nyambizi ya Jefe de Jefes SPD (‘the Silent Predator of the Deep’),
iliyotengenezwa na Belinsky, katika Ghuba ya Meksiko Septemba 16, 1986.
Kolonia Santita (KS-14) ni genge hatari kuliko yote la madawa ya
kulevya katika eneo lote la Hemisifia ya Magharibi. Lilianzishwa mwaka
1980 kwa kuunganisha magenge saba ya madawa ya kulevya ya Amerika,
Meksiko na Kolombia, na magenge mengine madogomadogo zaidi ya tisini ya
Amerika ya Kusini na Kaskazini.
Genge hili kubwa, pengine kuliko
yote duniani, lilianzishwa na watu kumi na nne kwa lengo la
kujiimarisha kibiashara ndani na nje ya Hemisifia ya Magharibi (na
kupanua wigo wa biashara yao kimataifa – kuanzia Hemisifia ya Magharibi
mpaka ya Mashariki, Kusini na Kaskazini).
Magenge hayo ni Baja
California, Matamolos, Guanajuato (Meksiko), The Benson Brothers of
Chicago, The Family (Marekani) na Cartagena na Diablos de Amazonas au
Mashetani wa Amazoni (Kolombia).
Benson Bennett Stansfield (‘El
Tigre’) wa Marekani, Gortari Manuel (‘El Padrino’) wa Meksiko na Eduardo
Chapa de Christopher (‘El Chupacabra’) wa Kolombia ndiyo wakurugenzi
waanzilishi wa KS-14.
Wengine ni Ignacio Leonardo de la Fuente,
Marciano Moreno Herrera – Hana uhusiano na mchumba wa Debbie, Giovanni
Gonzalez Murillo, Herrera Monteagudo, Panceano Nieto, Raymundo Escoto
Martinez (kutoka Meksiko), José Alberto Araújo, Victor Miguel Enrique,
Javier Ricardo Antonio, Carlos Pulecio Alcántara, Roberto Mosquera
Portocarrero (kutoka Kolombia) na Freeman Boyd Figueroa kutoka Amerika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Roho Yako
289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...
-
Mercury Cougar ya John Murphy aliyonunua mwaka 1990 kwa gharama kubwa huko Michigan nchini Marekani. Gari hilo lililorekebishwa kwa ajili ...
-
Siku ya kuzaliwa ni siku ya kwanza ya safari nyingine ya siku 365, saa 5, dakika 48, sekunde 46 na maili milioni 600 kulizunguka jua. Safi...
-
KITENDAWILI CHA KOLONIA SANTITA Shilingi milioni moja za Kitanzania kushindaniwa ndani ya miezi sita kuanzia leo Swali: Kila namba ...
No comments:
Post a Comment