Kuna mambo yanatokea hapa ulimwenguni ambayo yanafanya nikiri uwepo wa Mungu kwa asilimia kubwa. Wanasayansi wanasema ulimwengu ulianzishwa na mlipuko wa ‘Big Bang’, uliotokea takribani miaka bilioni 14 iliyopita, kutoka katika kitu kidogo zaidi kuliko ncha ya sindano, lakini hawatuambii nini kilisababisha mlipuko huo utokee au hicho kitu kidogo kuliko ncha ya sindano kilitoka au kilikuwa wapi.
Wanaendelea kusema kuwa baada ya ‘Big Bang’ kutakuwepo na ‘Big Crunch’, ambapo ulimwengu utarudia hali yake ya awali ya udogo kuliko ncha ya sindano, na kila kitu kinachoonekana leo ulimwenguni hakitaonekana tena.
Hapo sasa ndipo utata unapokuja. Mlipuko wa ‘Big Bang’ ulipotokea ulimwengu ulilipuka na kusambaa pande zote nne za ulimwengu kwa mwendokasi wa zaidi ya kilometa milioni 2 kwa saa, mpaka hivi leo unavyoonekana na bado unaendelea kusambaa. Kutokana na dhana ya ‘Big Crunch’, wanasayansi wanaamini ulimwengu utapanuka ila baadaye utapungua mwendo na utarudi mwanzo kabisa mahali ulipolipukia.
Lakini mwaka 1995 wanasayansi hao hao waligundua kitu. Ulimwengu – badala ya kupungua mwendo wa kupanuka kama wanasayansi walivyokuwa wakitabiri – sasa unaongeza mwendo, tena kwa mwendokasi ambao haujawahi kutokea.
Hiki ni nini kinachosababisha ulimwengu uongeze mwendokasi kiasi hicho badala ya kuupunguza? Hicho ni nini ambacho ulimwengu unapanukia? Wanasayansi hawana jibu. Wanasingizia kitu kinaitwa ‘dark matter’, maada ambayo haijawahi kuonekana, kwamba ndicho kinachosababisha ulimwengu uongeze mwendokasi kwa kiwango hicho ambacho hakijawahi kutokea; na hicho ambacho ulimwengu unapanukia wanahisi ulimwengu wetu unapanukia katika ulimwengu mwingine, kwa mujibu wa dhana nyingine kabisa iitwayo ‘multiverse’ au ‘meta-universe’.
Kuna kitu kinaitwa ‘Higgs boson’ – chembe ndogo inayosemekana kuhusika na uzito (‘mass’) wa chembe ndogo 16 zilizomo ndani ya atomu, kasoro chembe ya mwanga, iliyopotea mara tu baada ya mlipuko wa ulimwengu wa ‘Big Bang’ miaka bilioni 13.7 iliyopita katika kipindi kilichoitwa ‘epoch’ – ambayo ilianza kutafutwa katika maabara za CERN, Uswisi, toka mwaka 1964, maabara ambazo kazi yake kubwa ni kutengeneza mazingira ya mwanzo kabisa ya mlipuko wa ‘Big Bang’, kusudi wanasayansi waone kama wanaweza kubahatisha kuiona na kuidhibiti hiyo bosoni.
Bosoni itakapopatikana wanasayansi watajua siri ya ‘dark matter’, watajua jinsi ulimwengu unavyofanya kazi na jinsi ulivyoumbwa na jibu la kitendawili cha ‘Standard Model’ litapatikana.
Hiyo ni kazi ngumu. Ndiyo maana ‘Higgs boson’ mwaka 1993 iliitwa ‘The God Particle’. Yaani, wanasayansi wanahisi kuna muujiza wa Kimungu na huenda wasiipate kabisa hiyo bosoni. Wanasema waliipata mwaka 2013. Lakini hiyo waliyoipata bado ina utata.
Kutokana na kushindwa huko kwa sayansi na historia, kutokana na kushindwa kwa sayansi kutengeneza binadamu au mnyama, kutokana na miujiza iliyorekodiwa katika vitabu vitakatifu; naamini, Mungu yupo.
Wanasayansi wana uwezo wa kupeleleza hadi kipindi cha karne ya kwanza ambapo Yesu aliishi, alikufa, alifufuka na alipaa kwenda mbinguni, na wana uwezo wa kujua mambo mengi kwa hakika yaliyofanyika katika kipindi hicho na hata katika kipindi cha kabla ya hapo.
Kuna miujiza ambayo Yesu aliifanya ambayo haiko ndani ya Biblia. Kwa mfano, Biblia inasema Yesu alizaliwa ndani ya zizi la ng’ombe wakati sayansi inasema alizaliwa nje ya zizi la ng’ombe; na muujiza wa kwanza kuufanya ambao hauko ndani ya Biblia ni kutembea mara tu baada ya kuzaliwa, na watu na ndege wa angani kuganda kabla ya kuzaliwa Masihi na kabla ya wakunga kufika kumsaidia Maria Magdalena kujifungua.
Akiwa na umri wa miaka sita, sayansi inasema, Yesu alikuwa akicheza na mtoto mwenzake juu ya paa la nyumba ya jirani na mara Yesu akamsukuma mwenzake kutoka juu hadi chini na mwenzake huyo akafariki papo hapo. Watu walipomsonga sana Yesu kwa kumtuhumu kuwa yeye ndiye aliyesababisha kifo cha mwenzake, na kwamba wangemfungulia mashtaka, Yesu alikataa katakata kuhusika na kifo hicho.
Lakini walipozidi kumsonga, aliusogelea mwili wa rafiki yake kisha akamwita na kumwambia asimame. Yule mtoto alisimama! Huo ukawa muujiza mkubwa wa kwanza wa Yesu Kristo, kufufua mtu nje ya maandiko matakatifu.
Kuna mifano mingi inayodhihirisha uwepo wa Mungu ambayo wanasayansi hawawezi hata kuipatia majibu. Tukio la Yoshua kusimamisha jua limewashangaza wanasayansi hadi nyakati za leo. Mwanzoni mwa miaka ya 70 wanasayansi walijaribu kurudisha muda nyuma kwa kompyuta kuona kama kweli wangekuta takribani siku moja imepotea kama ilivyorekodiwa katika Biblia.
Cha kushangaza, cha kushangaza mno, walikuta saa 23 na dakika 20 zimepotea katika mazingira ambayo hawakuweza na hawataweza kuyaelewa. Walipochunguza vizuri walikuta ni kipindi cha miaka ya 1500 KK (Jumanne tarehe 22 Julai) ambacho ndicho tukio la Yoshua la kusimamisha jua na kusogeza mwezi nyuma digrii 10, ambazo ni sawa na mzunguko wa dakika 40, lilipotokea.
Kwa kutumia elimu ya wendo, elimu ya kupanga miaka na matukio ya Kibiblia, dunia iliumbwa Jumapili tarehe 22 Septemba mwaka 4000 KK. Hata hivyo, mahesabu ya kalenda yanaonyesha kuwa Septemba 22 ilikuwa Jumatatu (si Jumapili) na kwamba kosa hilo labda lilisababishwa na siku ya Yoshua iliyopotea.
Hayo yote ni kwa mujibu wa Profesa C. A. Totten, wa Chuo Kikuu cha Yale, katika kitabu chake cha ‘Joshua’s Long Day and the Dial of Ahaz: A Scientific Vindication and a Midnight Cry’ kilichochapishwa mwaka 1890.
Kama hakuna Mungu iliwezekanaje Yoshua aombe jua lisimame na jua likasimama kweli? Iliwezekanaje Yesu aseme atakufa, atafufuka na atapaa kwenda mbinguni na kweli ikatokea kama alivyosema? Ndani ya Biblia kuna tabiri 333 zilizotabiri maisha yote ya Yesu Kristo hapa duniani na zote zilitimia – bila kupungua hata moja. Utasemaje hapo hakuna Mungu? Mungu yupo, naamini, sijui.
Tukio la Yesu kufa, kufufuka na kupaa kwenda mbinguni si la vitabu vitakatifu pekee, hata sayansi inakubaliana na hilo.
Bado sayansi haijanishawishi kuamini inavyotaka niamini.
ReplyDelete