Yesu alipokuwa msalabani watu wengi walimzunguka. Askari wa Kirumi aliyekuwa na chongo, na mkuki, alikuwa na jukumu la kumtesa Yesu hadi kufa kwa amri ya Pilato. Yesu alipolia kwa sauti kuu, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?”, yule askari alikurupuka na kumwendea Yesu. Lakini Yesu alishakata roho. Kuthibitisha kama Yesu alishakata roho, askari alimchoma Yesu mkuki kwenye mbavu kwa nguvu zake zote. Mkuki huo ukamtoboa Yesu hadi upande wa pili, ukatoboa hata moyo wake. Askari alipochomoa mkuki, damu na maji viliruka na kupiga jicho lake bovu. Papo hapo askari akapona na kuona vizuri. Alipoona kweli amepona na kuona vizuri, askari alipiga kelele, alipiga magoti na kuomba Mungu amsamehe dhambi zake.
Msamaha una nguvu kuliko dhambi. Askari huyo atakwenda mbinguni. Haijalishi umechukia watu kiasi gani. Haijalishi umetesa watu kiasi gani. Haijalishi umeua watu kiasi gani. Haijalishi umetenda dhambi kiasi gani. Mungu anachotaka kutoka kwako, tubu.
Damu na maji vilitoka katika mbavu za Yesu Kristo kutokana na upungufu wa damu mwilini, hipovolimia, kulikotokana na kuchapwa bakora. Yesu alichapwa bakora arobaini kabla ya kupelekwa Golgotha. Matokeo ya hipovolimia katika mwili wa mtu ni moyo kwenda mbio kusukuma damu iliyopungua, kuzimia kutokana na msukumo wa damu kuwa chini, figo kushindwa kufanya kazi na kiu ya maji.
Kuna ushahidi wa kutosha katika maandiko kwamba Yesu aliugua hipovolimia kutokana na kuchapwa. Yesu alipobeba msalaba wake kuelekea Golgotha alianguka, na mtu mmoja aliyeitwa Simoni alilazimishwa ama kuubeba au kumsaidia Yesu kuubeba msalaba huo hadi kilimani. Kuanguka huko kunaonyesha kwamba Yesu alikuwa na shinikizo la damu. Alama nyingine inayoonyesha kwamba Yesu alipatwa na ugonjwa wa hipovolimia ni pale alipodai kuwa alikuwa na kiu, akiwa msalabani, akimaanisha kiu ya maji.
Kabla ya kukata roho mapigo ya kasi ya moyo aliyoyapata Yesu kutokana na mshtuko wa hipovolimia, pia yalisababisha maji kujikusanya katika vifuko vya maji au ute kandokando ya moyo na kandokando ya mapafu. Mkusanyiko huu wa maji kandokando ya moyo hujulikana kama ‘pericardial effusion’ na mkusanyiko wa maji kandokando ya mapafu hujulikana kama ‘pleural effusion’. Hii ndiyo maana baada ya Yesu kukata roho, na askari wa Kirumi kurusha mkuki katika ubavu wake, baada ya kutoboa mapafu na moyo, damu na maji vilitoka katika mbavu za Yesu kama Yohana alivyorekodi katika injili yake. Mapafu ya Yesu na tumbo la Yesu vilijaa damu na maji. Mkuki ulivyotupwa maji yalitoka katika mapafu ya Yesu na katika tumbo la Yesu; na katika utando unaozunguka moyo wa Yesu, kutokana na kupasuka kwa moyo.
Lakini damu na maji vina maana kubwa katika maisha yetu. Biblia inaeleza kuwa wakati Yesu Kristo akiwa msalabani alichomwa ubavu wake kwa mkuki, ikatoka damu na maji. Hapo ndipo zilipozaliwa sakramenti za kanisa.
Aidha, tukio la askari wa Kirumi kumchoma Yesu na damu na maji kutoka lina maana nyingine kubwa katika maisha yetu. Hapo ndipo Ukristo ulipozaliwa; na ni kwa sababu hiyo mwanamke anapojifungua hutoa damu na maji kutokana na kupasuka kwa utando wa mfuko wa uzazi. Kutokana na hayo, Wakristo wanapoabudu msalaba wanaeleza umuhimu wa matukio na mafundisho waliyopata kupitia mateso aliyopata kiongozi wao na kuwa, msalaba ni chombo cha ukombozi.
Askari wa Kirumi alimchoma Yesu mkuki ili andiko litimie. Askari huyo ambaye Biblia haikumtaja jina kwa sababu zilizoko nje ya uwezo wetu, alivyoona kweli amepona na ameona alishuhudia, na ushuhuda wake ulitoka moyoni, ili nasi tupate kusadiki. Wauaji wa Kirumi walipoona kwamba wale wezi waliosulubiwa pamoja na Yesu walikuwa bado hawajakata roho, waliwavunja miguu ili washindwe kupumua na hivyo kuharakisha kifo chao. Kwa upande wa Yesu, waliona alishapoteza fahamu na labda alishafariki. Kuthibitisha hilo askari wa Kirumi alirusha mkuki, nao ukatoboa utando unaozunguka moyo wa Yesu na mapafu ya Yesu, na damu na maji kutoka.
Lakini yote hayo yalishatabiriwa miaka mingi kabla ya Yesu: “Hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa” na “Nao watamtazama yeye ambaye walimchoma”.
Mungu anachotaka kutoka kwako ni kuzitambua dhambi zako na kuziungama. Yesu alikuwa dhambi kwa ajili yetu. Alikubali kulaumiwa badala ya sisi kulaumiwa. Omba maghufira kwa Mungu kwa makosa uliyofanya.
Kilio kikuu cha Yesu, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?”, yaani, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”, na “Imekwisha”, vilitabiriwa katika Zaburi 22 ili watu waliompinga Kristo waamini kama Yesu alikuwa Masihi. Zaburi 22 ulikuwa wimbo maarufu katika kipindi cha karne ya kwanza, kipindi ambacho Yesu alizaliwa na kufa, uliotungwa na mfalme Daudi, ulioitwa ‘Zaburi ya Mateso na Matumaini ya Mwadilifu’. Kwa hiyo Yesu aliposema maneno hayo yaliwaingia watu akilini, na kuanzia hapo imani hasa ya Ukristo ikachukua kasi hadi leo hii.
Zaburi 22 inaanza na “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” na inaisha na “Imekwisha”, miongoni mwa maneno saba aliyoyasema Yesu pale msalabani Golgotha. Kwa hiyo, Zaburi 22 ni utabiri wa kifo cha Yesu.
Kuna sababu za msingi na za kinabii za damu na maji vilivyotoka katika mbavu za Yesu Kristo msalabani. Ubavu wake uliochomwa na mkuki ulithibitisha kifo chake cha kibinadamu, huku vingine vyote vikitimiza unabii wake uliotajwa na Yohana.
Maji yalimaanisha ubatizo, damu ilimaanisha mwisho na mwanzo wa Injili ya Yesu.
Habari hiyo inapatikana katika mafungu yafuatayo: Yohana 19:17 (Msalaba), Yohana 19:28-29 (Kiu), Yohana 19:30 (Imekwisha), Yohana 19:34 (Damu na Maji), Mathayo: 27:32-33, Marko 15:21-22, Luka 23:26 (Simoni), Marko 1:9-10 (Ubatizo), Waebrania 9:14, (Kifo), Yohana 19:36-37, Kutoka 12:46, Hesabu 9:12, Zekaria 12:10 (Unabii), 1 Wakorintho 11:23-26 (Sakramenti za Kanisa), Mathayo 27:46 na Zaburi 22:1 (Kilio). Soma pia kitabu cha unabii cha ‘Tumaini la Vizazi Vyote’ cha Ellen G. White (Askari wa Kirumi).
Maji yanayotoka kwa mwanamke maana yake ni kwamba mtoto atakayezaliwa ameshabatizwa. Na damu inayotoka inamaanisha kwamba mtoto atayezaliwa atahubiri Injili ya Yesu Kristo maisha yake yote. Kwani maji yanamaanisha ubatizo. Damu inamaanisha Injili ya Yesu Kristo.
No comments:
Post a Comment