Sunday, 15 January 2017

Mpelelezi wa Tume ya Dunia Kutoka Tanzania John Murphy


John Murphy (mtoto wa mwanajeshi – kwani baba yake Gideon Ambilikile alikuwa luteni kamanda wa JWTZ, na babu yake Ambilikile Makojo alikuwa koplo wa KAR katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia) ni mwanajeshi bora kuliko wote Tanzania.

Kama Radia Hosni alivyo kwa Tunisia, John Murphy ni miongoni mwa mashujaa adimu waliowahi kukanyaga ardhi ya Tanzania. Akiwa bado kijana, wa miaka 32, John Murphy ni mpelelezi maarufu duniani – kuliko wote katika bara la Afrika – kachero wa kwanza katika historia ya Tume ya Dunia kukamilisha operesheni ya STKJ peke yake (STKJ ni Shabaha ya Tume ya Kiwango cha Juu) bila msaada wowote, na mshindi wa Tuzo ya Shujaa wa Taifa la Tanzania.

Kwa sababu za kiusalama, akiwa nje ya Bodi ya Makamishna ya Tume ya Dunia (WBC) na WODEC-Intelligence, John Murphy hujulikana kama John Ambilikile kukwepa shari na mashabiki hususan wanawake; wanaoweza kuleta misukosuko kuonana ana kwa ana na shujaa wa maisha yao. Mashabiki wachache mno wamebahatika kumtambua; huku wengine, kuanzia Tanzania mpaka sehemu za mbali kama Australia na India, wakibahatika tu kumsikia katika vyombo mbalimbali vya habari.

John Ambilikile alizaliwa tarehe 6/11/1960 Jumapili saa saba usiku, Dar es Salaam, Tanganyika – wazazi wake walipohamia huko kwa shughuli mbalimbali za kikazi kutokea Arusha, kaskazini mwa Tanganyika, walikokuwa wakiishi.

Akiwa na umri wa miaka kumi John alianza kuonyesha kipaji katika sanaa ya mapigano. Wengi walitabiri angefuata nyayo za baba yake, Luteni Kamanda Gideon Ambilikile, aliyekuwa mchezaji mzuri wa miereka katika miaka ya nyuma. John aliweza kucheza sarakasi na kung’fu vizuri bila hata ya kufundishwa na mtu.

Luteni Kamanda Ambilikile alivyogundua kipaji cha mwanaye, alimwandikisha haraka katika Chuo cha Kung’fu na Sarakasi cha Kinondoni, Kinondoni, mjini Dar es Salaam. John alikuwa mwanachuo kwa miaka minane mfululizo akihudhuria mafunzo kila jioni baada ya kutoka shule bila kukosa.

Alipotimiza umri wa miaka kumi na saba na nusu, John Ambilikile alianza kuwa tishio; hasa kwa wanafunzi wenzake na watu wengine wa kawaida. Sasa alikuwa na uwezo mkubwa, wa kupambana na watu (sita mpaka nane waliokuwa na visu vikali), aliokuwa akiwaharibu sura ndani ya dakika mbili tu.

Siku moja, John alihudhuria sherehe ya ndugu yake katika ukumbi fulani huko Kariakoo, Dar es Salaam. Sherehe hiyo ilikuwa kubwa na watu walikuwa wengi. Lakini, baada ya saa moja hivi tangu shughuli zianze, majambazi watano walivamia ukumbi na kusababisha fujo ya hali ya juu.

Majambazi wale, waliokuwa na visu na mapanga na miti, walifanya vurugu nyingi – kitendo kilichosababisha watu waogope na kulala chini, kufuatia amri kali ya kufanya hivyo. Hata hivyo, John hakutii amri. Hawakuwa na silaha yoyote ya kumtisha. Kitendo hicho kikawaudhi majambazi lakini John akakataa kuwa kondoo.

Bila kupoteza muda, John Ambilikile alivuta pumzi. Alipoishusha, watu walishangaa (zaidi ya mia nne, ambao tayari walishaanza kuinuka na kutafuta njia za kusambaa) aliporudisha punje za matumaini yao kwa umahiri na ufundi wa hali ya juu. Alikwepa visu, mapanga na miti, huku nukta ileile akitoa mapigo makali – na dakika chache akawa amewashinda wote. Bila yeye kuwa na jeraha hata moja katika mwili wake.

Watu waliushangilia ushujaa wa John Ambilikile kila kona ya jiji la Dar es Salaam. Ambilikile akawa maarufu kuanzia kipindi hicho na kuendelea; na kujawa na mashabiki, hasa watoto na baadhi ya wanawake.

Serikali ya Tanzania, kupitia Jeshi la Wananchi (JWTZ), ambako baadaye Ambilikile alijiunga kufuata nyayo za baba yake, ilikihitaji sana kipaji cha John Ambilikile kwa ajili usalama (wa nchi na watu wake). Kwa niaba ya nchi na kwa niaba ya JWTZ, serikali ilimkaribisha Ambilikile katika usaili wa Idara ya Usalama wa Taifa na hatimaye mwaka 1980 – akiwa na miaka ishirini – akawa rasmi mtumishi wa serikali.

Akiwa Usalama wa Taifa, Ambilikile alifanya kazi kwa bidii na utiifu wa hali ya juu. “Usalama wa Taifa ni akili si ukali. Kazi yake, au wajibu wake; ni kukusanya, kuchanganua, kudurusu na kuunganisha kwa makini, taarifa nyeti za kijasusi za ndani na nje ya nchi kuilinda Tanzania na watu wake. Ukitaka kuwa na akili kuwa kawaida. Ukitaka kuwa na nguvu kuwa mkarimu. Ukitaka kuwa tajiri kuwa tajiri wa unyenyekevu.” Falsafa ya John Ambilikile alipojiunga na Usalama wa Taifa Desemba 1980.

Akiwa jeshini John Ambilikile hakutaka mchezo hali kadhalika, na kwa sababu ya falsafa zake aliheshimu watu wote lakini alikuwa jasiri. Mbali na mafunzo ya kazi hakuacha kung’fu, mchezo anaoupenda kuliko yote. Kila alipofanya mazoezi alijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake WOTE, mpaka akawaogopesha (na hata kuwafurahisha) mabosi wake na hata baba yake mzazi.

Sifa ya bidii, nidhamu na heshima kwa wote ilimsaidia John kupata msaada wa masomo. Akiwa meja, mwaka 1984, baada ya kuhitimu digrii yake ya biashara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, John alipata nafasi ya kusafiri. Alikwenda China, Japani na Israeli (kwa mafunzo ya upelelezi, kung’fu, judo na tikwandu).

Katika jimbo la Henban huko China, John alikokuwa akichukua kozi ya dani ya pili ya mkanda mweusi wa kung’fu, meja aliwaacha hoi Wachina. Alicheza kung’fu na sarakasi, vizuri zaidi, kuliko viongozi wao. Aliweza kuzunguka, hewani, mara tatu au nne bila kugusa chini – na alikuwa akipigana kama Bruce Lee.

Chuo cha Ambilikile cha Mount Songshan siku moja kilipata mwaliko huko New Jersey nchini Marekani, ambako walikwenda kwa mashindano ya kirafiki na vyuo vya kung’fu na kareti vya Amerika.

Siku ya John kucheza, aidha, meja aliwashangaza Waamerika kwa staili zake walizoziita za kishamba, hasa alipopambana fainali na bingwa wa kareti wa kipindi hicho katika New Jersey nzima David Brookshield. Katika mpambano huo Brookshield alimsumbua kidogo Ambilikile. Lakini haikuchukua muda. John alipagawa, na kukunja mwili wake katika staili moja ya kichina halafu; bila kupoteza muda akatoa pigo, fupi, zito; Brookshield akaumia vibaya! Ngumi ya Ambilikile ilitua barabara katika kichwa cha Brookshield na kuleta madhara makubwa. Sehemu moja ya kichwa, cha Brookshield, ilibonyea kabisa!

Kimya cha hofu kilichotawala kiliwasisimua sana mashabiki. Walipovamia ulingo, kushuhudia kisichofikirika, walitoka pale wakiwa na hakika ya asilimia 100; kwamba John alikuwa na nyundo (au chuma chochote) katika mfuko wake wa bukta – aliyoitoa (harakaharaka), wakidhani ni mtindo wa kipigo, na kumpondea mwenzake kichwani!

Ile haikuwa nyundo. Wala haukuwa uchawi. Ilikuwa ngumi, imara, ya uzito wa kilo 90, uzito wote wa John Ambilikile – na Amerika wakaanza kumjua kwa hilo.

Aliporejea kutoka Amerika, miaka miwili baada ya tukio la Brookshield, alikokuwa amekwenda kwa mafunzo ya kikomandoo kwa msaada wa kikosi cha Navy SEALs cha Marekani, John hakukaa sana nyumbani. Alikaribishwa ‘China’, Cowloon Tong, Hongkong; katika Chuo cha Cowloon Bay International Martial Arts (CIM) cha Barabara ya Kai Chueng, alipokabidhiwa nishani ya heshima (kwa ajili ya mchango wake katika sanaa ya mapigano) na dani ya nne ya mkanda mweusi wa mchezo wa kung’fu.

Huyo ndiyo John Murphy Ambilikile, mpelelezi hatari na maarufu duniani wa Dar es Salaam, Tanzania. Baba yake, Gideon Butimba Ambilikile, 58, alikuwa kanali kamanda wa jeshi la wanamaji la Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ); na mama yake, Penina Ambilikile, 55, alikuwa mwalimu wa Chuo cha Ualimu cha Kinondoni. Murphy ana wadogo zake wawili: Jemima, 28, ameolewa. Ana mtoto mmoja wa kiume – Prometheous A. Joanna, 26, alikuwa mwanafunzi (wa digrii ya uzamili) katika Chuo Kikuu cha California – California Institute of Technology, Caltech Pasadena – Pasadena nchini Marekani. Kipindi hicho, kipindi Murphy alipopokea wito wa Copenhagen, Joanna alikuwa Dar es Salaam kusherehekea siku yake ya kuzaliwa na marafiki zake wawili wa Los Angeles, California.

Murphy ana mpenzi anaitwa Sophia Dickson Kaswiga, wa miaka mitatu. Ana miaka 28, mzuri, mwembamba na mwenye umbo zuri la kupendeza. Murphy ni mrefu na maji ya kunde, Sophia ni mfupi na mweupe.

Hata hivyo, familia yake yote, kasoro baba yake, wanamjua kama John Ambilikile – mfanyabiashara maarufu, ‘Makun’gfuu’, anayependelea judo, kung’fu na kareti. Hawamjui kama John Murphy – mpelelezi hatari duniani.

Pichani ni gari la John Murphy aina ya BMW 850i alilonunua nchini Ujerumani mwaka 1992. Gari hilo ndicho kitu cha kwanza kilichomshtua kachero wa Kolonia Santita Giovanna Garcia, kabla hajaonana na John Murphy uso kwa uso katika ofisi za Kanda ya Afrika ya Kusini ya Tume ya Dunia, Mtaa wa Samora, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...