Kuna
 hadithi nyingi maarufu ambazo zimekuwa zikisimuliwa katika vitabu vingi
 huko Okinawa na Japani kuhusiana na ‘nunchaku’ (nanchaku – Kamusi ya 
Enock Maregesi), kwamba nanchaku hapo mwanzo ilikuwa mipini ya kuvunia 
mpunga (au puta), iliyobadilishwa na wakulima wa Kijapani kuwa silaha 
hatari dhidi ya askari wa tabaka la watawala wa kijeshi wa samurai! 
Hadithi hizi, hata hivyo, si za kweli katika nyanja zote nne: Nanchaku 
haijawahi kuwa silaha ya Kijapani, wala haijawahi kutumika kama puta ya 
kuvunia mpunga. Haikutengenezwa na wanavijiji, wala haikuwahi kutumika 
dhidi ya askari wa samurai. 
Nanchaku,
 kama tunavyoijua leo, inatoka katika Kisiwa cha Okinawa huko Uchina … 
ambayo leo ni sehemu ya Japani. Okinawa ipo takriban katikati ya Taiwani
 na Japani bara, na ni kisiwa kikubwa kuliko vyote katika mkusanyiko wa 
visiwa vya Ryukyu (au ‘kamba’), mlolongo wa maili 650 wa visiwa 
vidogovidogo kati ya Japani Kusini na Taiwani. 
Okinawa
 ni sehemu ya Japani, lakini Waokinawa si Wajapani, na wanayo lugha na 
utamaduni wao, ijapokuwa siku hizi lugha yao imemezwa sana na lugha ya 
Kijapani. Hata hivyo, cha kushangaza ni kwamba, lugha ya Kijapani haina 
hata neno moja la nanchaku! Mtu akihitaji kuandika neno ‘nanchaku’ kwa 
lugha ya Kijapani, anaweza kufanya hivyo kwa njia mbili: Anaweza kutumia
 mfumo wa alfabeti wa silabi na matamshi wa ‘katakana’ – unaotumika 
katika lugha ya Kijapani kuandika maneno ya kigeni na maneno ya mtaani, 
au maneno ya kihuni – kuandika silabi za neno ‘na-n-cha-ku’. Au, 
vinginevyo, anaweza kutumia herufi za Kichina za maneno ya ‘double part 
baton’ (au virungu viwili); ambayo hutamkwa ‘shuang jie gun’ kwa 
Kichina, ‘nanchaku’ kwa Kiswahili, ‘nun cha kun’ kwa Kiokinawa na ‘so 
setsu kon’ kwa Kijapani. 
Watu
 wengi hudhani kwamba nanchaku ilianza kama puta ya kuvunia mpunga 
(‘utzu’) katika kipindi cha ukabaila, lakini haya ni makosa. Kupata 
jibu, hebu fikiria ya kuwa unataka kutumia nanchaku kuvuna mpunga ambao 
mimea yake umeilaza chini ardhini. Ili kipande cha mkono wa nanchaku 
kinachoning’inia kitue vizuri kwenye ardhi, lazima utatakiwa kuinama kwa
 kiasi cha kichwa chako kuwa karibu na magoti yako (au utatakiwa kupiga 
magoti kwenye ardhi). Kwa staili ya kwanza, kila mara utakapoinama na 
kuinuka utaweza kupata maumivu ya mgongo; wakati staili ya pili 
haitakuwa nzuri sana, maana mtu yeyote aliyewahi kufanya hivyo anaweza 
kukwambia madhara yake ni yapi. 
Puta
 halisi ya Kiokinawa, kama ilivyo puta ya Kiulaya, ina mpini mrefu sawa 
na urefu wa kawaida wa mwanamume ili kazi ya uvunaji iwe rahisi. Hivyo, 
imani ya kwamba nanchaku inatokana na puta ya Kiokinawa ya kuvunia 
mpunga ni imani isiyo na msingi hata kidogo. Sababu nyingine ya makosa 
haya, licha ya mfanano wa waziwazi wa puta za kuvunia mpunga na virungu 
vya kupigania vya nanchaku, inaweza kuwa uwepo wa magongo ya kupigania 
(‘uchibo’); ambayo kiukweli ni puta zilizorekebishwa za kuvunia mpunga –
 miongoni mwa silaha nyingi kadha wa kadha za sanaa ya mapigano za 
Okinawa ziitwazo ‘kobujutsu’. 
Bado
 ipo mifano zaidi ya imani kali juu ya sampuli kifani (‘prototype’) ya 
nanchaku. Hata hivyo, imani sadikifu kuliko zote (iliyothibitishwa na 
baadhi ya wataalamu wa silaha za Kijapani za ‘kobudo’, au magongo ya 
kupigania) ni kwamba nanchaku inatokana na hatamu za farasi ziitwazo 
‘muge’. Mwanzoni kabisa, mikono ya hatamu ilikuwa imejipinda. Lakini 
baadaye ilirekebishwa na kuwa silaha iliyonyooka kama inavyojulikana 
leo. 
Aidha,
 zipo imani zingine za historia ya nanchaku zisemazo kwamba hapo mwanzo 
nanchaku zilikuwa njuga za walinzi wa usiku au zana za kukatia mimea ya 
ndizi (barawaji bora zaidi katika visiwa vya Okinawa hutoka katika gamba
 la mgomba). Mwishowe, imani nyingine ya mwisho – inayoungwa mkono na 
wataalamu kama vile wataalamu wa Miyagi na Ikeda wa Japani na Okinawa – 
inasema kuwa nanchaku iliigwa kutoka katika silaha moja ya Kichina 
iliyopelekwa Okinawa na wahamiaji wa Kichina. Ushahidi usiokuwa wa moja 
kwa moja (dhahiri) wa imani hii ni ukweli kwamba, neno linalotumika kwa 
ajili ya neno ‘nanchaku’ limenakiliwa kutoka katika lugha ya Kichina. 
Historia
 kwa ufupi ya nanchaku na Okinawa haikuanza mpaka mwanzoni mwa karne ya 
kumi na tano. Mnamo mwaka 1429, Mfalme Sho Hashi alianzisha himaya ya 
Sho kwa kuunganisha falme tatu za wana mfalme wa Okinawa: Hokuzan, 
Nanzan na Chuzan, na hivyo kutengeneza ufalme wa Ryukyu, huku jiji la 
Shuri likiwa ndiyo mji mkuu wa ufalme. Sho Hashi sasa alikuwa na eneo 
lililokuwa na muungano wa tawala kadha wa kadha; lakini si nchi moja. 
Kila mwana mfalme aliishi katika kasri lake na alitawala himaya ya kwake
 mwenyewe; alikuwa na jeshi la kwake mwenyewe, alikuwa na sheria za 
kwake mwenyewe za kodi, na alikuwa na mfumo wa kwake mwenyewe wa sheria 
na mahakama. Mchakato wa kuunganisha hizi falme kuwa nchi moja 
iliyoungana ulimalizika baada ya takriban miaka 50 iliyofuata, chini ya 
mmoja wa warithi wa Mfalme Sho Hashi – Mfalme Sho Shin – aliyegeuza 
ufalme kuwa nchi moja yenye serikali moja, jeshi moja na mfumo mmoja wa 
sheria, kama zilivyo nchi nyingi za leo. 
Kupunguza
 uwezekano wa uasi nchini Okinawa, Sho Shin aliwakusanya wana wote wa 
mfalme (‘aji’) katika mji wa Shuri na kupiga marufuku umilikaji wa 
silaha. Ni jeshi la mfalme pekee pamoja na malodi walioruhusiwa kumiliki
 silaha, lakini ni mfalme pekee aliyeruhusiwa kumiliki silaha nyingi kwa
 wakati mmoja. Matokeo yake, jeshi la mfalme likawa jeshi pekee nchini 
Okinawa. 
Miaka
 180 baadaye – baada ya Mfalme Sho Hashi kuanzisha himaya ya Sho – 
ufalme wa Ryukyu ambao, mpaka kipindi hicho, ulikuwa bado ni nchi moja 
huru, ulichukuliwa na dola ya mwana mfalme wa Satzuma wa Japani; na kuwa
 chini ya miliki ya tawala hiyo mpaka mwaka 1879 ambapo, baada ya 
mapinduzi ya Meiji, Okinawa ilichukuliwa na Japani. Hata hivyo, katika 
kipindi chote cha kati ya mwaka 1609 na 1879, uwepo wa Japani nchini 
Okinawa ulikuwa mdogo! Kulikuwepo na dazani chache tu za askari wa 
samurai nchi nzima, na wengi wao waliishi katika jiji la Shuri. Serikali
 ya Japani ilikubaliana na amri ya Sho Shin dhidi ya silaha, na 
ikaongeza kwa kupiga marufuku uingizaji na umilikaji wa silaha nchini 
Okinawa hali kadhalika. Hata hivyo, hadithi kuhusu udhibiti hasa wa 
silaha katika kisiwa cha Okinawa zimebakia kuwa hadithi tu. Watu maarufu
 wa Okinawa bado waliruhusiwa kumiliki na kubeba mapanga yao, na 
wanafamilia ya kifalme na wanawafalme walikuwa hata wakiruhusiwa kuwa na
 bunduki za marisau kwa ajili ya kuwindia. 
Katika
 vitabu vingi vya kareti, mara nyingi imekuwa ikiandikwa kuwa wakulima 
ndiyo waliyoanzisha sanaa ya mapigano ya Okinawa. Lakini hii haileti 
maana yoyote. Okinawa haikuwahi kuwa nchi tajiri na halafu, baada ya 
kuanzishwa kwa mfumo wa ajira wa Kijapani katika karne ya 17, Okinawa 
ilizidi kuwa maskini. Wakulima walilazimika kufanya kazi kuanzia macheo 
mpaka machweo kwa ajili ya chakula cha familia zao wenyewe. Wanavijiji 
hawakuwa na muda au hamasa ya kujifunza kupigana na kuendeleza sanaa ya 
mapigano iliyokuwa bora zaidi. 
Watu
 maarufu na wenye uwezo ndiyo waliyoanzisha sanaa ya mapigano ya 
Okinawa. Tabaka la makabaila (‘kazoku’) lilijifunza sanaa ya kupigana, 
sanasana kama kitu cha kupoteza muda. Lakini kwa tabaka la malodi 
wafanyakazi (‘shizoku’) maarifa juu ya sanaa ya mapigano kilikuwa kitu 
cha lazima; kwa vile waliifanyia kazi serikali kama maafisa wa jeshi na 
polisi, wakusanyaji wa kodi na kadhalika. Tukiangalia nasaba ya mtindo 
wowote wa kareti au ‘kobujutsu’ wa Okinawa, tunaona kuwa waanzilishi wa 
mitindo hiyo ni vitawishina vya familia ya kilodi, au walijifunza sanaa 
ya mapigano kutoka kwa lodi. 
Lakini,
 kama kweli sanaa ya mapigano ya Okinawa ilianzishwa na malodi 
walioruhusiwa kuwa na mikuki na mapanga, kwa nini basi walianzisha mbinu
 za kupigania miundu, makasia, majembe na vifaa vingine vya wavuvi na 
wakulima? 
Tabaka
 la malodi wafanyakazi wa Okinawa (kama unavyoweza kutabiri kutokana na 
jina lenyewe) waliifanyia kazi serikali kama maafisa wa jeshi na polisi,
 au maafisa wa serikali. Waliitunza na kuilinda katiba ya nchi yao, na 
walipata mishahara yao kutoka kwa mfalme. Hawakuwa na vyanzo vingine vya
 mapato. Sheria iliwabana kufanya kazi za ziada. Hata hivyo, ilifikia 
kipindi hiyo mishahara waliyokuwa wanapata ikawa haiwatimizii mahitaji 
yao ya lazima, matokeo yake wengi wao wakageukia wizi na ujambazi 
uliokubuhu. Mnamo mwaka 1724 (ili kutatua tatizo hili) wafanyakazi wa 
serikali wakapewa fursa ya kuwa wafanyabiashara, wahunzi na wakulima. 
Wengi wao waliacha kazi serikalini na walihitaji kuhamia vijijini na 
familia zao, ili tu waweze kujilisha wenyewe. Baada ya karne moja na 
nusu, kabla ya mapinduzi ya Meiji, fursa za wafanyakazi wa serikali ya 
Okinawa pamoja na askari wa samurai wa Japani zilisitishwa (ikiwa ni 
pamoja na haki ya kumiliki mapanga) na walinyimwa hata mishahara yao. 
Ukikisoma vizuri kitabu cha ‘Gone With the Wind’ cha Margaret Mitchell 
wa Marekani, utakumbuka kisa cha makabaila wa jana waliolazimika kuwa 
wafanyabiashara wa maduka na waoka mikate ili waweze kuishi. 
Vivyo
 hivyo ilitokea hata kwa makabaila wa Okinawa. Wanafamilia ya kifalme 
walifanya kazi kama wasaisi, watu wanaofanya kazi za kuchunga au 
kuangalia wanyama wanaopandwa kama vile farasi au punda, na walinzi wa 
usiku. Wana wafalme walikuwa wakataji wa miti na wauzaji wa nguruwe 
kwenye masoko. Wafanyakazi wengi wa serikalini walihamia vijijini. 
Wakulima, bila shaka, wakawa na kinyongo kukutana na majirani wao wapya 
na kujaribu hata kuwafukuza katika ardhi ya vijiji vyao. Juhudi hizi 
mara nyingi zilipelekea makundi haya mawili ya watu kupigana. Idadi ya 
wezi na majambazi kadhalika iliongezeka katika nchi, ambapo chakula 
kilikuwa ni kitu cha thamani. Matokeo yake, ‘wana-wafalme-wakulima’ 
walilazimika kufufua ujuzi au weledi wao wa kupigana. 
Tabaka
 la malodi wafanyakazi wa serikali bila ya shaka, wangependelea kupigana
 kwa mapanga (au majambia) badala ya kupigana kwa mikono mitupu. Lakini 
hawakuruhusiwa kuwa na silaha. Hata hivyo, askari hufanya nini 
anaposhindwa kutumia silaha? Huchukua chochote kinakachokuwa karibu 
yake. Watawa wa Shaolin walivumbua mbinu za kupigana kwa ndala na 
vikapu, huku maninja wa Japani wakijifunza kuua wapinzani wao kwa vijiti
 vya kulia chakula. Tabaka la malodi wafanyakazi wa Okinawa, wakiwa 
hawaruhusiwi kumiliki silaha, hali kadhalika walivumbua silaha kutokana 
na kitu chochote walichoweza kupata. 
Fimbo
 na vitu mbalimbali vyenye marefu tofauti (‘rokushakubo’ yenye urefu wa 
futi sita, ‘jo’ futi nne, ‘hanbo’ futi tatu, nk.) siku zote zilitumika 
kama silaha za ziada, hivyo zilitumika kwanza. Miundu (‘kama’), makasia 
(‘eku’), majembe (‘kuwa’), ndoana (‘nunt-bo’), mawe ya kusagia (‘tonfa’)
 na vifaa vingine vilivyoonekana kuwa vizuri zaidi katika ugomvi 
kadhalika havikusahaulika. Fimbo mbili zilizounganishwa kwa kamba 
zilivutia macho ya mtu fulani. Shujaa mmoja alizizungusha, halafu 
akapata picha kichwani mwake yule shujaa akimpiga adui kichwani – na 
nanchaku ikazaliwa. 
Nanchaku
 haikuwa silaha maarufu miongoni mwa silaha zingine huko Japani na 
Okinawa. Tumelihitimisha hili kwa sababu hakuna mtindo wowote wa 
kienyeji wa nanchaku unaojulikana leo. Kinyume chake, leo tunajua ‘kata’
 (staili) nyingi za kale za silaha za kienyeji. Pengine ukosefu wa 
umaarufu wa nanchaku ulitokana na uwezo wake mdogo wa kufanya kazi pale 
ilipolinganishwa na silaha zingine za kienyeji ukiachilia mbali upanga. 
Kwa upande mwingine, mtu aliyekuwa na utaalamu wa matumizi ya nanchaku 
alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwashinda wapinzani wachache waliokuwa na 
visu au waliokuwa hawana silaha yoyote. Aidha, nanchaku ilikuwa rahisi 
kufichika. Watu walikuwa wakitembea nayo kila siku. Hivyo, huko Okinawa,
 zaidi nanchaku ilikuwa ikitumika kama silaha ya mtaani ya kujilindia 
dhidi ya watu wakorofi na majambazi. 
Silaha
 kama nanchaku zinapatikana katika mifumo ya sanaa nyingi za mapigano 
duniani kote. Mifano michache ya silaha bora zinazofanana na nanchaku ni
 kama vile ‘erjiegun’ ya Kichina, ‘tabak-toyok’ ya Filipino, 
‘ssangjulbong’ ya Korea, na puta za kupigania za bara la Ulaya. Silaha 
(zote) hizi zinatengenezwa kama nanchaku. Baadhi yazo ni nanchaku 
zilizotengenezwa kutokana na silaha za asili za Japani na Okinawa 
ziitwazo ‘kobudo’. ‘Chako’ ya Filipino na ‘tabak-toyok’ kwa mfano, 
hazina tofauti yoyote na nanchaku za Okinawa; zilizotengenezwa kutokana 
na mbao au miti ya Filipino. Hata hivyo, sanaa zingine za mapigano zina 
aina zake zenyewe za ‘silaha za minyororo’, kama ‘sanjiegun’ ya Shaolin 
au mipini ya kupigania ya bara la Ulaya… 
Lakini
 leo nanchaku ni maarufu sana – kiasi kwamba karibu kila aina mpya ya 
sanaa ya mapigano hutumia nanchaku katika programu zake za mazoezi. 
Kutokana na urahisi wa upatikanaji wa malighafi na urahisi wake wa 
kutengeneza, uwezo wake mkubwa wa upiganaji wa mtaani na umaarufu wake 
kuongezeka kutokana na sinema za Bruce Lee, nanchaku imezaliwa upya 
katika nyakati za leo. Nanchaku, leo, ni miongoni mwa silaha maarufu 
sana baada ya kisu na kirungu. 
Habari hii imetafsiriwa (kutoka kwa Alex Levitas) na Enock Maregesi. 

Nanchaku ilitumiwa na majambazi wa Kolonia Santita katika pori la Benson Bennett walipokuwa wakipigana na Vijana wa Tume katika chumba cha tatu cha usalama. Katika chumba hicho maadui walikuwa na ujuzi mkubwa wa karibu fani zote za mapigano, na waliruhusiwa kuwa na silaha za aina yoyote isipokuwa bunduki na bastola. Walikuwa na majambia makali na mikuki ya ‘Qiang’; walikuwa na visu vipana, magongo na minyororo ya nanchaku ya chuma ya kupigania. Hata hivyo, Vijana wa Tume walishinda! Ila kazi ikawa katika chumba cha nne na cha mwisho cha usalama, ambapo mmoja wa Vijana wa Tume aliuwawa.
ReplyDelete