Msomaji
wa kawaida wa hadithi au maandiko yoyote hajali iwapo anachokisoma
kimeandikwa kwa utaalamu au la – hakuna atakayejali iwapo kanuni za
fasihi zitavunjwa ili kupendezesha hadithi au maandiko yoyote. Wengi
wanachojali ni utamu wa hadithi wanayoisoma, si kanuni za fasihi
zilizotumika katika maandalizi ya hadithi hiyo. Lakini hayo yanaweza
kusamehewa. Kisichoweza kusamehewa ni tahajia, sarufi au matumizi ya
mazungumzo ya kawaida ya mtaani katika maandiko ya hadithi.
Hupaswi
kuandika mambo ya kihuni au utani katika hadithi itakayosomwa na watu
wengi kwani wengine hawapendi utani au uhuni hasa wale waliotoa pesa zao
kununua hadithi wakitarajia kupata la maana isipokuwa katika hadithi za
vichekesho peke yake. Hadithi za vichekesho peke yake ndiyo unaweza
kuandika chochote unachojisikia kuandika. Andika mambo ya kihuni au
utani ndani ya funga na fungua semi ionekane si wewe uliyesema bali
wahusika wako katika hadithi.
Usiangalie
tu nani atasoma hadithi yako leo, bali angalia nani atasoma hadithi
yako miaka mia moja ijayo. Na kumbuka, huwezi kumdanganya msomaji.
Usiandike kosa kwa makusudi ukidhani msomaji hatagundua. Anaweza
kugundua, na akigundua anaweza asiwe shabiki yako tena katika hadithi
zako zitakazofuata.
Kanuni
maarufu katika fasihi ni “Onesha, usiambie”. Ukisema “John alikuwa na
furaha,” unamtaarifu msomaji kwamba John alikuwa na furaha. Lakini
ukisema “John alitabasamu,” unampa msomaji akili itakayofanya ajue kama
John alikuwa na furaha. Unamwonesha, humwambii! Kanuni hii ni nzuri
katika fasihi na ndivyo mambo yalivyo katika maisha ya kila siku. Kama
John ni mfanyakazi mwenzako, hatuna mtu wa kutuambia kama John ana
furaha kwa sababu ya kupandishwa cheo au mshahara. Tunachotakiwa kufanya
ni kuchunguza vizuri tabia ya John na kujua nini kinaendelea katika
maisha yake. Kuonesha humfanya msomaji azame katika hadithi – hufanya
hadithi ionekane ya kweli – hasa mwandishi anapounganisha vyema ubunifu
na uhalisia.
Kanuni
za fasihi ndiyo msingi wa maandiko yote ya kitaalamu hapa ulimwenguni.
Watu hawana budi kuzifuata kanuni hizo iwapo wanataka kutumia vipaji
vyao katika ngazi ya kimataifa.
Mambo ya kihuni au utani ni kama vile misimu au simo (‘slang’) au lugha za mitaani, au matusi.
ReplyDelete