197. Sabato ilianzishwa na Mungu siku ya saba ya uumbaji wake. Siku
ya Sabato ni siku takatifu, iliyoko katika Amri Kumi za Mungu, ambayo
hatuna budi kuitunza na kuiheshimu. Sheria ya Siku ya Sabato haikufa
baada ya kifo cha Yesu Kristo msalabani kama Wakolosai wanavyodai.
Wakolosai walifuata falsafa za kipagani, na walizileta falsafa hizo
ndani ya mwili wa Kristo ambalo ni kanisa. ‘Usiiamini’ Wakolosai 2:17.
Iamini Wakolosai 2:20-23, ambapo Paulo anafundisha Mataifa jinsi ya
kuitunza Sabato, na 1 Wakorintho 12:27 ambayo inatoa maana halisi ya
Wakolosai 2:17. ‘Mwili wako ni wa Kristo’ ni tofauti na ‘mwili wa
Kristo’ na ni tofauti na kanisa. Ukiamini kama mwili wako ni wa Kristo
na ni kanisa, utaitunza Sabato.
Kumbukumbu la Torati 5:12-15
inasema, “Ishike siku ya Sabato uitakase, kama BWANA, Mungu wako,
alivyokuamuru. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku
ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako; siku hiyo usifanye kazi yo
yote, wewe wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi
wako, wala ng’ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako ye yote, wala
mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako na mjakazi wako
wapumzike vile vile kama wewe. Nawe utakumbuka ya kuwa wewe ulikuwa
mtumwa katika nchi ya Misri, na ya kuwa BWANA, Mungu wako, alikutoa huko
kwa mkono wenye nguvu, na mkono ulionyooshwa; kwa sababu hiyo BWANA,
Mungu wako, akikuamuru uishike Sabato.”
Tazama jinsi
tunavyoamrishwa kuitakasa Sabato. Msisitizo hapa ni katika suala la
uhuru. Mungu anasema, “Nawe utakumbuka ya kuwa ulikuwa mtumwa katika
nchi ya Misri,” Kidokezo hiki kiko wazi! Wana wa Israeli walipokuwa
watumwa, hawakuwa na uhuru hata wa kujiamulia mambo yao wenyewe. Kwa
hiyo, iwapo tutaitunza Sabato kama vile inavyotakiwa, tutakuwa huru.
Iwapo itatumika vizuri, Sabato itatushurutisha kukumbuka siku za nyuma;
sawa tu na itakavyotushurutisha kukumbusha siku za mbele, kule maisha
yetu yanapoelekea.
Tutafanya hivyo kwa kujifunza Biblia na
kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu; ujumbe ambao utatuhamasisha, pamoja
na taamuli na mazungumzo ndani ya ushirika. Katika ibada za kanisani,
tunasikia mengi juu ya Ufalme wa Mungu na juu ya dunia ya leo. Ibada
nyingi uhusisha dhambi kwa namna fulani. Dhambi ni uvunjaji wa sheria (1
Yohana 3:4), lakini Amri Kumi za Mungu ni sheria ya uhuru (Yakobo
1:25). Kwa kuzitunza amri hizo tutabaki kuwa huru dhidi ya utumwa wa
Shetani, dunia hii, na hata kifo. Katika siku ya Sabato, Mungu huelekeza
watu wake kupitia Neno lake juu ya jinsi ya kuzitunza amri zake na
hivyo kubaki huru. Kutoka 16:4, 25-30 inaeleza zaidi:
Ndipo BWANA
akamwambia Musa, “Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka
mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku sehemu ya siku;
ili nipate kuwajaribu, kwamba watakwenda katika sheria yangu, ama
sivyo.” … Kisha Musa akasema, “Haya, kuleni hiki leo; kwa kuwa leo ni
Sabato ya BWANA; leo hamtakiona nje barani. Siku sita mtaokota; lakini
siku ya saba ni Sabato, siku hiyo hakitapatikana.” Ikawa siku ya saba
wengine wakatoka kwenda kukiokota, wasikione. BWANA akamwambia Musa,
“Mtakataa kuyashika maagizo yangu na sheria yangu hata lini? Angalieni,
kwa kuwa BWANA amewapa ninyi hiyo Sabato, kwa sababu hii huwapa siku ya
sita chakula cha siku mbili; kaeni kila mtu mahali pake, mtu awaye yote
asiondoke mahali pake kwa siku ya saba.” Basi hao watu wakapumzika kwa
siku ya saba.
Amri ya kwanza kabisa ambayo Mungu aliwafunulia Wana
wa Israeli baada ya kuwakomboa kutoka utumwani ilikuwa ni ile iliyokuwa
na dhamira ya kuwaweka huru, yaani Sabato. Mungu aliwapa ushuhuda huu
wa chakula cha maajabu cha siku mbili cha mana, katika siku ya sita,
bila kuwapa chochote katika siku ya saba, kwa muda wa miaka arobaini!
Kinyume cha wale wanaodai kuwa Sabato imebatilishwa au imebadilishwa,
Sabato ni zawadi ya ajabu kutoka kwa Mungu.
Kwa karne nyingi, watu
wamejaribu kutafuta njia za kujishawishi wenyewe na kuwashawishi
wengine kwamba Wakristo hawatakiwi kutunza Sabato na siku takatifu.
Mojawapo ya mafungu wanayoyapenda zaidi katika harakati zao hizo ni
Wakolosai 2:16-17. Baadhi hufundisha ya kwamba, kundi la uasi la
Wayahudi katika kanisa la Kolosai lilikuwa likijaribu kutekeleza utii
kwa tamaduni za Kiyahudi; kama vile sheria za nyama safi na najisi na za
kutunza siku takatifu. Chini ya mazingira kama hayo, wanasema, Paulo
anawaambia Wakolosai ya kwamba hawakuwa na haja ya kuwa na wasiwasi juu
ya kile wengine walikuwa wakihukumu na kusema kuhusu wao.
Upindishwaji
wa sehemu hii ya maandiko kwa kiasi fulani huanza kwa kutokuielewa
vizuri Wakolosai 2:14, jambo ambalo wengi huthibitisha kwamba sheria
iliondolewa na kugongomewa misumari msalabani. Wanaamini kwamba Paulo
anasema katika fungu la 16, “Basi [kwa vile sheria imeondolewa], mtu
asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu
au mwandamo wa mwezi, au Sabato.” Kwa hiyo, hutafsiri mstari wa 17
kumaanisha kwamba Paulo anakanusha Sabato na siku takatifu kirahisi kama
ishara zisizo muhimu za matukio yajayo; huku wakisisitiza kuwa, haja
pekee ya kweli ya Mkristo wa kweli ni imani katika Kristo. Kutokana na
hili, wanahitimisha kwamba hatupaswi kuwa na wasiwasi kutokana na hizi
siku takatifu kwa sababu, kwa kuwa Kristo alikufa, maadhimisho yake
hayatakiwi tena.
Paulo anasema nini hasa katika mafungu haya
ambayo aghalabu hueleweka vibaya? Kuyaelewa maandiko haya vizuri lazima
kwanza tuufikirie usuli wa kiutamaduni na kihistoria wa watu ambao Paulo
alikuwa akiwaandikia. Wakolosai walikuwa wameathiriwa kwa kiasi kikubwa
na falsafa za kipagani, ambazo zilifundisha kuwa ukamilifu uliweza
kupatikana kwa njia ya kujinyima na kujiepusha na anasa. Matokeo yake,
Kolosai ikawa jumuiya ya kujiepusha na raha na anasa ambayo ilizingatia
utawala wa dini, wananchi wake wakadhani mtu yoyote aliyekuwa na dini
alipaswa kuishi kama walivyoishi wao.
Wengi wa watu waliobadilisha
imani zao na kuwa Wakristo walikuja kanisani na falsafa zao za
kipagani, na baadaye wakaanza kuwa na ushawishi mbaya juu ya Wakristo
wote wa huko Kolosai. Paulo anawasahihisha Wakristo waliokuwa wanafanya
hivyo katika Wakolosai 2:20-23:
“Basi ikiwa mlikufa pamoja na
Kristo mkayaacha yale mafundisho ya awali ya ulimwengu, kwa nini kujitia
chini ya amri, kama wenye kuishi duniani, Msishike, msionje, msiguse;
(mambo hayo yote uharibika wakati wa kutumiwa); hali mkifuata maagizo na
mafundisho ya wanadamu? Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima,
katika namna ya ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea, na
katika kuutawala mwili kwa ukali; lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tamaa
za mwili.”
Inavyoonekana, baadhi ya watu walishaanza kufikiria
kwamba kujinyima huko kwa raha na anasa waliojitwisha kungeweza kwa
kiasi fulani kuchangia kwenye wokovu wao na walishaanza kuwa na mtazamo
tofauti dhidi ya Yesu Kristo. Walikuwa na imani zaidi katika kazi zao za
kipagani. Paulo aliwaonya kuhusu hili katika Wakolosai 2:8: “Angalieni
mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa
jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya
ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo.”
Mungu alishawaita watu
katika kanisa la Kolosai waachane na tamaduni zao za kipagani, na
walishaanza kujifunza jinsi ya kufurahia maisha kwa namna ya uwiano kama
Mungu alivyokusudia. Hii ilikuwa ni pamoja na kula nyama, kunywa divai,
na kufurahia chakula na ushirika, huku wakitunza Sabato ya Mungu na
sherehe zake. Inavyoonekana watu walifurahia kukutana pamoja na
kushirikiana kwa kiasi cha hata wengine kusherehekea miezi mipya,
sikukuu ambazo Mungu hakutaka zifanyike lakini, ambazo zilishakuwa
tamaduni chini ya Agano la Kale.
Kwa vile wale Wakolosai
walioongoka walikuwa wakijifunza jinsi ya kuyafurahia maisha kama Mungu
alivyokusudia, watu nje ya kanisa walianza kuwaonea gere na kuwashutumu.
Katika kushughulikia matatizo haya, Paulo anawakumbusha Wakolosai ya
kuwa wamekamilika katika Yesu Kristo; hawana haja tena ya falsafa za
kipagani za dunia hii. “Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa
Mungu, kwa jinsi ya kimwili. Na ninyi mmetimilika katika yeye aliye
kichwa cha enzi yote na mamlaka.” Wakolosai 2:9-10.
Katika mistari
ya 11 na 14, Paulo anaonyesha jinsi Yesu Kristo alivyokufa kulipa
adhabu kwa ajili ya dhambi zetu na sasa dhambi zetu zilizopita;
zilizotokana na kufuata njia, tamaduni, na falsafa za dunia hii, zilivyo
na kasoro na zilivyogongomewa msalabani kwake. Anawakumbusha ya kuwa
Kristo ameshawashinda kabisa roho wote wabaya wanaoendelea kutawala
ulimwengu huu mbaya wa sasa, na ambao uhamasisha falsafa za kipagani
zilizokuwa zikitawala katika jamii ya Kolosai: “Akiisha kuzivua enzi na
mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika
msalaba huo.” (mstari wa 15).
Kwa maneno hayo yenye nguvu na ya
kutia moyo kama usuli, Paulo anaelekeza katika mstari wa 16 kwa nini
Wakristo wa kipindi hicho hawakupaswa kuwa na wasiwasi dhidi ya tabia ya
jamii ya Kolosai juu ya desturi zao na maisha mapya ya kanisa:
“Basi
[Kwa kuwa Yesu Kristo ni Bwana na Mwalimu wenu na ameshinda na ana
mamlaka juu ya nguvu zote za giza katika dunia hii], mtu asiwahukumu
ninyi katika vyakula, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au
sabato.”
Kwa maneno mengine, msiwe na wasiwasi juu ya nini watu
katika jamii hufikiri juu ya starehe yenu ya kula chakula kilicho bora,
kunywa divai, na kuadhimisha Sabato na siku takatifu kwa furaha. Kristo
ameishinda dunia na watawala wake wote, hivyo hatuna haja ya kuwa na
wasiwasi kuhusu nini dunia inasema kuhusu sisi.
Katika mstari wa
17, Paulo anataja kwamba Sabato na sikukuu takatifu ni ‘kivuli’ – ishara
au aina fulani ya mambo yajayo katika mpango wa Mungu. Sabato ni aina
ya Milenia ambapo Yesu Kristo na watakatifu watatawala dunia kwa miaka
elfu moja. Siku takatifu huashiria hatua mbalimbali katika mpango wa
Mungu, na hutukumbusha kila mwaka kusudi kuu la Mungu katika uumbaji wa
mwanadamu.
Maneno ya mwisho katika mstari wa 17 – “bali mwili ni
wa Kristo.” – ni tafsiri mbaya iliyotokana na kushindwa kuelewa maana
halisi ya kile ambacho Paulo alikuwa akikisema. Huo ni mfano bora wa
jinsi watafsiri wakati mwingine wanavyoitafsiri Biblia pale
wanapotafsiri Kigiriki cha awali kwenda katika lugha ya Kiingereza, na
hivyo kwenda katika lugha zingine.
Tafsiri halisi ya maneno ya
mwisho ya Wakolosai 2:17 inasema, “bali mwili wako ni wa Kristo.” Lakini
mwili wa Kristo ni nini? 1 Wakorintho 12:27 inatupatia jibu: “Basi
ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake.” Mwili
wa Kristo ni kanisa! Nukuu halisi ya Kigiriki inayofanana kabisa na
tafsiri ya “mwili wa Kristo” katika 1 Wakorintho 12:27 (‘soma Christou’)
imetumika katika Wakolosai 2:17.
Maana kamili sasa ya kile Paulo
alichokuwa akikisema inajidhihirisha wazi! Anawaambia Wakolosai kwamba
hawapaswi kuruhusu mtu yoyote kuwahukumu au kuwauliza maswali juu ya
mambo haya bali waache kanisa lifanye maamuzi hayo. Anawaelekeza wafuasi
wake kwenye mfano wa viongozi wa kiroho wa kanisa ambao walijenga
msingi na kuweka utaratibu wa kuabudu katika siku ya Sabato na katika
siku takatifu, akiwasihi wasiwe na wasiwasi kuhusu mtu yoyote katika
jamii anasema nini kuhusu wao. Ushawishi kama huo unatolewa katika
mistari ya 18 na 19:
“Mtu asiwanyang’anye thawabu yenu, kwa
kunyenyekea kwa mapenzi yake mwenyewe tu, na kuabudu malaika, akijitia
katika maono yake na kujivuna bure, kwa akili zake za kimwili; wala
hakishiki kichwa, ambacho kwa yeye mwili wote ukiruzukiwa na
kuungamanishwa kwa viungo na mishipa, hukua kwa maongeo yatokayo kwa
Mungu.”
Katika mafungu haya, Paulo kwa mara nyingine
anawatahadharisha Wakolosai kwamba hawapaswi kuruhusu shinikizo la jamii
ambamo waliishi kuwa na ushawishi wowote juu ya imani zao na tamaduni
zao na anaendelea kuwasihi walitegemee kanisa pekee kwa ajili ya chakula
chao cha kiroho na ustawi wa maisha yao.
Hivyo basi, tunaona
kwamba, mbali na kuibatilisha Sabato na siku takatifu, Wakolosai 2:16-17
ni ushahidi tosha kwamba kanisa la awali lilizitunza siku hizi na
kwamba Paulo alifundisha Mataifa jinsi ya kuzitunza.
http://www.facebook.com/koloniasantita
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Roho Yako
289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...
-
KITENDAWILI CHA KOLONIA SANTITA Shilingi milioni moja za Kitanzania kushindaniwa ndani ya miezi sita kuanzia leo Swali: Kila namba ...
-
Mpelelezi wa Tume ya Dunia kutoka Jerusalem, Israeli, Kanali Daniel ‘Yehuda Ben-Asher’ Ebenezer, Daniel Yehuda, alikuwa komandoo wa kit...

Paulo, mtumishi wa Bwana aliyefanya kazi kubwa zaidi ya Mungu kuliko mitume wote, alikuwa akiongea na Wakolosai katika ‘lugha’ waliyoielewa.
ReplyDelete‘Usiiamini’ imeandikwa kwa alama za kudondoa (‘ ’) kuonyesha kwamba Wakolosai 2:17 ni fungu lisiloeleweka vizuri, lakini si kwamba usiliamini. ‘Usiiamini’ Wakolosai 2:17 maana yake ni iamini Wakolosai 2:17 lakini kwa makini, kwani ina ujumbe uliojificha! Ujumbe huo unapatikana katika 1 Wakorintho 12:27.
ReplyDeleteSi kweli kwamba Wakolosai walikuwa hawaitunzi Sabato na siku takatifu kama vile Majilio, Epifania, Meza ya Bwana, Kwaresima, Ijumaa Kuu, Pasaka ya Kikristo, Sikukuu za Vibanda, na kadhalika. La hasha! Walikuwa wakizitunza. Utata ni kwenye tafsiri ya baadhi ya mafungu ya kitabu cha Wakolosai kutoka katika lugha ya Kigiriki (tafsiri ya kwanza kabisa ya Biblia ya Kihebrania ilikuwa ni katika lugha ya Kigiriki) kwenda katika lugha ya Kiingereza, na katika lugha zingine.
ReplyDelete