195. Sipendi dharau: mimi kumdharau mtu au mtu kunidharau mimi.
Sitakudharau kwa sababu sikujui. Hupaswi kunidharau kwa sababu hunijui.
Mzazi
hamjui mtoto wake na mtoto hamjui mzazi wake. Kila mtu hapa duniani ni
wa kipekee na wanasayansi wanatuambia kuwa tuko peke yetu hapa
ulimwenguni. Lazima tujifunze kupendana na kuheshimiana.
Mama mmoja alimpenda sana mtoto wake hata akatoa jicho lake moja
na kumpa mwanaye ambaye alipata ajali ya gari akiwa mdogo na kupofuka
jicho moja. Mama na mtoto na mume wake walikuwa wakitokea Dumila,
Morogoro, lakini walipofika Gairo gari lao dogo lilipinduka, lakini
baadaye mume akafariki alipokuwa hospitalini Dodoma. Mama alikuwa na
mapenzi yasiyokuwa na masharti yoyote kwa mtoto wake, na mtoto
alionyesha mapenzi yasiyokuwa na masharti yoyote kwa mama yake.
Baada ya kumaliza masomo, kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya
Mazengo iliyokuwa pembezoni kidogo mwa mji wa Dodoma, mtoto alikwenda
Ulaya kwa masomo zaidi. Akiwa huko akaoa lakini akamsahau kabisa mama
yake pamoja na ndugu zake wote. Si kwa simu, si kwa barua, si kwa pesa!
Miaka mingi baadaye mama akawa amemkumbuka sana mtoto wake hata akaamua
kujichanga na akafanikiwa kupata hati ya kusafiria na viza kwenda Ulaya
kumtafuta mwanaye. Ulaya kuna Watanzania ambao huyo mama aliwafahamu,
kupitia kwa waumini wenzake wa kanisa la Wasabato la Dodoma. Watanzania
hao walimsaidia kusafiri kwa maana ya udhamini na tiketi ya ndege, kwani
hata wao hawakupendezwa na tabia ya Mtanzania mwenzao. Alipofika
Lasembagi, ambapo ndipo mwanaye alikuwa akiishi na mke wa Kifaransa na
watoto wao wawili, mama alielekezwa nyumbani kwa mwanaye na akachukuliwa
teksi ambayo ilimpeleka moja kwa moja mpaka kwenye anuani ya nyumba
yake. Cha kushangaza, yule mtoto akamkana mama yake na akamfukuza kama
mbwa na mama akaondoka huku machozi yakimtoka katika jicho lake moja.
Miaka mitatu baadaye yule mtoto alikuja Tanzania kutalii akiwa na mke
na watoto wao wawili. Wakiwa Dar es Salaam, watu wakampa taarifa za
msiba wa mama yake. Nafsi ilimsuta. Hata mke wake nafsi ilimsuta pia!
Walipotoka Manyara, ambapo walikwenda kuangalia wanyama, mke akamsihi
mume wakahani msiba wa mama yake. Hivyo, wakasafiri kwenda Dodoma.
Walipofika Area C, nyumbani kwa mama yake, walikutana na majirani. Mama
mmoja akamkabidhi yule mtoto barua aliyopewa na marehemu ili amkabidhi
palipo majaaliwa.
Barua ilikuwa na ujumbe mzito na wa
kusikitisha. Mama alimwomba radhi mtoto wake kwa makosa yoyote ambayo
labda aliwahi kumfanyia. Hakukumbuka kama aliwahi kumfanyia mwanaye
makosa ya aina yoyote ile licha ya kumchapa, kwa faida ya mtoto mwenyewe
ya baadaye. Barua ilikuwa ndefu. Lakini ilimalizia kwa kusema,
“Nilikupenda mwanangu, nakupenda hata sasa, na nitakupenda daima. Siku
yoyote Mungu atakapokupa neema ya kurudi, kama nitakuwa hai,
nitakuchinjia kuku; kama nitakuwa nimekufa, nitatumia mifupa yangu
kukukumbatia.”
Yule mama hakuwa na makosa. Mtoto alikuwa na
makosa. Lakini hawa walikuwa ni watu wawili tofauti, kabisa! Mama
hakumjua mtoto wake, na mtoto hakumjua mama yake. Mama hakujua kama
mtoto wake alikuwa na akili ya kumgeuka. Mtoto hakujua kama mama yake
alimpenda kwa dhati!
Kuna nguzo saba ambazo hazina budi
kuzingatiwa kama unataka kuheshimiwa na kuwaheshimu wengine. Kwanza
kabisa jitambue: wewe ni nani na unafanya nini hapa duniani. Halafu,
kabla ya kusema jambo lolote kwa mtu yoyote fikiria kwanza maana au
madhara ya hilo unalotaka kulisema. Kisha jifunze tamaduni mbalimbali na
watendee wengine kama vile unavyotaka kutendewa au kama vile
wanavyotaka kutendewa. Jifunze kusamehe na kusuluhisha migogoro katika
jamii unamoishi huku ukidumisha heshima na utu kwa binadamu wenzako.
Jijengee imani kwa watu, punguza upendeleo, fanya kazi kama timu kwani
hakuna ‘mimi’ katika umoja ila kuna ‘sisi’, na jitahidi kwa kadiri ya
uwezo wako WOTE kwa manufaa ya wote. Kuwa kiongozi katika kila jambo
unalofanya na katika kila kitu unachofanya. Jitahidi kufanya jambo au
kitu kwa usahihi kwa kadiri utakavyoweza.
Migogoro inatokea
kwa sababu watu wameshindwa kuheshimiana. Ukijiheshimu na ukaheshimu
wengine, utaacha dunia katika hali nzuri kuliko ulivyoikuta.
http://www.facebook.com/koloniasantita
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Roho Yako
289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...
-
KITENDAWILI CHA KOLONIA SANTITA Shilingi milioni moja za Kitanzania kushindaniwa ndani ya miezi sita kuanzia leo Swali: Kila namba ...
-
Mpelelezi wa Tume ya Dunia kutoka Jerusalem, Israeli, Kanali Daniel ‘Yehuda Ben-Asher’ Ebenezer, Daniel Yehuda, alikuwa komandoo wa kit...


Ukitaka kuwa na mahusiano mema na watu wa muhimu katika maisha yako, waheshimu. Heshima yako itakulipa!
ReplyDeleteTuko peke yetu ulimwengu mzima halafu bado tunagombana na kudharauliana!
ReplyDelete