Monday 7 May 2018

Nuru ni Ukweli wa Kiroho

276. Musa asingekufa wana wa Israeli wasingefika Kanaani. Kwa sababu alikuwa tayari kwenda kuzimu ili wenzake waende mbinguni. Musa alikuwa katika nuru. Alimwasi Mungu katika maji ya Meriba, lakini maji yalitoka. Alikubali kumkosea Mungu kusudi wenzake wabarikiwe, na kweli wakabarikiwa. Nuru ni ukweli wa kiroho. Ukiwa katika nuru miujiza itatokea. Jisikie raha kuumia kwa ajili ya matatizo ya watu. Vaa viatu vya yule anayeumia, ili ujue anaumia kiasi gani, kisha msaidie kwa kadiri ya uwezo wako wote.

Sisi wote tunao uwezo wa kufanya miujiza na kweli ikatokea. Kama mtu anaumwa, tunao uwezo wa kusema apone na kweli akapona. Lakini lazima tuwe tayari kuumia kwa ajili ya hao tunaowaombea miujiza, na hao tunaowaombea miujiza lazima waamini kama kweli tunao uwezo wa kuwaombea miujiza hiyo.

Mtu anapoumwa, hata kama si ndugu yako, unaumia kiasi gani kumwona anaumwa? Uko tayari kujitolea kiasi gani kuhakikisha anapona na kurudia hali yake ya kawaida? Kwa nini leo wale wanaofanya miujiza hata kwa kutamka tu jambo likawa ni wachache sana kuliko wale wa kipindi cha akina Ibrahimu, Musa au Yesu? Kwa sababu leo hatuko tayari kujitolea maisha yetu kwa ajili ya watu wengine kupata miujiza.

Miriamu dada yake Musa na Haruni alipofariki huko Kadeshi katika mwezi wa kwanza wa mwaka wa arobaini wana wa Israeli walikosa maji. Miriamu ndiye aliyekuwa baraka ya maji ya wana wa Israeli jangwani, kwani Mungu aliwapa neema ya kisima cha maji popote pale walipopita kwa sababu ya Miriamu. Miriamu alipofariki, baraka hiyo ilifikia kitembo. Hivyo wana wa Israeli wakajikuta hawana maji.

Kwa nini Musa alikaidi agizo la Mungu? Kwa sababu alikuwa na huzuni kubwa juu ya kifo cha dada yake mpendwa na juu ya malalamiko ya wana wa Israeli kuhusu maji na mambo mengine. Kumbuka Miriamu alikuwa na mchango mkubwa sana katika maisha ya Musa. Farao alipotoa amri ya kuua watoto wote wa kiume wa wana wa Israeli, baba yao Amramu alimtaliki mama yao Yokebedi. Mimba ya Musa ilikuwa bado haijatungwa. Lakini ukatili wa Farao ulipozidi, Amramu alisalimu amri na kuwa mateka wa Farao; kama walivyofanya waume wengine wote wa Kiisraeli katika jamii ya Wamisri.

Nabii Miriamu ndiye aliyerudisha moyo wa Amramu nyuma na kukubali kumwoa tena Yokebedi. Hapo ndipo Musa akazaliwa, na hapo ndipo uhakika wa wokovu wa wana wa Israeli ukathibitika.

Baada ya Musa kuzaliwa, mama yake alipomficha katika magugu ya Mto Nile akiwa mtoto mdogo, Miriamu ndiye aliyemlinda na ndiye aliyemshawishi binti wa Farao amchukue Musa akamlee nyumbani kwao.

Kwa hiyo, Musa alikuwa na wakati mgumu wakati Mungu akimwagiza aongee na mwamba ili maji yatoke huku wana wa Israeli wakilalamika bila kukoma. Alikuwa akiomboleza kifo cha mtu wa muhimu sana katika maisha yake, kilichosababisha akose hata uwezo wa kuwaongoza tena wana wa Israeli.

Wana wa Israeli walipoendelea kulalamika kuhusu maji na mambo mengine, Mungu alimtokea Musa na Haruni katika hema. Alimwambia Musa awakusanye watu kisha aseme na mwamba mbele yao, kwamba maji yangetoka na watu na wanyama wao wote wangekunywa.

Musa na Haruni walipofika kwenye mwamba husika, badala ya kuongea na mwamba kama walivyoagizwa, Musa akaupiga mwamba huo kwa fimbo mara mbili, maji mengi yakatiririka kwa kiasi cha ajabu! Fimbo ile haikuwa kwa ajili ya kupigia mwamba, ilikuwa kwa ajili ya kukusanyia watu.

Lakini Mungu akawakasirikia Musa na Haruni. Kwa nini? Kwa sababu waliasi kinyume cha neno lake pale kwenye maji ya Meriba! Mungu alimwambia Musa aongee na mwamba lakini yeye akaupiga mwamba huo, tena akaupiga fimbo mara mbili. Mungu akamwambia Musa na Haruni akasema, kwa sababu hawakumwamini hawangeweza kufika katika Nchi ya Ahadi.

Ukikisoma vizuri kisa cha Musa na mwamba utaona kuwa Musa na Haruni walifanya kosa kubwa la kizembe. Mungu alisema wafanye hiki lakini wao wakafanya kile. Mungu akawaadhibu, lakini akawapa wana wa Israeli baraka ya maji kama Musa na Haruni walivyoomba.

Mungu alikubaliana na kile ambacho Musa na Haruni walifanya ijapokuwa lilikuwa kosa. Maana maji yalitiririka kutoka kwenye mwamba! Kama Musa na Haruni walikosea kwa nini Mungu aliwapa wana wa Israeli muujiza wa maji? Kwa nini hakuwanyima kwa sababu viongozi wao walikosea? Huwezi kumzawadia mtu aliyekosea. Unamzawadia mtu aliyepatia. Kama Musa alikosea kwa nini maji yalitoka?

Kile alichokifanya Musa na Haruni hakikuwa na makosa machoni pa wanadamu; hakikuwa na makosa machoni pa Mungu pia! Lakini mtu mwenye haki yukoje? Mwenye haki ni yule ambaye siku zote yuko tayari kuumia kwa ajili ya watu wengine. Hata kama tendo analotaka kufanya kuwasaidia wengine litamkasirisha Mungu yuko tayari amkasirishe ili Mungu huyohuyo awabariki wengine.

Sisi wote ndivyo tunavyotakiwa kuwa. Tunatakiwa kuwa na upendo usiokuwa na masharti yoyote; na tunatakiwa kuwa tayari kufa kwa ajili ya maisha ya wenzetu.

Upendo usiokuwa na masharti yoyote una nguvu kubwa kuliko ulimwengu wote. Mathalani, uongo ni kitu kibaya. Dini zote zinakataza uongo. Lakini kama itakubidi kuongopa kuokoa maisha ya mtu, uongo ni kitu kizuri. Kwa sababu hakuna kitu kizuri kama maisha ya mtu.

Musa alipiga jiwe mara mbili kwa sababu kuna baadhi ya wana wa Israeli hawakuamini kama maji yangetoka. Kwa sababu hiyo alikuwa tayari kuangamia ili wenzake wabarikiwe.

Utafanya nini kuwasaidia watu wengine hata kama ni kwa gharama ya maisha yako? Utakuwa tayari kufa ili wengine waishi; kama itakubidi hata kuacha kazi yako ili mtu apone acha na atapona kwa ruhusa ya Mungu.

1 Yohana 2:10 inasema, “Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo.”

Jisikie raha kuumia kwa ajili ya matatizo ya wengine. Vaa viatu vya yule anayeumwa ili ujue anaumwa kiasi gani, kisha msaidie kwa kadiri utakavyoweza. Kama hana damu au figo zake zimefeli, uwe tayari kutoa damu au figo kumsaidia. Ukifika kwenye ngazi hiyo ya upendo, ukiomba muujiza ili mgonjwa apone, anaweza kupona. Si kuomba muujiza ilhali wewe ni mnafiki.

No comments:

Post a Comment

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...