Monday 21 August 2017

Ulimwengu wa Roho

239. Ulimwengu wa roho au ulimwengu wa giza ni vitu halisi ambavyo vipo, na vinafanya kazi usiku na mchana, ingawa haviwezi kuonekana kwa macho. Kitu kinachofanya kila kitu kionekane hakionekani. Kwa nini hatuwezi kuona mwanga?

Umewahi kuona hewa? Hapana. Unaamini kama hewa ipo? Ndiyo. Umewahi kuona upepo? Hapana. Unaamini kama upepo upo? Ndiyo. Umewahi kumwona Mungu? Hapana. Kwa nini usiamini kama Mungu yupo?

Binadamu hawezi kuona hewa, lakini ipo. Molekuli zake zikikusanywa kwa pamoja zina uwezo wa kunyanyua ndege kubwa kutoka ardhini. Hakuna anayeweza kuona molekuli, atomu, elektroni, nutroni au protoni, lakini zipo. Hapa duniani kila siku tunakabiliana na nguvu nyingine nyingi ambazo haziwezi kuonekana kwa macho, kama vile umeme na mwanga, lakini zipo.

Hicho ndicho kiini cha maana ya ulimwengu wa roho, au ulimwengu wa giza. Hakuna anayeweza kubisha kuwa hewa, inayotumika kuunda upepo, si kitu halisi; na licha ya kuwa haionekani, imeundwa kwa chembe ndogo mno zisizoweza kuonekana kwa macho ya kawaida.

Biblia hutoa ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa Mungu na malaika si viumbe hewa waliozagaa huko na huko ulimwenguni. Mungu si akili ya ulimwengu wote, dhamiri, au wema. Hana uwezo dhahania uwezao kuujaza ulimwengu wote kwa wakati wote. Tofauti pekee kati ya binadamu na Mungu licha ya tofauti kubwa ya nguvu na uwezo ni kwamba binadamu ni mwili wa kidunia ambaye maisha yake yamo ndani ya damu, wakati Mungu pia ni mwili lakini ulioundwa kwa Roho na milele.

Kauli hii ina utata ambao unafaa kufanyiwa utafiti wa kina, kwa sababu inaonyesha kuwa Mungu hawezi kuwa kila mahali akiwa katika mwili mmoja.

Maelezo thabiti ya Biblia kuhusu wasifu wa Mungu huonyesha kuwa Mungu yuko mahali pake kwa wakati mmoja, na anaonekana akisimamia au kushiriki moja kwa moja katika uumbaji wake. Tunamwona akiwa ameketi, amesimama, akitembea, akiongea, akila, akinywa, akitoa amri kwa malaika, na kadhalika, akiwa katika makazi yake maalumu.

Lakini hakuna mahali popote palipotajwa ukubwa wa Mungu, na hivyo hitimisho lazima liwe kwamba ni wa kawaida, mwenye umbo la kibinadamu; na alipokuwa binadamu, Maandiko yanasema, hakukuwa na ishara yoyote iliyoonyesha kwamba ni Mungu isipokuwa tabia na mafundisho yake yaliyotukuka.

Mwanga ni nishati ambayo ndani yake kuna chembe ziitwazo ‘photons’, na huonekana kwa darubini pekee katika ulimwengu wa nyama. Pia ni inkishafi, maono ya ghafla akilini mwa mtu kutoka katika ulimwengu wa roho. Nuru ni mwanga unaonekana kwa macho. Ukiwasha tochi usiku unachokiona ni nuru ya mwanga.

Kitu kinachofanya kila kitu kionekane hakionekani. Kwa nini hatuwezi kuona mwanga? Hatuwezi kuona mwanga kwa sababu, wengi wetu, hatuna macho ya rohoni.

1 comment:

  1. Hivyo ndivyo ulimwengu wa roho ulivyo. Hatuwezi kuuona lakini upo na unafanya kazi.

    ReplyDelete

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...