Monday, 14 August 2017

Ahadi za Mungu

238. Wachungaji wengi ni watumishi wa fedha na mali si watumishi wa Bwana. Mungu wao ni Mammon, ambaye ni mungu wa uchoyo na utajiri wa dunia hii.

Wachungaji waliofanikiwa sana katika maisha uhubiri kile kinachoitwa “Injili ya Mafanikio”. Kwa kutumia baadhi ya Maandiko, wanafundisha kuwa iwapo mtu atampa Yesu maisha yake, na iwapo atafuata kanuni fulani za kibiblia, Mungu ana wajibu wa kutimiza ahadi zake za utajiri, afya, na maisha bora. Mwishowe, Mungu anakuwa kama Shetani anayetoa baraka hata kwa mambo ambayo ni mabaya, akiwatimizia watu kila kitu kulingana na matakwa ya mioyo yao. Kwa wahubiri hawa, haya ndiyo maisha bora ambayo Mungu anatuahidi, na mamilioni ya watu wanakubaliana nao.

Ni kweli kwamba Biblia imejaa ahadi. Pia ni kweli kwamba Yesu anatuambia mara kadhaa katika Yohana 14-16, “Mkiniomba neno lolote kwa jina langu, nitalifanya” (Yohana 14:14; angalia pia 14:13; 15:7,16; 16:23-24, 26). Zaburi 37:4 inasema, “Nawe utajifurahisha kwa BWANA, Naye atakupa haja za moyo wako.” Mafungu haya huonekana kama ahadi za kweli kabisa, na kama Mungu ni mkweli kwa Neno Lake, lazima atazitimiza, sivyo?

Hivi ndivyo wachungaji walivyohitimisha, lakini mwishowe, ni hitimisho jepesi mno. Kuna ahadi chache mno za Mungu katika Biblia ambazo ni za kweli kabisa kiasili. Badala yake, ahadi hizo zina masharti, zikiongozwa si tu na majibu yetu kwa Mungu, zikitimiza mahitaji fulani, lakini pia kwa hukumu kamili ya Mungu.

Kama Yakobo 1:17 inavyosema, Yeye hutoa zile zawadi ambazo ni nzuri tu na kamilifu; kamwe hatatoa “baraka” kwa mtoto wake yeyote ambayo baadaye itafanya aukose ufalme wa mbinguni au baraka itakayokuwa kubwa sana zaidi ya uwezo wake.

Hata kwa walalahoi iko hivyohivyo. Mzazi hataweza kumpeleka mwanawe katika shule ya ufundi kama kweli alitaka awe daktari, hata kama masomo ya ufundi lingekuwa jambo zuri kwa mtoto wake. Hali kadhalika, mzazi huyohuyo hatamwamini mwanawe kumpa mamilioni ya pesa ili akanunue vitu Mlimani City, licha ya ukweli kwamba kiasi hicho cha pesa kwa mtoto kingeonekana kama zawadi ya ajabu kabisa.

Kama wazazi wana hekima ya kutosha kuwapa watoto wao kiasi cha kutosha ili waweze kufanya mambo ya maana katika maisha, Mungu anaweza kuwapa watoto wake kiasi gani (Warumi 11:33)?

Baba wa imani Ibrahimu na Sara ni mifano mizuri ya aina hii ya ahadi za Mungu. Katika Mwanzo 12:2, Mungu anamwambia Ibrahimu, akiwa na umri wa miaka 75 kipindi hicho (mstari wa 4), kwamba atamfanya kuwa “taifa kubwa”, akimaanisha kwamba atapata watoto. Mungu anatoa ahadi hii tena katika mstari wa 7: “BWANA akamtokea Abramu, akasema, ‘Uzao wako nitawapa nchi hii.’” Lakini, bado hampi Ibrahimu mtoto wa ahadi akiwa na umri wa miaka 76 au 78 au 80!

Rutu baada ya kuokolewa kutoka shirikisho la wafalme, Ibrahimu anapatana na Mungu katika Mwanzo 15:2-3 – Ibrahimu hapo akiwa na umri wa miaka 80 – kuhusu mrithi. Mungu anarudia ahadi, na Ibrahimu anamwamini Mungu (mistari ya 4-6), lakini Sara si mjamzito bado. Baadaye, baada ya Ismaili kuzaliwa Ibrahimu akiwa na umri wa miaka 86 (Mwanzo 16:16), Ibrahimu anashangaa kama kweli hii ni mbegu ya ahadi, lakini wakati Ismaili ana umri wa miaka kumi na tatu – Ibrahimu sasa akiwa na miaka 99! – Mungu anasema tena na Ibrahimu, “Sivyo, lakini Sara mkeo atakuzalia mwana wa kiume (Mwanzo 17:19).

Hatimaye, Mungu alimtembelea Sara kama alivyoahidi, na alimtendea Sara kama alivyosema. Kwani Sara alipata mimba, na Isaka alizaliwa Ibrahimu akiwa mzee, katika muda mahususi ambao Mungu aliongea na Ibrahimu. Ibrahimu alikuwa na umri wa miaka mia moja wakati mwanawe Isaka anazaliwa.

Ni wazi kwamba mambo mengi yalipaswa kutokea katika maisha ya Ibrahimu na Sara, hususan yale yaliyohusu suala la ukomavu wa kiroho, kabla Mungu hajaona muda mwafaka ulikuwa umefika wa kuwapa mtoto wao wa kiume aliyewaahidi. Mungu alitimiza ahadi yake baada ya miaka ishirini na tano kupita.

Tambua kwamba maandiko yenyewe yanatuambia kuwa Mungu alifanya muujiza kuruhusu Sara apate mimba “katika wakati uliopangwa.” Kulikuwa na wakati mmoja kamili kwa ajili ya ahadi hii kutimizwa, na Mungu aliitimiza katika kipindi ambapo hali zote zilikuwa sahihi.

Na tunaweza kumshukuru Mungu bila kukoma kwa kufanya hivyo kwa ajili yetu (II Wakorintho 4:15).

Mungu anamsaidia yule anayetaka kumsaidia. Alimpenda zaidi Yakobo kuliko Esau licha ya kwamba walikuwa mapacha. Alimkubali zaidi Abeli kuliko Kaini watoto wa wazazi wetu wa kwanza Adamu na Hawa. Alimchagua Nuhu peke yake miongoni mwa mamilioni ya watu wengine ambao angeweza pia kuwachagua. Ibrahimu alikuwa mpagani; lakini, akiwa na umri wa miaka 70, bado Mungu akamchagua yeye na kumbariki.

Mungu anapokuchagua kufanya kazi yake haijalishi wewe ni nani au unafanya nini, usifikirie mara mbili, fanya kazi hiyo mara moja.

Ahadi nyingi zinazohubiriwa na baadhi ya wachungaji si ahadi za kweli. Ahadi za Mungu ni ahadi za kweli, zenye vipengele ndani yake, ambazo hutimia baada ya vipengele vyote kutimia.

Maombi yako yasipojibiwa usikate tamaa, Mungu alishakusikia na tayari alishaandaa malaika wa kukuletea jibu. Jibu wakati mwingine huchelewa kufika kwa sababu ya nguvu za giza. Usiwe na haraka, muda wako ukifika utajibiwa.

No comments:

Post a Comment

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...