Mwaka 1992, mara tu baada ya kuhitimu masomo yangu ya kidato cha nne, nilianza kuandika Kolonia Santita. Kipindi hicho iliitwa Salina Cruz. Kolonia Santita ni kitongoji ndani ya Salina Cruz, katika jimbo la Oaxaca, nchini Meksiko, hapo ndipo shirika la madawa ya kulevya la Kolonia Santita lilipozaliwa.
Nikiwa hapa Dar, niliandika riwaya ya Kolonia Santita kila siku kwa muda wa miezi mitatu mfululizo. Nilihamasishwa na watu na mambo mengi.
Miaka miwili kabla ya hapo, yaani mwaka 1990, niliandika hadithi yangu ya kwanza kabisa iliyoitwa Magaidi wa Namba One. Namba One ni eneo lililoko nje kidogo ya mji wa Dodoma, kama unakwenda Iringa au Bihawana.
Kuanzia hapo moto ukalipuka moyoni mwangu wa kuwa mwandishi rasmi wa riwaya, hasa riwaya za kijasusi, kwa sababu hadithi yangu ya kwanza ilikuwa ya kijasusi. Hivyo, licha ya kuhamasishwa na watu na mambo mengi, nilihamasishwa na mimi mwenyewe.
Mwaka 1994 niliupeleka muswada wa Kolonia Santita katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya kuuchapa kwenye kompyuta kwa dada mmoja aliyekuwa akifanya kazi pale. Kwa bahati mbaya simkumbuki jina huyo dada na sijawahi kumwona tena.
Nikiwa na muswada wangu kwenye disketi, mwaka 1999, niliupeleka kwenye kampuni ya uchapishaji kwa mara ya kwanza ili uchapishwe kitabu. Lakini ndani ya mwaka huohuo nikauchukua tena muswada wangu na kujiwekea nadhiri ya kuuchapisha kama kitabu mimi mwenyewe nje ya Afrika.
Hata hivyo, nikiwa Uingereza, mwaka 2004, sikuandika chochote kuhusiana na Kolonia Santita kwa angalau mwaka mmoja na nusu.
Lakini baada ya hapo nilianza tena rasmi kufanya utafiti wa Kolonia Santita. Hilo likanipelekea mwaka 2008 kuweka nadhiri ya miaka mitano ya kuhakikisha hadithi ya Kolonia Santita inakamilika na kuchapishwa kama nilivyotarajia tangu mwaka 1999.
Mungu si Athumani. Mnamo mwaka 2012 Kolonia Santita ikachapishwa kama kitabu kwa mara ya kwanza na kampuni ya uchapishaji wa vitabu ya Author Solutions ya Uingereza na Marekani.
Author Solutions ikawa kama vile imefungua milango fulani ya bahati! Kwani mwaka 2015 Kolonia Santita ilishinda Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornel ya Fasihi ya Kiafrika. Na mwaka 2017 ikachapishwa RASMI na kampuni ya uchapishaji wa vitabu ya East African Educational Publishers (EAEP) ya Nairobi, Kenya.
Sasa nitasoma kipengele ndani ya kitabu cha Kolonia Santita. Nitaanza na John Murphy akitumbukia ardhini; na nitamalizia na ‘foreshadowing’ kubwa kuliko zote katika kitabu cha Kolonia Santita, ‘foreshadowing’ iitwayo ‘Peter Peter’, kuanzia ukurasa wa 122 hadi 124.
Baada ya hapo niliulizwa maswali mengi, sana, kutoka kwa wadau wa fasihi, ambayo nitayapeleka EAEP kwa ajili ya uhariri.
Majadiliano ya namna hii ya vitabu, hasa vitabu vya Kiswahili, yanapaswa kupewa kipaumbele kikubwa iwapo tunataka kupambana na ugonjwa wa kutokupenda kujisomea. Nawashukuru sana
No comments:
Post a Comment