Thursday, 12 January 2017

Vijue Zaidi Vidonge vya Eksitasi - Dawa ya Kulevya Inayotumika Katika Majumba ya Starehe Duniani Kote

Eksitasi na methi ni biashara kuu ya tatu ya Kolonia Santita baada ya kokeini na heroini. Maabara ya kutengenezea eksitasi na methi ya Kolonia Santita (inayoitwa ‘maquiladora’ au kiwanda cha uzalishaji) yenye uwezo wa kutengeneza vidonge 17,000 vya eksitasi kwa saa na tani 20 za methi kwa mwezi, zenye thamani ya mtaani ya shilingi trilioni moja za Kitanzania, ni kubwa kuliko zote katika Jimbo la Sinaloa.

Ndani ya methi kuna LSD (ambayo ni ‘Lysergic acid diethylamide’ – au ‘Laisajiki asidi dayatholamaidi’ kwa Kiswahili chepesi). Ndani ya eksitasi kuna MDMA (‘Methylenedioxymethamphetamine’ – au ‘Metholini-dayoksi-meth-amfetamini’ kwa Kiswahili chepesi). Hizi ni kemikali za taswira za kiwendawazimu.

Eksitasi, MDMA, au Furaha – Kamusi ya Enock Maregesi – ni vidonge vinavyotokana na madawa yanayotengeneza methamfetamini, vilivyotengenezwa kwa mara ya kwanza na Mkemia Fritz Harber mnamo mwaka 1898 huko Ujerumani (lakini vikapewa kibali rasmi na serikali mnamo mwaka 1914) na ambavyo leo hii vimekuwa na umaarufu mkubwa hususan katika majumba ya starehe ya Ulaya na Amerika. Koka hutengeneza kokeini. Afyuni hutengeneza heroini. ‘Ephederine’ au ‘afedrini’ hutengeneza methi. Sassafrasi hutengeneza eksitasi.

Mafuta ya sassafrasi (‘sassafrass’) yamekuwa malighafi muhimu sana katika utengenezaji wa viungo vya chakula, manukato ya wanawake na wanaume na dawa za kuulia wadudu kwa karne nyingi. Kiungo kikuu cha mafuta ya sassafrasi ni safro (‘safrole’) ambayo kikemia huweza kugeuzwa na kuwa ‘isosafrole’. Safro na ‘isosafrole’ hutumika kama malighafi ya mwanzo kabisa katika utengenezaji wa eksitasi.

Safro ilitumiwa kwa mara ya kwanza kama malighafi ya eksitasi na mkemia wa Kijerumani Fritz Habar mnamo mwaka 1898; lakini kidonge halisi cha eksitasi kilikuwa hakijatolewa kibali mpaka mwaka 1914, kampuni ya madawa ya Merck iliporuhusiwa kisheria kukitengeneza.

Eksitasi inaweza kutengenezwa kirahisi mno kwa kutumia safro, na bei yake ni ndogo sana kulinganisha na baadhi ya madawa kama kokeini na heroini.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka ya Kituo cha Uangalizi wa Madawa na Uraibu wa Madawa cha Bara la Ulaya (EMCDDA – ‘European Monitoring Centre for Drugs and Drugs Addiction’), uzalishaji wa eksitasi na methi waweza kukadiriwa kufikia mpaka tani 520 kwa mwaka duniani kote.

Eksitasi huzalishwa zaidi barani Ulaya, huku Uholanzi ikiwa ya kwanza kwa uzalishaji, na pia Kusini Mashariki mwa Asia (China, Indonesia, na Hong Kong) na Amerika ya Kaskazini.

Kwa mujibu wa ripoti hiyohiyo ya EMCDDA, tani 8.5 za eksitasi zilikamatwa mwaka 2004 katika operesheni ya dunia nzima; asilimia 50 ya hizo ikitoka Ulaya ya Kati (na Magharibi), 23 ikitoka Amerika ya Kaskazini, na 16 ikitokea Oshania (‘Oceania’).

Bei ya wastani ya kidonge cha eksitasi mwaka 2004 ilikuwa karibu shilingi 6,000 za Kitanzania nchini Polandi na nchi za Mashariki, na shilingi 30,000 – 50,000 za Kitanzania nchini Ugiriki na Italia.

Malighafi, kama vile mafuta ya sassafrasi, inayotumika kutengeneza eksitasi na aina zingine za methi, hufikirika mara nyingi kutumiwa na mamafia wa madawa ya kulevya. Kukomesha na kuzuia biashara isiyo halali ya eksitasi, mamlaka za kimataifa zimeunda sheria na taratibu za kiushirikiano za udhibiti wa kemikali tangulizi (‘precursors’) za eksitasi; na kemikali zingine zinazotumika katika uchakataji wa uzalishaji wa sassafrasi.

Mafuta ya sassafrasi hupatikana kutoka katika mizizi na matawi ya aina mbalimbali ya miti. ‘Sinamomamu Pathenoksiloni’ (‘Cinnamomum Parthenoxylon’) kwa mfano, ni mmea kutoka Indochina wenye kiwango kikubwa cha safro – ambao sasa umejumuishwa katika kitabu chekundu cha Umoja wa Kimataifa wa Hifadhi ya Maliasili (au IUCN kwa kifupi).

Huu si mfano pekee unaoweza kutajwa na wadau. China ni mteja mkubwa wa mafuta ya sassafrasi, kuliko nchi zote duniani, ikiwa imefikisha mpaka kiwango cha matumizi ya tani 2000 kwa mwaka – kwa ajili ya kutengeneza kemikali ya manukato na viungo iitwayo ‘heliotropine’ na bidhaa zingine.

Vyanzo vya mafuta ya sassafrasi vimekuwa vigumu sana kupatikana siku hizi kutokana na sheria kali za mamlaka, na jitihada za serikali katika kuzuia ukataji miti ovyo katika misitu ya ukanda wa joto. China, Brazili na Vietnamu – ambao ndiyo wazalishaji wakuu wa mafuta ya sassafrasi – zimepiga marufuku ukataji miti ili kuzuia uhaba wa miti kwa jumla.

Brazili ndiyo ilikuwa nchi ya kwanza kuzuia mavuno ya miti ya sassafrasi mwaka 1990. Kisha Vietnamu ikachukua nafasi ya Brazili kama mzalishaji; lakini mnamo mwaka 1999, Vietnamu nayo ikazuia mavuno; huku usafirishaji wa sassafrasi nje ya nchi ukisimama kabisa mnamo mwaka 2000. Mpaka kufikia mwaka 2003, Vietnamu ilikuwa ikifuata sera ya kuingiza sassafrasi nchini mwake na kuisafirisha tena kwenda nchi za nje.

Kuanzia mwaka 2003 uzalishaji ulihamia nchini Kambodia katika Milima ya Cardamom inayodhibitiwa na Khmer Rouge (chama cha kikomunisti cha Kampuchea, Kambodia), lakini miaka michache tu baadaye (kuanzia mwaka 2005) serikali ya Kambodia ikapiga marufuku uvunaji wa miti inayotoa sassafrasi hali kadhalika – ambayo sasa inajulikana zaidi kama miti iliyoko hatarini sana kupotea.

Kimsingi sheria ya usimamishaji wa uzalishaji haikufanya kazi sawasawa. Tangu mwaka 2005 zaidi ya tani 600 za mafuta zilizalishwa na kusafirishwa nje ya nchi. Sheria kali zaidi kutoka serikalini – ikisaidiwa na Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya Nchini Marekani DEA – ilipelekea kukamatwa kwa makontena matatu (kwenye bandari ya Tailandi Oktoba 2007) yaliyokuwa na tani 50.4 za safro, zilizokuwa tayari kusafirishwa kwenda Amerika na China.

Mwaka 2008 (Juni) ushirikiano wa mamlaka za Kambodia na jeshi la polisi la Australia ulizuia na kukamata tani 33 za mafuta ya safro, zilizokuwa na uwezo wa kutengeneza vidonge milioni 245 vya eksitasi. Kwa mujibu wa azimio la Ubalozi wa Australia nchini Kambodia, vidonge hivyo vilikuwa na thamani ya mtaani ya shilingi trilioni 11.8 za Kitanzania. Mafuta hayo yaliharibiwa na serikali ya Kambodia kwa kuyachoma moto katika kipindi cha siku tatu mfululizo, chini ya usimamizi wa jeshi la polisi la Australia.

Mamlaka za Kambodia zimekuwa zikifanya kazi usiku na mchana toka mwaka 2002 kuzuia uzalishaji wa mafuta ya safro; na tangu kipindi hicho zimefanikiwa kugundua na kuharibu zaidi ya maabara 50 za siri, zilizokuwa na uwezo wa kuzalisha hadi galoni 15 za mafuta kwa siku kwa mujibu wa jeshi la polisi la Australia.

Uzalishaji wa mafuta ya sassafrasi nchini China unadhibitiwa vikali na serikali, lakini makampuni ya Kichina (na hata yale ya Kivietnamu) hufanya shughuli zake nchini Laosi na Bama katika vipindi tofautitofauti. Biashara ambayo makampuni hayo yanafanya si halali; lakini pamoja na hilo, tani chache za mafuta ya safro kutoka katika maeneo hayo huingia nchini China mara kwa mara kwa njia za kimafia.

Ndani kabisa ya Milima ya Cardamon na Hifadhi ya Taifa ya Phnom Samkos huko magharibi mwa Kambodia, viwanda vya siri vinatengeneza mafuta ya safro kwa ajili ya kutengeneza vidonge vya eksitasi. Matokeo yake serikali ya Kambodia inalipa gharama kubwa kwa maana ya mazingira.

Miti yenye mafuta ya safro, yanayofanana na mafuta ya samli kwa kiasi fulani, hukatwa wakati wa uchakataji wa uzalishaji (‘manufacturing process’). Mizizi ya miti hiyo, pamoja na matawi, ambayo ndiyo sehemu hasa yenye mafuta ya safro, hukatwa kwa misumeno ya umeme na baadaye kuchemshwa ndani ya mapipa makubwa ya chuma. Kimiminika kinachotokea baada ya hapo huchujwa kitaalamu (‘distilled’) juu ya mioto inayohitaji kiasi kikubwa mno cha kuni kuweza kuichochea.

Uzalishaji wa mafuta ya safro ni biashara kubwa. Hivyo ukataji mkubwa wa miti, na mmomonyoko wa ardhi, uharibu kabisa sehemu za milimani zinazozunguka viwanda.

Mabaki ya mapipa na vifaa vyote vinavyotumika katika utengenezaji wa safro ni hatari kwa afya ya binadamu; na milipuko hutokea mara kwa mara. Mifereji ya jirani inayoleta maji kwa ajili ya upishi wa mafuta ya sassafrasi, muda si mrefu nayo huziba – kutokana na uchafu wa viwandani na hivyo kuathiri kabisa mazingira ya kibiolojia (‘ecosystem’) ya maeneo hayo. Hata mafuta yenyewe si salama. Mafuta ya sassafrasi huweza kusababisha ugonjwa wa saratani, na eksitasi husababisha sumu katika mishipa ya damu ya serotonini.

Pamoja na kwamba uzalishaji mdogo mdogo wa mafuta ya safro umekuwa ukiendelea kwa muda mrefu nchini Kambodia kwa ajili ya madawa ya kienyeji, na kwa ajili ya shughuli za kisayansi na tafiti za kitabibu, uzalishaji mkubwa wa mafuta ya safro kwa ajili ya biashara ya madawa ya kulevya umekuwa ukipungua – tangu mwishoni mwa miaka ya tisini.

Katika miaka ya hivi karibuni, mamlaka zimechukua hatua kali dhidi ya biashara ya safro; ikiwa ni pamoja na uvamizi wa hali ya juu wa kipolisi – kuwakumbusha watu kwamba, biashara ya safro itawapeleka jela. Uvamizi wa tarehe 12/6/2009 uliofanywa na taasisi isiyokuwa ya kiserikali inayojihusisha na hifadhi ya mazingira ya Flora and Fauna International, kwa kushirikiana na mamlaka za Kikambodia, walikamata madumu 142 yaliyokuwa na tani 5.7 za mafuta ya sassafrasi. Shehena hiyo, iliyokamatwa nyumbani kwa mtu katika kijiji cha O' Kambou, magharibi mwa milima ya Cardamom, ilikuwa na uwezo wa kuzalisha vidonge milioni 44 vya eksitasi; vyenye thamani ya mtaani ya shilingi trilioni 1.94 za Kitanzania.

Viwanda vingi vya mafuta ya safro vinaweza kupatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Wanyamapori ya Phnom (‘Fnam’) Samkos, ambayo inapatikana katikati ya Milima ya Cardamom na ambapo ndipo miti mingi ya sassafrasi inapopatikana.

Milima ya magharibi ya Cardamom ni sehemu ya ukanda mkubwa kuliko yote wa msitu wa mvua katika eneo la Kusini Mashariki mwa Asia; na ni makazi ya aina zaidi ya themanini za wanyama zilizoko mbioni kupotea; kama vile chui, tembo na mamba.

Mafuta ya safro, ambayo pia hutumika katika utengenezaji wa vipodozi na madawa ya kienyeji ya waasi wekundu (‘rouge’) wa Khmer, yanazalishwa kutoka katika mafuta ya mti unaojulikana kwa Kikhmer kama ‘Mreath Prew Phnom’ – ambao wataalamu hudhani ni Sinamomamu Pathenoksiloni (au ‘Cinnamomum Parthenoxylon’).

Aina hiyo ya miti inasemekana kuwa chache mno duniani, na nchini Vietnamu, imewekwa katika kundi la miti iliyoko hatarini sana kupotea. Mti wa Sinamomamu Pathenoksiloni hauna jina kamili kwa Kiingereza au Kiswahili, na hakuna mtu ajuaye ni miti kiasi gani ya namna hiyo imebaki duniani.

Miti minne ya ‘Mreath Prew Phnom’ hutakiwa kuzalisha pipa moja la galoni arobaini la mafuta ya safro, na miti mingine sita ambayo haina umuhimu sana hukatwa na kutumika kama kuni – kwa ajili ya mti mmoja wa ‘Mreath Prew Phnom’!

Wafanyakazi wanaopika na kuchuja mafuta ndani kabisa ya misitu, kadhalika hutegemea mawindo ya wanyama adimu wa msituni (kama kakakuona, tausi, chatu, duma na chui) kwa ajili ya chakula au kipato katika masoko kadha wa kadha ya wanyamapori. Uwindaji wa wanyama uhatarisha maisha ya wawindaji zaidi ya 15,000 wanaokaa pembezoni mwa hifadhi hizo za wanyama.

Kwa bahati mbaya mahitaji ya eksitasi na mafuta ya sassafrasi na mafuta ya safro, kwa ajili ya matumizi ya viwandani, bado hayajapungua hata kidogo. Kukidhi haja ya mahitaji ya leo ya mafuta haya, misitu ya ukanda wa joto wa dunia hii hupoteza miti kadiri ya 500,000 kwa mwaka. Miti hii haitoki mashambani, la hasha! Inatoka katika misitu ya asili ya China, Brazili, Vietnamu, na sasa Kambodia; licha ya juhudi za hizi nchi za kupiga marufuku uvunaji wa miti yenye mafuta ya sassafrasi au safro, na uchujaji wake kwa ajili ya kuzalisha mafuta.

Kutoka katika misitu mikubwa ya Kambodia, Vietnamu, Brazili na China, mpaka katika majumba ya starehe ya duniani kote; eksitasi itaendelea kuburudisha watu duniani – na mamafia wataendelea kufanya biashara haramu – iwapo watu hawatasimama kidete, kusema vidonge vya burudani sasa basi.

Eksitasi ni ngumu sana kudhibitiwa na serikali peke yake. Udogo wake (udogo wa umbo lake) hufanya iwe rahisi sana kulanguliwa na mamafia; na viwanda huweza kuhamishika kirahisi (kutoka msitu mpaka msitu au nchi mpaka nchi) kukwepa vyombo vya dola na taasisi za kimataifa.

Wataalamu wengi (hususan Wafaransa) wametahadharisha umma juu ya eksitasi, na madhara ya muda mrefu ya madawa hayo katika ubongo. Magonjwa mengi yanayohusiana na eksitasi ni mabaya. Unaweza kuugua kansa, mawazo na ugonjwa wa akili.

No comments:

Post a Comment

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...