Mungu alikuumba miaka mingi kabla hujazaliwa. Ndani ya roho yako kulikuwa na mpango mkuu wa Mungu juu ya maisha yako katika kipindi chote utakachokuwa hai, na katika kipindi chote utakachokuwa mfu. Lakini Shetani katika mji wa angani unaosemekana kuzuia majibu ya maombi ya Danieli ya siku ishirini na moja, kutoka mbinguni kuja duniani, uitwao Sadiki, wenye mashetani wenye nguvu kuliko mashetani wote katika ufalme wa giza, akaizuia roho hiyo kisha akaiwekea mpango mkuu wa Shetani juu ya maisha yako ili umtumikie yeye badala ya kumtumikia Mwenyezi Mungu.
Kwa mfano Mungu alipanga uzaliwe mkoani Arusha. Halafu akapanga mke au mume wako azaliwe mkoani Mwanza. Mkoani Arusha Mungu alipanga uwe mwinjilisti wa vitabu, wakati mkoani Mwanza alipanga mke au mume wako awe mwimbaji wa nyimbo za injili.
Katika mikoa yote miwili Mungu alishatuma malaika wema wa kuwasaidia katika mipango mikuu ya maisha yenu na kuwaepusha na hila zote za adui.
Lakini badala ya kuzaliwa Arusha au Mwanza Shetani akaziprogramu roho zenu upya ili wa Arusha azaliwe Dodoma au Mara au Venezuela, na wa Mwanza azaliwe Lindi au Kagera au Mombasa, ambapo hakutakuwa na malaika wema wa kuwasaidia. Badala ya kuwa mwinjilisti wa vitabu, Shetani atakufanya uwe jambazi; na badala ya kuwa mwimbaji wa nyimbo za injili, Shetani atakufanya uwe mwimbaji wa nyimbo za kilimwengu.
Ndiyo maana wakati mwingine ni vizuri kuhama sehemu unapoishi na kwenda kuishi sehemu nyingine, ambapo kwa kusaidiana na malaika wako wa mwanzo ambaye Mungu alikupangia kabla hujazaliwa, utafanikiwa katika maisha yako, kama alivyofanya Ibrahimu.
Roho ya mtu inapotoka kwa Mungu ili ije izaliwe duniani inapita katika mji wa angani uitwao Sadiki, uliotengenezwa na ulimwengu wa roho, kwa ajili ya kuzuia kila kitu kinachotoka mbinguni kuja duniani. Katika mji huo, mashetani yatajaribu kusoma kumbukumbu ya ‘destiny’ ya kila binadamu inayoitwa mpango mkuu wa maisha ya binadamu. Mpango mkuu inamaanisha maisha kamili ya mtu toka kuzaliwa hadi kufa na baada ya hapo, kile ambacho ulizaliwa kufanya hapa duniani.
Iwapo mashetani yatagundua kwamba unakuja duniani kufanya kazi ya Mungu, na kwamba una mpango wa kuleta madhara katika ufalme wa giza, yatabuni mpango mpya juu ya mpango asilia wa Mungu na kujifanya kama Mungu ndivyo alivyopanga.
Kwa mfano kama Mungu alikuleta duniani kuwa raia wa Kanada, yataprogramu maisha yako ili uzaliwe nchini Ghana, wakati Mungu tayari alishakutumia malaika wa kukusaidia katika mambo mema nchini Kanada. Lakini yanapobadilisha mpango wa maisha yako, kila kitu ambacho Mungu alikiprogramu katika maisha yako kitakuwa Kanada wakati wewe ukizaliwa nchini Ghana ambapo hakuna malaika wa kukulinda.
Ndiyo maana unakuta watu wanapata shida na kumuuliza Mungu kama walizaliwa kuhangaika, lakini kihalisia mpango wa maisha yao ulibadilishwa kutokea mwanzo na malaika waovu waliobadilisha mpango wa Mungu na kuprogramu wa kwao. Hivyo, mpango wa Mungu unahitaji kukombolewa.
Watu wengi wanaishi maisha ambayo si ya kwao. Kuishi maisha ya kwako – maisha ambayo Mungu alikupangia ndani ya roho yako kabla hujazaliwa, na kabla roho yako haijazuiwa na mashetani wa angani – kuwa karibu na Mwenyezi Mungu. Kwa Mungu hakuna siri, atakufunulia tu.
No comments:
Post a Comment