Meli ya kwanza kuondoka katika Bandari ya Salina Cruz kusini mwa Meksiko katika Bahari ya Pasifiki ni ‘La Diosa de los Mares’, ‘Mungu wa Bahari’, au ‘Goddess of the Seas’, Tani 6000, iliyoondoka saa tisa kamili usiku kuelekea Miami nchini Marekani; wakati ya mwisho kuondoka ilikuwa CSS (‘Colonia Santita of the Seas’, Tani 10000), na SPD (‘El Silencio Depredador del Profundo’, ‘Mnyama Mtulivu wa Kina Kirefu’, ‘The Silent Predator of the Deep’ – nyambizi ya Panthera Tigrisi), zilizoondoka saa kumi na moja alfajiri kuelekea Gwatemala na Kolombia.
Salina Cruz ni sehemu iliyopo kandokando mwa Bahari ya Pasifiki kusini kabisa mwa Meksiko, na kaskazini-mashariki kwa Reparo Jicara katika jimbo la Oaxaca. Kambi ya Panthera Tigrisi ilijengwa ndani ya Msitu wa Benson Bennett – katika ufuko wa bahari kubwa kuliko zote ulimwenguni, iliyopuliza hewa na kuyumbisha miti anuai juu ya maabara kubwa kuliko zote katika Hemisifia ya Magharibi; ya kokeini, heroini, bangi, eksitasi na hielo ya China na Kolombia. Panthera Tigrisi alikamatwa katika Bahari ya Pasifiki. Kahima Kankiriho alikamatwa katika Msitu wa Benson Bennett.
Kazi ya Vijana wa Tume si kuua, ni kukamata, wataua itakapobidi. Kwa hasira zake, John Murphy alitaka El Tigre (Panthera Tigrisi) auwawe na mwili wake utupwe katikati ya Bahari ya Pasifiki ili dunia imsahau milele – kwa maana ya kupoteza ushahidi wa kaburi lake. Lakini Christoffer Sortevik, Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Tume ya Dunia, aliwatuma wamkamate – ili mahakama ifanye kazi yake.
ReplyDelete