Friday, 11 December 2015

Hotuba

Siku ya Alhamisi tarehe 3 Desemba 2015 nilipokea rasmi tuzo yangu ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika jijini Nairobi nikiwa na washindi wenzangu Anna Samwel Manyanza, Mohammed Khelef Ghassani na Christopher Bundala Budebah. Hiki ni kitu kikubwa sana kutokea katika maisha yangu ya uandishi wa vitabu.

Awali ya yote ningependa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha siku hiyo na kunidhihirishia jibu kwa mara nyingine (baada ya miaka 20 aliponidhihirishia kwa mara ya kwanza) la kwa nini nilizaliwa na nini natakiwa kufanya.

Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika, Kampuni ya Mabati Rolling Mills ya Kenya, Kampuni ya Uchapishaji wa Vitabu ya Kwani Trust ya Kenya na watu wote waliohudhulia sherehe ya tuzo hii katika ukumbi wa Klabu ya Capital ya Nairobi. Ningependa kuwashukuru hao kwa kukifanikisha kitu hiki, kwa ufadhili wao, kwa uenyeji wao na kwa kuacha shughuli zao kuja kutushuhudia sisi tukipata tuzo zetu kwa mpangilio huo.

Ningependa pia kuwashukuru wale wote waliochaguliwa na Mungu kunifikisha katika mafanikio haya ya Tuzo ya Mabati-Cornell; akiwemo Nyamuyengi Maregesi, Amos Nungu na Beredy Malegesi kwa urafiki wao wa kweli.

Mwisho kabisa ningependa kumshukuru bibi yangu, Martha Maregesi, aliyefariki siku 18 kabla ya kutangazwa rasmi kwa tuzo hii huko Nijeria (tarehe 22 Novemba 2014) katika tamasha la vitabu la Ake Arts & Book Festival la Abeokuta, kwa kunifundisha upendo kwa watu na uvumilivu katika maisha. Tuzo hii ni kwa ajili ya bibi yangu. Asanteni sana.

No comments:

Post a Comment

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...