Wednesday, 12 April 2017

Mtoto Mchanga Bila Kujitambua Hutamani Sana Mama Yake Amwambie Neno Zuri Atakalolitumia Baadaye Katika MaishaYake

Watoto hupenda vitu vinavyong’aa ambavyo havijatulia na vilivyopangiliwa vizuri. Hivyo ndivyo macho ya binadamu yalivyo: yana unyevu na yanaakisi mwanga, hayajatulia, na yana rangi kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na kope na vigubiko vya macho ambavyo pia havijatulia.

Mtoto mchanga hasa yule anayeona vizuri huangalia macho pale anapopata nafasi kwa maana ya kuyashangaa. Vilevile, huangalia macho kwa maana ya kupokea molekuli ya maadili au homoni inayorahisisha maisha kutoka kwa mama yake iitwayo ‘oxytocin’. ‘Oxytocin’ husisimua ubongo wa mtoto na kuutayarisha ubongo huo kupokea neno lolote litakalosemwa na mama yake mzazi au mama yake mlezi.

Jicho ni kiungo cha ajabu zaidi kuliko viungo vyote katika mwili wa mwanadamu baada ya ubongo. Jicho moja linatengenezwa na viungo vidogovidogo zaidi ya milioni mbili vinavyofanya kazi kwa pamoja bila kukosea.

Macho yana nguvu ya ajabu. Huu ni wito kwa akina mama wanaonyonyesha: Usizungumze maneno mabaya mtoto wako mchanga anapokuangalia machoni wakati ananyonya ziwa lako. Neno lolote utakalomwambia, zuri au baya, pamoja na kwamba amekuwa akisikia sauti yako kwa miezi kadhaa akiwa tumboni, litajirekodi katika akili yake isiyotambua bila wewe au yeye mwenyewe kujua.

Neno hilo litakuja kumuathiri baadaye atakapokuwa mkubwa. Atakapopevuka, atakapokuwa na uwezo wa kupambanua mambo, atakuwa anaota na kuwaza kile ambacho ulikuwa ukimwambia alipokuwa tumboni, na alipokuwa akinyonya na kukukodolea macho.

Kama ulikuwa ukimwambia mwanao kuwa atakuwa jambazi labda kwa sababu ya fujo zake alipokuwa mdogo, mambo mengi atakayokuwa akiyafikiria au akiyaota atakapopevuka akili ni ya kihalifu. Kwani hayo ndiyo mambo ya kwanza kabisa kujirekodi katika ubongo wake alipokuwa hajitambui.

Lakini kama ulikuwa ukimwambia kuwa atakuwa daktari au mwanasheria, mambo mengi atakayokuwa akiyafikiria au akiyaota ni ya kidaktari au kisheria. Kuna uwezekano mkubwa akawa daktari au mwanasheria baadaye katika maisha yake.

Mwambie mtoto wako maneno mazuri anapokuwa ananyonya na kukuangalia machoni kwa kukukodolea. Maneno utakayomwambia ndiyo yatakayokuwa msingi wa mawazo yake ya baadaye, na ndiyo yatakayoumba maisha yake atakapokuwa mkubwa.

Tengeneza maisha ya mwanao kwa kuongea naye maneno mazuri anapokuwa tumboni mwako, na anapokuwa ananyonya akikuangalia machoni.

Mtoto asipokuangalia machoni wakati ananyonya anaweza kuwa na matatizo ya akili. Heri kumwona daktari mapema.

No comments:

Post a Comment

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...