215. Yesu Kristo hakufa siku ya Ijumaa jioni na kufufuka siku ya Jumapili asubuhi. Alikufa siku ya Jumatano jioni na kukufuka siku ya Jumamosi jioni. Wakati kifo kinamkumba, hakuwa na umri wa miaka 33, alikuwa na umri wa miaka 31. Kama Yesu Kristo alikufa siku ya Ijumaa jioni, na kufufuka siku ya Jumapili asubuhi, hatuna Mwokozi!
Yesu Kristo wa Nazareti ni mtu mashuhuri zaidi kuliko wote kuwahi kukanyaga ardhi ya dunia hii. Alikufa majira ya saa 9 kamili za mchana, siku ya Jumatano, katika kipindi cha demani cha AD 31. Saa chache baadaye, jua lilipokuwa likizama, alilazwa katika kaburi jipya la Yusufu wa Arimathaya. Katika siku ya kawaida ya Sabato, Jumamosi, siku tatu kamili baada ya mazishi yake, Mungu Baba alimfufua Mtoto Wake kwa ajili ya uzima wa milele.
Lakini ninawezaje kuwa na jeuri na hakika kiasi hiki kuhusiana na hizi siku tatu ambazo Yesu Kristo alikaa kaburini mwake?
Litakuwa jambo la kipumbavu kutoa madai mazito kama haya bila kuwa na ushahidi wowote. Tutajuaje kama haya matukio ya muhimu kabisa yalitokea lini, siku gani ya juma, na mwaka gani kabla Mwokozi wetu hajafufuliwa na kupaa kwenda mbinguni?
Matukio haya yameandikwa kwa uwazi kabisa katika maelezo ya kifo na ufufuo wa Yesu katika injili nne (MAMALUYO) ambazo ni Mathayo, Marko, Luka na Yohana. Chini ya uongozi wa Mungu (2 Timotheo 3:16) wanaume hawa waaminifu walirekodi maneno na matendo ya Bwana na Mwokozi wao kwa manufaa ya wanadamu wote duniani kote. Mungu, kama mwandishi halisi wa injili, alitaka maelezo yote muhimu ya maisha ya mwanawe yaandikwe, kama ushahidi juu ya maisha yake ya ukamilifu na ya kafara yake.
Dalili zote, viashiria vyote vya tarehe na nyakati za matukio haya, zimetapakazwa “huku kidogo na huku kidogo” (Isaya 28:10) katika vitabu vyote vya injili. Vipengele vingine vya muhimu kuhusiana na maelezo haya vimetapakazwa hapa na pale miongoni mwa vitabu vingine vya Biblia, kwa kiasi fulani kama vipande vya fumbo la chemshabongo! Vipande mbalimbali vikiwekwa pamoja, na maelezo mwanana ya waandishi wa injili, tutapata muda halisi wa kifo na ufufuo wa Yesu Kristo.
Tunaweza kujua kwa hakika Yesu alikufa lini na alifufuka lini!
Je, tunataka kujua?
Je, ni muhimu kiasi hicho kuwa na uwezo wa kuyajua matukio haya kwa usahihi? Wakristo wamezaliwa na kufa kwa karibu milenia mbili. Je, maarifa haya yalikuwa na umuhimu gani katika wokovu wao? Na je, maarifa haya yana umuhimu wowote katika wokovu?
Labda!
Tarehe hizi zenyewe kama zenyewe zingekuwa na umuhimu mdogo kama zingekuwa hazina uhusiano wa ndani kabisa na ukweli wa kiroho. Lakini Ukristo wa dunia hii umejikita katika imani ya sikukuu zake mbili za muhimu zaidi katika kutambua matukio yaliyotokea kwenye lile juma ambapo Yesu alikufa na kufufuka. Ijumaa Kuu na Jumapili ya Pasaka, zikiwa na lengo la kuadhimisha kumbukumbu ya kifo na ufufuo wa Yesu, zimejengwa juu ya dhana kwamba Mwokozi wetu alisulubiwa siku ya Ijumaa na kufufuka kutoka wafu alfajiri siku ya Jumapili iliyofuata.
“Kwa hiyo?” mtu anaweza kuuliza. “Kuadhimisha sikukuu hizi katika muda maalumu wa mwaka si jambo jema? Je, huko si kumheshimu Kristo? Hapana, si jambo jema, huko si kumheshimu Kristo!
Mungu si wa kudhihakiwa (Wagalatia 6:7)! Katika maneno kadhaa ya Biblia, anasema bila masihara kabisa kwamba yeye ni Mungu mwenye wivu (Kutoka 34:14; Kumbukumbu la Torati 6:4-15) – Yeye si wa kuabudiwa kama mungu mwingine yeyote yule (Kumbukumbu la Torati 12:3-4, 30-31). Alipowaagiza watu wake wateule Israeli kwa njia ya ibada yake, aliwaonya wasiongeze juu ya kile alichokuwa amewapa wala wasipunguze chochote (Kumbukumbu la Torati 4:2; 12:32; angalia pia Ufunuo 22:18-19).
Kwa mfano, angalia hasira yake kuu wakati wana wa Israeli walipojaribu kumwabudu kupitia Ndama wa Dhahabu (Kutoka 32:1-9). Walitangaza kuwa ilikuwa sikukuu ya Bwana (mstali wa 5), lakini Mungu hakulithamini hilo! Alikuwa na hasira kali juu ya ibada ya sanamu za watu, kiasi kwamba alifikiria kuangamiza taifa zima na kuanza upya na familia ya Musa.
Mungu huyohuyo – Yahweh, Bwana wa Agano la Kale – akawa Yesu Kristo! Je, Mwokozi wetu atakubali kuabudiwa kwa namna yoyote ambayo misingi yake imejikita kwenye uongo? Hapana! Na hili kwa vyovyote vile limezingatia mila na desturi zisizo za kibiblia (labda tunaweza kusema za “kipagani”) ambazo zimechukua nafasi ya maadhimisho ya kafara na ushindi wa kishindo wa Yesu Kristo.
Mafundisho mengine ambayo si ya kweli ya Ukristo ambayo hutokana na utambuzi wao wa matukio haya ni “Siku ya Bwana”. Makanisa ya Kikatoliki na Kiprotestanti kote duniani yanaonekana kuwa na nia njema lakini huwadanganya watu kuamini kuwa Kristo alibadili siku ya kupumzika kutoka Sabato kwenda Jumapili. Angewezaje kufanya hivyo? Angeweza kufanya hivyo kwa ufufuo wake!
Iwapo ingeweza kuthibitishwa kuwa Yesu alifufuka kutoka kaburini kwake siku ya Sabato, nini kingetokea katika msingi wa mafundisho haya? Yasingekuwepo tena! Wanateolojia wao wangekuwa na ushahidi mdogo tu wa kimaandishi ambao ungesimamia ukweli wao (1 Wakorintho 16:1-2; Ufunuo 1:10)!
Hakuna mahali popote katika Agano Jipya ambapo sheria ya Sabato imekomeshwa (Kutoka 31:12-17), kwani Mungu alianzisha Sabato kwa ajili ya wanadamu wote (Marko 2:27). Kinyume cha hapo, Yesu aliitunza (Luka 4:16), Paulo aliitunza (Matendo 17:2) na Wamataifa waliitunza pia (Matendo 13:42-44; 16:13)! Mwandishi wa Waebrania anaandika bila kificho, “Basi, imesalia raha ya Sabato kwa watu wa Mungu” (Waebrania 4:9).
Hivyo tunaweza kuona vizuri kabisa kwamba tarehe sahihi kwa ajili ya kifo na ufufuo wa Yesu Kristo vinaweza kuwa na umuhimu wa pekee katika wokovu wetu.
Ishara
Kama Yesu alifufuka kutoka kaburini kwake siku ya Jumapili asubuhi baada ya kuwa ameuwawa siku ya Ijumaa jioni, hatuna Mwokozi!
Ni kweli! Yesu alitoa ishara moja tu ya Umasihi wake:
“Hapo baadhi ya waandishi na Mafarisayo wakamjibu, wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako. Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona. Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi.” (Mathayo 12:38-40)
Kwa nini Mafarisayo walimwomba ishara? Jibu linaonekana mara tu baada ya wao kuuliza swali. Yesu alikuwa akihubiri kwamba “mti hujulikana kwa matunda yake” (mstali wa 33) hivyo, kihalisia, Wayahudi hawa walikuwa wakimwomba Yesu ishara kuthibitisha kama alikuwa Masihi! Walitaka kuona tunda gani angelitoa!
Harakaharaka Yesu aliwakemea kwa sababu hawakuelewa alichokuwa akikimaanisha (mistali ya 41-42)! Ili waridhike, walitaka kuona muujiza, lakini tunda ambalo Yesu alimaanisha ni toba, matendo mema na ukuaji wa kiroho. Alitaka baadaye waje waone matunda ya uchungaji wake.
Hivyo anasema, kwa ufafanuzi zaidi, “Ishara pekee ambayo itathibitisha kwa ukamilifu ukweli wa ujumbe wangu ni moja tu ambayo sitakuwa na uwezo nayo. Nitakuwa kaburini siku tatu kamili (yaani mchana 3 na usiku 3). Nitakuwa nimekufa. Nitakuwa sina uwezo wa kujifufua mwenyewe. Hivyo kama Mungu Baba atanifufua baada ya hizo siku tatu, itathibitika vizuri zaidi kama mimi ni Masihi.”
Yesu alitoa ishara hiyohiyo katika maeneo mengine aliyotembelea na kwa nyakati na watu tofauti, mara zote akitumia maneno yaleyale. Katika Yohana 2:19-21 anasema, “’Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha.’… Lakini alikuwa akizungumzia hekalu la mwili wake.”
Kwa wanafunzi wake anasema, “Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuwawa, baada ya siku tatu atafufuka (Marko 9:31; 10:33-34; Mathayo 17:22-23; 20:18-19; Luka 9:22).
Marko 8:31 inazungumzia kipindi hicho kwa njia ya tofauti kidogo: “Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuwawa, na baada ya siku tatu kufufuka.” Hata makuhani wakuu na Mafarisayo waliikumbuka ishara yake. Wanamwambia Pilato baada ya kusulubiwa kwa Yesu, “Mheshimiwa, tunakumbuka, wakati bado akiwa hai, jinsi yule mwongo [yaani Yesu] alivyosema, ‘baada ya siku tatu nitafufuka’” (Mathayo 27:63).
Nini Maana ya Siku Tatu?
Je, tunaweza kupata siku tatu kati ya Ijumaa jioni na Jumapili asubuhi? Imani ya wengi miongoni mwa ‘Wakristo’ ni kwamba Kristo alimaanisha ‘sehemu’ ya hizo siku tatu: yaani sehemu ya Ijumaa, siku nzima ya Jumamosi, na sehemu ya Jumapili. Lakini je, hivyo ndivyo Yesu alivyosema?
Mojawapo ya sheria muhimu zaidi za tafsiri ya kibiblia ni kuruhusu Biblia ijitafsiri yenyewe. Mara nyingi Biblia huelezea ishara zake na hufafanua vigezo na masharti yake. Je, kuna tafsiri yoyote ya kibiblia ya nini maana ya ‘siku’ na ‘usiku’? Ndiyo, ipo!
Yesu mwenyewe anatoa ufafanuzi katika Yohana 11:9-10:
“Je! Saa za mchana si kumi na mbili? Mtu akienda mchana hajikwai; kwa sababu aiona nuru ya ulimwengu huu. Bali akienda usiku hujikwaa; kwa sababu nuru haimo ndani yake.”
Maana ya wazi ni kwamba Yesu alitambua saa kumi na mbili za mchana kuunda ‘siku’, na saa zingine kumi na mbili za giza zilizofuata akaziita ‘usiku’. Hivyo siku tatu na usiku tatu zitakuwa zimeundwa kwa vipindi sita vya saa kumi na mbili au saa 72.
Kusema ukweli hii ni sawa na njia ambayo Mungu anatumia katika Agano la Kale, katika sura ya kwanza kabisa ya Biblia! “Mungu akaiita nuru Mchana, na giza akaliita Usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku moja … Hivyo jioni na asubuhi zikawa siku ya pili … Hivyo jioni na asubuhi zikawa siku ya tatu.” (Mwanzo 1:5, 8, 13). Hapo siku tatu na usiku tatu zimefafanuliwa kwa kiasi cha kila mtu kuelewa!
Lakini vipi kuhusiana na ishara ya Yona? Nabii Yona alikuwa katika tumbo la samaki mkubwa kwa saa 72 kamili? Yona 1:17 inasema, “Bwana akaweka tayari samaki mkubwa ili ammeze Yona, naye Yona akawa ndani ya tumbo la samaki yule muda wa siku tatu, mchana na usiku.” Nahau ya Kihebrania ya ‘Siku Tatu’ inaweza kutumika kwenye sehemu ya siku tatu (na hata ya miaka): lakini si wakati neno ‘usiku’ linapoongezwa. Kwa kuongeza neno ‘usiku’, nahau hiyo inakuwa bayana, ile dhana ya ‘sehemu’ ya siku ikiondoka!
Nahau tofautitofauti alizozitumia Kristo zinatusaidia kujua maana halisi ya nahau ya ‘Siku Tatu’ kwa mapana zaidi. Tayari tunajua ‘siku tatu na usiku tatu’ zinamaanisha kipindi cha saa 72. Lakini vipi kuhusu nahau zingine? Je, nazo zina maana sawa?
Yesu alisema angefufuka “siku ya tatu.” Hii ina maana kipindi hicho kingepungua na kuwa si chini ya saa 48 na si zaidi ya saa 72 kutokea siku alipozikwa.
Lakini vilevile alisema “katika kipindi cha siku tatu” angefufuka. Kikomo cha muda aliokaa kaburini kisingeweza kuwa zaidi ya saa 72.
Mara nyingine mbili inasemekana ya kuwa angefufuka “baada ya siku tatu”, ikimaanisha lazima angekuwa ndani ya kaburi kwa angalau saa 72 bila kupunguza hata sekunde moja!
Tunapovikusanya vigezo vyote hivi, tunaweza kufikia hitimisho moja tu la hakika: Yesu Kristo alikuwa ndani ya kaburi la Yusufu wa Arimathaya kwa saa 72 kamili! Kama alifufuliwa kabla au baada ya muda huo, hatuna Mwokozi kwa sababu ishara pekee aliyotoa ingeshindwa kutimia! Asingekuwa mkweli!
Lakini tunayo hakika kwamba “Maandiko hayawezi kutanguka” (Yohana 10:35). Kile Mungu anachokitabiri lazima kitimie (Isaya 46:9-11). Kwa maelezo haya, neno lake lilitimia kama lilivyotabiriwa!
Yesu Kristo Alizikwa Muda Gani wa Siku?
Sasa kwa kuwa tunajua Yesu alilala mauti kaburini kwake kwa saa 72, tunaweza kuondokana na jadi ya Ijumaa Kuu na Jumapili ya Pasaka. Ni jambo ambalo haliwezekani kuweka siku tatu zenye saa 24 kila moja kati ya Ijumaa jioni na Jumapili asubuhi.
Hii jadi au mila – ufufuo wa alfajiri – ina msingi wowote katika ukweli? Kama haina, ni muda gani wa siku ambao Yesu alifufuka?
Mathayo, Marko na Luka wana jibu mahususi kuhusu muda ambao Yesu alikufa. Yohana anaelezea tu muda ambao Yesu alisulubiwa (Yohana 19:14-16). Luka anatoa taarifa sahihi zaidi:
“Hapo ilikuwa yapata saa sita [Yesu alipokuwa akisulubiwa], kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu. Alipokwisha kusema hayo alikata roho.” (Luka 23:44-47)
Yesu alining’inia msalabani kwa saa tatu kabla ya kifo chake saa tisa mchana (Marko 15:34; angalia pia Mathayo 27:46). Kwa kuwa walikuwa wakitumia kanuni ya Kihebrania ya kuhesabu saa za siku kuanzia asubuhi, waandishi wa injili wanaonyesha kuwa Yesu alisulubiwa majira ya saa sita mchana na kukata roho majira ya saa tisa mchana. Wamekubaliana kwa kiwango cha hali ya juu kuhusiana na hili.
Marko anaendelea:
“Hata ikiisha kuwa jioni, kwa sababu ni Maandalio, ndiyo siku iliyo kabla ya sabato, akaenda Yusufu, mtu wa Arimathaya, mstahiki, mtu wa baraza ya mashauri, naye mwenyewe anautazamia ufalme wa Mungu; akafanya ujasiri, akaingia mbele ya Pilato akauomba mwili wake Yesu … Hata alipokwisha kupata hakika kwa yule akida, alimpa Yusufu yule maiti. Naye akanunua sanda ya kitani, akamteremsha, akamfungia ile sanda, akamweka katika kaburi lililochongwa mwambani; akavingirisha jiwe mbele ya mlango wa kaburi.” (Marko 15:42-43, 45-46)
Pointi kadhaa zinajitokeza katika ujumbe huu:
Jioni ilikuwa ikikaribia – Yusufu alikuwa na kadiri ya saa tatu tu kabla ya machweo, muda ambao Sabato ingeingia. Kazi ya kuandaa na kutumia manukato kwa ajili ya mazishi ilihitaji kazi nyingine ya ziada, ambayo imekatazwa kabisa katika siku ya Sabato (Kutoka 20:8-10). Zaidi ya hayo, Kumbukumbu la Torati 21:22-23 inadai kwamba mhalifu aliyeuwawa lazima azikwe kabla giza halijaingia, na sheria za Wayahudi za kipindi hicho zilitaka miili yote izikwe kabla ya Sabato au kabla ya sikukuu nyingine yoyote ile (Yohana 19:31).
Kabla hajauteremsha mwili wa Yesu, Yusufu alihitaji kwenda kwa Pilato kuomba ruhusa. Mwanzoni Pilato hakuamini kama Yesu alikufa kwa haraka hivyo, hivyo alimwita kamanda wa kitengo cha mateso kumthibitishia (Marko 15:44-45). Kuchelewa huku kuliweza kuchukua angalau nusu saa.
Baada ya kuruhusiwa kuchukua mwili, Yusufu alikwenda dukani na kununua meta kadhaa za kitani safi kwa ajili ya kumfunika Yesu. Kwa msaada wa Nikodemo, Yusufu aliuteremsha mwili, akauzungushia sanda – pamoja na mchanganyiko wa manemane na uudi, yapata ratili mia – na kuuweka ndani ya kaburi (Yohana 19:39-41).
Pamoja na shughuli yote hii na kazi yote hii iliyofanyika katika maeneo mbalimbali, Yusufu na Nikodemo lazima walikuwa wamebakiwa na muda mchache sana wa mwanga wa jua walipofanikiwa kuviringisha jiwe juu ya mlango wa kaburi. Tena, katika pointi hii fikra zote zinafanana; machweo yalishakaribia mno (Mathayo 27:57; Marko 15:42; Luka 23:54; Yohana 19:31).
Hakuna mtu anapinga kwamba Yesu alilazwa “katika moyo wa nchi” katika kipindi cha machweo. Ikiwa, kama nilivyoonyesha, Yesu alikuwa kaburini kwa saa 72 kamili, kadhalika alifufuliwa jioni – si asubuhi!
Siku ya Maandalizi ya Pasaka
Waandishi wote wanne wa injili wanataja kuwa Yesu alijaribiwa, alitiwa hatiani, alisulubiwa na alizikwa katika siku ya maandalizi. Bila ufafanuzi mwingine wowote, mtu anaweza kudhani ya kuwa walimaanisha Ijumaa, siku ya maandalizi ya kila juma kabla ya Sabato. Lakini siku zingine pia zinaweza kuchukuliwa kama siku za maandalizi?
Naam, hakika! Mungu mwenyewe alitoa maelekezo kuhusu matumizi ya siku ya maandalizi kwa wana wa Israeli kabla ya kufika Mlima Sinai (Kutoka 16:23). Baadaye Wayahudi walilichukulia hilo kama jambo la muhimu sana kiasi kwamba walihakikisha kuwa kila siku takatifu, ambapo Sabato ni miongoni mwazo, ilitanguliwa na siku ya maandalizi. Kwa kuwa siku takatifu inaweza kutokea katika siku yoyote ya juma, siku ya maandalizi inaweza kutokea katika siku yoyote ya juma hali kadhalika.
Hii ni muhimu sana kwa Pasaka. Si tu kwamba Pasaka ni tamasha linalojitegemea, lakini kadhalika linatumika kama siku ya maandalizi kwa ajili ya siku takatifu, siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mkate Usiotiwa Chachu. Kwa mujibu wa hesabu za kalenda ya Kihebrania, Pasaka inaweza kuangukia siku ya Jumatatu, Jumatano, Ijumaa au Sabato.
Ni wazi kuwa Mwokozi wetu Yesu Kristo alisulubiwa katika siku ya Pasaka (Mathayo 26:2). Hivyo, ilikuwa katika moja ya siku hizi za juma ambapo Yesu aliuwawa na kuzikwa.
Lakini Sabato inayoongelewa ilikuwa ni ile ya kila juma au mwaka, siku takatifu ya Sabato? Biblia inatuambia nini kuhusiana na hili?
Yohana anaandika, “Nayo ilikuwa Maandalio ya Pasaka” (Yohana 19:14). Neno “Pasaka” kwa maana hii linahitaji maelezo. Wakati fulani kabla ya siku ya Kristo, Wayahudi walishaanza kuiita siku ya Pasaka na siku saba za Sikukuu ya Mkate Usiotiwa Chachu zilizofuata (Mambo ya Walawi 23:6-8) kwa jina moja la “Pasaka”. Hili limesababisha mkanganyiko mkubwa sana kwa wale ambao si Wayahudi, hasa wanaposoma taarifa za hii Pasaka tuliyoizoea.
Lakini Yohana 19:31 inatuondolea dukuduku:
“Basi Wayahudi, kwa sababu ni Maandalio, miili isikae juu ya misalaba siku ya sabato, (maana sabato ile ilikuwa siku kubwa) …”!
Hivyo, bila shaka, Yesu alisulubiwa siku ya Pasaka, Nisan 14, na Sabato iliyofuata ilikuwa siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mkate Usiotiwa Chachu, siku takatifu ya mwaka, siku kubwa. Hii inaleta maana, kwa kuwa mtume Paulo anasema katika 1 Wakorintho 5:7 (“… Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo.”
Siku Gani ya Juma?
Kila mwaka kadiri Pasaka inapokaribia, makanisa mara nyingi hutoa kauli mbiu kwenye mabango, mahema, ishara, magazeti na televisheni, “Amefufuka!” Pengine nitapatia nikibashiri kwamba wengi wa waumini wa makanisa haya hawajawahi kusoma kifungu cha maandiko ambako hii nukuu inatoka na vifungu vingine vinavyofanana na hicho katika injili zingine tatu.
Hatupaswi kuikubali mitazamo ya jadi kirahisi hivyo; na kupata ukweli, lazima turudi kwenye mlolongo wa hadithi. Waandishi watatu wa injili (Mathayo, Marko na Luka) wanarekodi kuwa Yusufu na Nikodemo walikuwa na hadhara walipokuwa wakiutayarisha mwili wa Yesu. “Na wale wanawake waliokuja naye toka Galilaya, walifuata, wakaliona kaburi, na jinsi mwili wake ulivyowekwa (Luka 23:55).
Tukiendelea na Injili ya Luka tutadhani tunajua ya kuwa wale wanawake walikimbilia kwenye duka la manukato, ambapo walinunua manukato na mafuta, wakayatayarisha kisha wakapumzika siku ya Sabato (mstari wa 56). Lakini hatutakuwa sahihi!
Tunapaswa kwenda katika kitabu cha Marko 16:1 kupata taarifa muhimu:
“Hata sabato ilipokwisha kupita, Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yakobo, na Salome walinunua manukato wapate kwenda kumpaka.” Kimantiki, mlolongo wa matukio hauwezi kuwa vinginevyo. Kama Yusufu alikuwa na muda mchache tu kuuzika mwili wa Yesu kabla jua halijazama, wale wanawake wangebakiwa na muda kiasi gani kufanya kile walichohitaji kufanya kabla ya Sabato?
Hivyo taarifa hizi za injili zinazowiana huonyesha kwamba Yusufu alipomteremsha Yesu kutoka msalabani, wanawake walimfuata kuona wapi wangeulaza mwili. Kisha walirudi katika makazi yao na kuikaribisha siku takatifu ya Sabato, siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mkate Usiotiwa Chachu. Siku moja baada ya siku takatifu, walikwenda dukani, wakanunua manukato na mafuta, wakarudi nayo kwenye makazi yao, wakayatayarisha kwa ajili ya kuyatumia kwenye mwili na “walipumzika siku ya Sabato kulingana na amri (Luka23:56). Kulikuwa na Sabato mbili ndani ya kipindi hicho cha saa 72!
Wanawake hawa walileta manukato na kuyatayarisha “Sabato ilipokuwa imepita” na kisha “wakapumzika siku ya Sabato”! Walipumzika mara mbili: Mara ya kwanza katika “siku kubwa” na mara ya pili katika Sabato ya kawaida ya kila juma siku mbili baadaye.
Hii inaweza kumaanisha jambo moja tu! Yesu alisulubiwa na kuzikwa siku ya Jumatano, siku takatifu ikawa Alhamisi, wanawake wakatayarisha manukato siku ya Ijumaa na Mwokozi wetu akafufuliwa machweo siku ya Sabato siku ilipokuwa ikimalizika! Matukio haya hayawezi kukokotolewa kwa namna nyingine yoyote ile kwa ushahidi huu wa wazi kabisa unaotolewa na maandiko matakatifu.
Mathayo 28:1 ina ushahidi mwingine kuhusiana na Sabato mbili zilizotokea katika lile juma moja. Hata hivyo, wafasiri wa Biblia, waliochanganywa na maneno ya Kigiriki ya fungu hili, wameendelea kulitafsiri ndivyo sivyo. Mathayo anasema, “Hata Sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma …” Hata hivyo, maneno ya maandishi haya ya awali yanasema, “baada ya Sabato (hiyo Sabato ikiwa katika wingi).” Yaani, “After the Sabbaths”.
Ushahidi Zaidi wa Kusulubiwa Jumatano
Nabii Danieli alipokea unabii mzuri sana kutoka kwa Malaika Mkuu Gabrieli katika Danieli 9:24-27. Kifungu hiki hujulikana kama Unabii wa Majuma Sabini, kwani Gabrieli anatoa muda wa majuma sabini wa kuja kwa Masihi. Anagawa majuma sitini na tisa ya mwanzo katika vipindi viwili, cha kwanza cha majuma saba na cha pili cha majuma sitini na mawili:
“Na baada ya yale majuma sitini na mawili, Masihi atakataliwa mbali … Naye atafanya agano thabiti na watu wengi kwa muda wa juma moja [juma la sabini]; na kwa nusu ya juma hilo ataikomesha sadaka na dhabihu.”
Unabii huu unaonyesha kuwa Masihi atakufa, “lakini si kwa ajili yake.” Hiyo inaendana kabisa na kifo cha kujitolea cha Yesu Kristo! Alijitolea maisha yake ili atukomboe kutoka katika utumwa wetu wa dhambi na mauti (Wagalatia 1:3-5; Waefeso 2:1).
Zaidi ya hapo, unabii unasema angefanya “agano thabiti na watu wengi.”
Sivyo hivyo alivyofanya? Kwani hakuwa mjumbe wa Agano Jipya na bora zaidi (Waebrania 9:15)? Alipoanzisha alama mpya kwa ajili ya Pasaka, Yesu anasema kuhusu mvinyo, “Kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi” (Mathayo 26:28; angalia pia Marko 14:24).
Kisha Gabrieli akatabiri kwamba Masihi atasitisha haja ya matambiko ya kafara za wanyama na sadaka. Mwandishi wa Waebrania anatamka waziwazi, “Maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi (Waebrania 10:4). Dhabihu ya Kristo ilikuwa na ufanisi zaidi: “Wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele (Waebrania 9:12).
Malaika anasema Masihi atalikamilisha hili “katikati ya juma.” Kwa kweli, maana yake ya msingi inahusu katikati ya juma la sabini, au kihalisia, miaka mitatu na nusu, muda halisi wa huduma ya Yesu.
Hata hivyo, kama tulivyoona, Mungu hutimiza unabii wake kikamilifu. Si tu kwamba huduma ya Yesu ilifanyika kwa miaka mitatu na nusu, lakini pia alikufa siku ya Jumatano, katikati halisi ya juma!
Unabii Ulibaini Hata Mwaka
Kinachofurahisha zaidi kuhusiana na Unabii wa Majuma Sabini unaoendelea kupuuzwa, si tu kwamba unatupa mwangaza juu ya kifo cha Yesu, unaonyesha pia mwaka wa kifo chake! Bila shaka, si rahisi kama kuhakikisha jambo kitabuni, lakini zipo taarifa za kutosha kugundua mwaka bila kukosea.
Gabrieli anasema, “Basi ujue na kufahamu, ya kuwa tangu kuwekwa amri ya kuutengeneza na kuujenga upya mji wa Yerusalemu hata zamani zake Masihi aliye Mkuu, kutakuwa na majuma saba; na katika majuma sitini na mawili utajengwa tena pamoja na njia kuu zake na handaki, naam, katika nyakati za taabu (Danieli 9:25). Pointi ya mwisho hapo iko wazi: Kujifunua kwa Masihi. Lakini pointi ya mwanzo inasemaje?
Wanahistoria wanazijua angalau amri nne zilizotolewa na watawala wa Kiajemi “kurejesha na kuijenga upya Yerusalemu.” Koreshi alitoa moja mwaka 538 BC, Dario wa Kwanza alitoa nyingine mwaka 520 BC na Artashasta wa Kwanza akatoa mbili: moja mwaka 457 BC na nyingine mwaka 444 BC. Amri ipi ni sahihi?
Zote zingeweza kutosheleza maelezo ya Danieli 9:25. Zote zinahusika na kuurejesha mji wa Yerusalemu katika nafasi yake ya mwanzo kama mji mkuu wa kidini wa Wayahudi na kama kitovu cha biashara. Lakini ni amri moja tu inayotosheleza kigingi cha muda, na hii inajionyesha wazi pale tunapokokotoa fumbo la majuma sabini.
Lazima tufanye hesabu kidogo kupata hitimisho la kila moja ya amri hizi. Neno “majuma sabini” linamaanisha “saba sabini,” na kanuni ya siku moja-mwaka mmoja lazima ifanye kazi hapa (Hesabu 14:34; Ezekieli 4:4-6). Ni lazima tuzidishe majuma sabini mara miaka saba iliyomo ndani ya juma moja la miaka, ambayo huleta jibu la miaka 490. Gabrieli, hata hivyo, anasema ni saba sitini na tisa tu “hadi kufika kwa Masihi aliye Mkuu.” Hivyo, 69 X 7 = miaka 483.
Tukijumlisha miaka 483 kwa kila tarehe ya amri tunapata nini? (Kumbuka kuongeza mwaka mmoja kufidia mwaka wa 0).
538 BC + 483 = 55 BC. Hakuna tukio la muhimu la kibiblia.
520 BC + 483 = 37 BC. Hakuna tukio la muhimu la kibiblia.
457 BC + 483 = AD 27. Yesu anabatizwa na kuanza rasmi huduma yake ya uchungaji.
444 BC + 483 = AD 40. Hakuna tukio la muhimu la kibiblia.
Mungu aliturahisishia! Tuna jambo moja tu la kufanya!
Danieli 9:26-27 inasema wazi kabisa kwamba Masihi angefanya kazi kwa miaka mitatu na nusu, nusu ya juma, kabla ya “kuikomesha sadaka na dhabihu.” Tunapojumlisha miaka mitatu na nusu kwa AD 27, tunagundua ya kuwa uchungaji wa Yesu ulikoma mnamo mwaka AD 31, mwaka wa kusulubiwa na kufufuliwa kwa Yesu!
Kwa hiyo, tunaona injili zote nne zinathibitisha huduma ya miaka mitatu na nusu iliyotabiriwa katika Utabiri wa Majuma Sabini. Hii hatimaye inathibitisha kwamba Yesu alikufa mnamo mwaka wa AD 31 wakati – kulingana na kalenda ya Kihebrania – Pasaka iliangukia siku ya Jumatano, si Ijumaa!
No comments:
Post a Comment