Monday, 22 June 2015

Hewa

142. Mafanikio unapaswa kuyataka kama unavyotaka hewa. Hewa ni kitu cha muhimu zaidi kuliko kitu kingine chochote kile ulimwenguni. Ukipewa hewa au shilingi bilioni kumi chagua hewa.

http://www.facebook.com/koloniasantita

3 comments:

  1. Jamaa mmoja, Meku Kikuyu, alimfuata mchungaji wa mojawapo ya makanisa ya kiroho ya Kimara, Sumbo Ambwene – aliyekuwa akijulikana sana kwa waumini wake kama mzee mwenye hekima, na kwa wapinzani wake kama mchungaji aliyekuwa akihubiri kwa jina la Yesu na kuokoa kwa nguvu za giza – kuomba ushauri kuhusiana na maisha. Meku, aliyekuwa na mke na watoto wawili, alihitaji kuonana na mchungaji ili amuombe hekima ya jinsi gani atafanikiwa katika maisha yake. Mchungaji alimuuliza Meku:

    "Haya mafanikio unayataka kwa kiasi gani?"

    "Mafanikio haya mchungaji, nayataka kwa gharama yoyote!"

    "Kwa nini unayataka hivyo?"

    "Nimeshajitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu wote, lakini nimeshindwa."

    "Kwa nini umekuja kwangu?"

    "Nimekuja kwako kwa sababu ya shuhuda za watu wengi ambao umeshawasaidia."

    "Kufanikiwa katika maisha lazima uwe tayari kufa kwa ajili ya kitu unachoweza kuwa. Uko tayari kufa kwa ajili ya kitu unachoweza kuwa?"

    "Niko tayari kwa chochote!"

    "Uko tayari kwa chochote."

    "Ndiyo, mchungaji."

    "Nimekuelewa. Sasa fanya hivi, nenda nyumbani kwako kashauriane na mkeo. Halafu kesho Jumapili, baada ya ibada, tuonane ofisini kwangu. Sawa?"

    "Sawa, mtumishi wa Bwana."
    Kesho yake baada ya ibada Meku alionana tena na Mchungaji Ambwene ofisini kwa mchungaji, kama walivyokuwa wameongea jana yake.

    "Mchungaji, niliongea na mke wangu na tulishauriana kwamba niko tayari kufanya chochote ili mimi na familia yangu tuishi vizuri."

    "Vyema," mchungaji alijibu akimwangalia Meku kwa makini sana usoni. Halafu akaendelea, "Leo usiku una ratiba gani?"

    "Leo usiku, nitakuwepo tu mchungaji."

    "Basi tuonane saa tisa usiku baharini. Tuonane pale Coco Beach, unapajua?"

    Meku alisita kwa muda, halafu akapata cha kusema, "Sawa mchungaji, napajua. Nije peke yangu?"

    "Njoo peke yako. Ukija utakuta nimeshafika, utakuta gari yangu imepaki mchangani."

    "Sawa mchungaji, asante."

    Mchungaji hakumjibu kitu. Badala yake alimwangalia kwa makini usoni, halafu akampa ishara ya kuondoka, na jamaa akaondoka.

    Usiku wa siku hiyo Meku alikuwa na mabishano makali sana na mkewe kuhusu safari ya Coco Beach ya saa tisa usiku. Wote – Meku na Manka – waliamini mchungaji wao alikuwa mchawi, au alikuwa mganga wa kienyeji. Labda ndiyo maana watu wengi walihisi ni wakala wa Shetani. Hata hivyo, ilipofika saa saba usiku walikubali liwalo na liwe – kwani kwa kiasi fulani walimwamini mchungaji wao. Walikuwa hawajawahi kushuhudia kitu chochote kibaya kutoka kwake, ijapokuwa watu wengi walikuwa wakimsema vibaya, kama vile nabii wa uongo na mambo mengine kama hayo. Waliamua Meku aondoke kwenda Coco Beach, lakini kwa makubaliano ya kuwa ikifika saa kumi alfajiri Manka hajasikia chochote kutoka kwake, Manka ampigie; na kama simu yake haipatikani Manka aende polisi moja kwa moja akatoe taarifa. Meku alikuwa na gari. Alichukua gari yake na kuondoka, saa nane na nusu, kuelekea Coco Beach huko Oysterbay.

    ReplyDelete
  2. Ufuko wa Bahari wa Coco Beach kipindi hicho haukuwa shwari hata kidogo. Upepo ulikuwa ukivuma kwa kasi, na mawimbi ya bahari yalikuwa mengi na makubwa kiasi cha kuogofya kabisa.

    Meku alipofika, Coco Beach, aliona gari la mchungaji kwa mbali limeegeshwa. Hivyo akaendesha yake (huku akitetemeka) mpaka jirani na la mchungaji; halafu akazima injini, na kutoka nje. Meku hakuona mtu. Lakini baada ya sekunde kadhaa aliona mtu kwa mbali amevaa mavazi meupe. Kuona vizuri akakuta ni mchungaji, aliyekuwa aking’ang’ana kumwita kwa ishara ya mkono. Mchungaji alikuwa amevaa suti nyeupe ya mikono mifupi, shati jeusi la mikono mifupi, viatu vyeupe vya sandarusi na saa ndogo ya kidijitali. Hakuwa na tai, wala soksi. Meku alimfikia mchungaji wake.

    "Shikamoo, mchungaji."

    "Marahaba, mbona umechelewa?"

    "Nimechelewa dakika chache tu mchungaji, niwie radhi."

    "Umeshindwa jaribio la kwanza. Sasa, nakuuliza kwa mara ya nyingine: Uko tayari kufa kwa ajili ya kitu unachoweza kuwa?"

    "Niko tayari, mzee!" Meku alijibu huku akitetemeka.

    "OK, twende zetu."

    "Wapi?"

    "Nifuate ninakokwenda."

    Meku, huku akitetemeka na kulia, alimfuata Mchungaji Ambwene mpaka majini. Mchungaji akiwa na nguo zake na viatu vyake na saa, akakanyaga maji na kuendelea kutembea kuelekea katika kina kirefu. Meku kuona hivyo akasita na kuanza kukemea kwa jina la Yesu kwa nguvu zake zote. Mchungaji, alivyoona hivyo, naye akaanza kukemea kwa jina la Yesu mpaka Meku akanyamaza – bila hata kusema Amina.

    "Usiwe mpumbavu, njoo!" mchungaji alimsihi.

    Huku akilia kwa sauti, Meku alikanyaga maji na nguo na viatu vyake na kumfuata Mchungaji Ambwene katika maji ya kiunoni.

    "Umesema uko tayari kwa chochote, sasa unafanya nini?"

    "Niko tayari, mchungaji."

    "Acha upumbavu."

    Waliendelea kutembea mchungaji mbele Meku nyuma mpaka maji ya shingoni, ambapo mchungaji alisimama na kumsihi Meku amfuate mpaka alipokuwa amesimama yeye. Meku alifika.

    "OK, nakuuliza tena kwa mara ya mwisho: Uko tayari kufa kwa ajili ya kitu unachoweza kuwa?"

    Mawimbi yalizidi kuwa makubwa, na wakati mwingine yalikuwa yakiwafunika, na upepo ulikuwa mkali sana.

    "Niko tayari, mchungaji." Meku alikubali yote.

    "OK, geuka, angalia huko tulikotokea."

    Meku, alipogeuka tu, kitu kibaya sana kilitokea katika maisha yake! Mchungaji alibadilika ghafla. Alipandisha hasira na kurusha mikono yake hewani! Halafu, huku Meku akiwa amempa mgongo, akamkaba muumini wake shingo kwa nguvu zake zote na kumzamisha majini! Ndani ya maji mtu huzimia baada ya dakika nne na hufa baada ya dakika saba. Zilipofika dakika tatu na nusu, mchungaji alimuibua Meku kutoka majini na kumpiga kofi. Meku akapata fahamu. Alipopata fahamu vizuri, alimwangalia mchungaji na kuendelea kulia. Lakini mchungaji akatabasamu na kumwambia kitu:

    "Ulipokuwa chini ya maji, kitu gani ulikitaka zaidi?"

    "Hewa!" Meku akajibu harakaharaka, huku akitetemeka.

    "Ungepewa hewa au shilingi bilioni kumi ungechagua nini?"

    "Ningechagua hewa!"

    "OK, twende zetu nyumbani."

    Mafanikio unapaswa kuyataka kama unavyotaka hewa. Miaka miwili baada ya tukio la Coco Beach, Meku alifanikiwa sana katika maisha yake. Aliendelea kulitangaza jina la mchungaji wake kama nabii wa kweli kutoka kwa Mungu.

    ReplyDelete
  3. Ukiambiwa leo kwamba ukishindwa mtihani utafukuzwa kazi, utafanya kila linalowezekana kushinda mtihani. Shauku utakayokuwa nayo kupata hewa, ndiyo utakayokuwa nayo kushinda mtihani.

    ReplyDelete

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu. ...